Nape ataka mashirika ya Posta Tanzania na Kenya kufanya biashara kidigitali
Muktasari:
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameyataka mashirika ya Posta Tanzania na Kenya kuhakikisha wanafanya biashara ya usafirishaji kwa njia ya kidigitali zenye kukidhi vigezo vya kimataifa lengo likiwa kuwavutia wananchi wa nchi hizo kufanya biashara na mashirika hayo.
Arusha. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameyataka mashirika ya Posta Tanzania na Kenya kuhakikisha wanafanya biashara ya usafirishaji kwa njia ya kidigitali zenye kukidhi vigezo vya kimataifa lengo likiwa kuwavutia wananchi wa nchi hizo kufanya biashara na mashirika hayo.
Hayo yamesemwa leo Novemba 1 jijini Arusha na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Kundo Mathew kwa niaba ya Waziri Nape katika hafla ya uzinduzi wa biashara ya kuvuka mpaka kwa njia ya kidigitali kati ya Tanzania na Kenya iliyofanyika katika mpaka wa Namanga.
Amesema kuwa,uwepo wa biashara hiyo kwa nchi hizo utabadilisha muundo mzima wa Kidigital katika kufanya usafirishaji wa vifurushi hivyo kwa wateja wake na kuwafikia ndani ya muda sambamba na kuokoa gharama zilizokuwepo hapo awali.
Nape amesema kuwa, uwepo wa mfumo huo utaongeza fursa za ajira kwa vijana walio wengi kwani kwa kufanya hivyo wanaendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
"Niwaombe sana muendelee kuwa wabunifu zaidi ili kuondoa usumbufu uliokuwepo awali kutokana na mzunguko mrefu uliokuwepo wa kufikiwa na huduma hizo. Nawaomba sana mashirika yote mawili muendelee kupata uzoefu zaidi kutoka nchi zingine sambamba na kuiga yale mazuri yaliyopo katika nchi zingine,"amesema.
Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macris Mbodo amesema kuwa, lengo la uzinduzi wa biashara ya kuvuka mpakani (Cross Border Business) kati ya Tanzania na Kenya ni kurahisisha utoaji wa huduma za usafirishaji wa vifurushi, vibeto na mizigo kwa wananchi wake na kuweza kuondokana na changamoto mbalimbali.
Mbodo amesema kuwa, zamani ilikuwa inawalazimu mizigo kwenda hadi jijini Da es Salaam ambapo ilikuwa inachukua muda mrefu na gharama pia, ila kwa sasa hivi itawasaidia kurahisisha gharama na kuweza kuchukua mizigo hiyo hapa hapa karibu ndani ya muda mfupi.
"Rais Samia Suluhu Hassan amefungua nchi yetu kwa kuweza kufanya biashara mbalimbali hivyo tumeona tuunge mkono jitihada za serikali kwa kuimarisha usafirishaji wa vifurushi mipakani na kuweza kuokoa gharama zilizokuwepo hapo awali na tumejipanga kuhakikisha huduma zetu zinawafikia wananchi waliopo na sio wananchi wazifuate huduma,"amesema.
Kwa upande wake Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Kenya,Dan Kagwe amesema kuwa,miaka iliyopita tulikuwa hatuna mipaka bali tulikuwa majirani na tulikuwa tunaishi kwa amani na upendo mkubwa hivyo uwepo mipaka umesaidia sana kuongeza ushirikiano zaidi kwa wananchi wa nchi Kenya na Tanzania.
"Uwepo wa uzinduzi huu wa biashara ya kuvuka mpakani utasaidia sana kufanya biashara zetu ziwe za mashirikiano zaidi na kuweza kukuza uchumi wa nchi zetu."amesema Kagwe.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU), Sifundo Chief Moyo amesema kuwa, uwepo wa ushirikiano huo kati ya nchi zote mbili itasaidia kuokoa muda na gharama walizokuwa wanatumia wananchi katika kupata huduma hizo kwani kwa sasa hivi watachukulia napa hapa mpakani tofauti na hapo awali.