Nape: Wanahabari ongezeni mwamko wananchi kupiga kura

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mafunzo wa 108 wa watayarishaji wa vipindi vya elimu kwa umma kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) uliofanyika jijini Mwanza leo, Februari 20, 2024. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

  • Wanahabari watakiwa kutoa elimu ya upigaji kura ili kuongeza mwitikio wa wananchi kushiriki katika chaguzi zijazo.


Mwanza. Wanahabari nchini wameaswa kutoa elimu ya upigaji kura ili kuongeza mwitikio wa wananchi kushiriki katika chaguzi zijazo.


Kulingana na takwimu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC), mwitikio wa wapigaji kura mwaka 2015 ulikuwa asilimia 64.7 ambapo kati ya wapiga kura milioni 23.2 waliojiandikisha ni milioni 15 ndio walipiga kura.

Mwaka mwaka 2020 asilimia 50.7 pekee ya wapiga kura waliojiandikisha ndiyo walijitokeza, ambayo ni sawa na milioni 14.8 pekee kati ya milioni 29.2.


Akizungumza leo  Februari 20, 2024 jijini Mwanza wakati akifungua mkutano wa mafunzo wa 108 wa watayarishaji wa vipindi vya elimu kwa umma kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema wanahabari wana mchango mkubwa katika kuongeza mwamko wa wananchi kushiriki katika chaguzi hizo.


"Mwaka huu taifa letu linaingia katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na mwakani uchaguzi mkuu, rai yangu kwa wanahabari naomba jikiteni kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kupiga kura kwa wananchi kupitia maudhui yenu mnayokuwa mnaandaa kwenye vyombo vyenu.


“Ukiangalia takwimu za nyuma zinaonyesha wapigakura wachache wanashiriki katika chaguzi hizo hata hawafiki nusu ya Watanzania wote," amesema Nnauye.


Pia waziri huyo amewataka wanahabari kuandika habari zao huku wakienzi falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan ya R nne (4R) ambazo ni Maridhiano (Reconciliation), UStahimilivu (Resillience), Mageuzi (Reforms), na Kujenga (Rebuild) ili kuendelea kudumisha amani na ushirikiano katika jamii.


"Falsafa hii ili iwe na matokeo  mazuri na isibaki tu kuwa ya Rais lazima iingie katika maisha yetu kuanzia ngazi ya mtu na mtu wafanye maridhiano, wastahimiliane na wajenge upya mahusiano yao kungazia ngazi ya familia, kitongoji au mtaa mpaka ngazi ya juu tutaweza kushirikiana na kuenzi umoja wa taifa letu," amesema Nnauye.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dk Ayub Rioba akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo ambao ni maofisa habari kutoka vitengo mbalimbali serikalini, amewataka kushiriki kikamilifu katika kuenzi falsafa ya Rais Samia kutokana na majukumu yao kwa jamii.


 "Falsafa ya 4R za Rais Samia Suluhu Hassan inahitaji ifahamike zaidi kwa wananchi kwa sababu ndio falsafa pekee itakayotufanya tuendeleze ile misingi ya waasisi wa taifa letu ya amani, umoja na mshikamano," amesema Dk Rioba.


Naye Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amewasihi waandishi wa habari kuibua, kuandika au kuripoti habari zinazohusu maisha na changamoto za wananchi bila woga ili kuisaidia Serikali kuchukua hatua.


 “Sisi katika Serikali tuhakikishe tunatoa ushirikiano kwa vyombo vya habari kwa sababu vinatusaidia kufikisha mambo yetu kwa wananchi na kuchukua ya wananchi kutufikishia kwetu, ili kuweza kuchukua hatua zinazo stahili," amesema Matinyi.


Nao washiriki wa mafunzo hayo wamesema elimu hiyo watakayoipata itawasaidia kutoka na ujuzi wa kuandaa vipindi bora na vizuri vitakavyokuwa na msaada katika kuleta mabadiliko katika jamii.


"Huu ni mwaka wangu wa 10 mfululizo kuhudhuria katika mafunzo haya tangu 2014, sasa kwanini tunafanya hivi ni kwa sababu kuna mabadiliko ya teknolojia ya mara kwa mara na kuna kujisahau, kwa hiyo tunapokuwa tunapatiwa mafunzo haya tunakuwa tunanolewa, kuongezewa nguvu na kujiimarisha zaidi ili kuongeza hali ya kufanya zaidi," amesema Karim Solyambingu.


Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Prisca Ulomi amesema mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa kwao, ili kuwafanya kuwa daraja kati ya Serikali na wananchi.


"Mkutano huu kwetu ni muhimu na tukiangazia kwamba tayari mwaka huu kuna uchaguzi wa Serikali za mitaa na mwakani uchaguzi mkuu, yapo mambo ambayo tunapaswa kuiambia Serikali na jamii, ili tuweze kuwa kioo cha kuwaangazia yale ambayo wanatamani kuona Serikali inayafanya na tuweze kuwa sikio la kuchukua changamoto zao na kuzifikisha kwa mamlaka husika," amesema Ulomi.


Mafunzo hayo ya siku tano kwa maofisa habari wa Serikali yamefunguliwa leo Februari 20, 2024, huku yakiratibiwa na TBC.