Mataifa zaidi ya 50 kupiga kura mwaka 2024

Muktasari:

  • Mwaka 2024 zaidi ya mataifa 50 yanatarajia kupiga kura katika chaguzi kuu za kitaifa huku hatua hiyo ikitarajiwa kuamua mustakabali wa kisiasa kidunia kwa miongo kadhaa ijayo.

Dar es Salaam. 2024 ni mwaka wa uchaguzi duniani, ndivyo unavyoweza kusema, kwani zaidi ya mataifa 50 yakiwamo makubwa ya Marekani na Russia, ayatakuwa na uchaguzi mkuu.

Chaguzi hizo zitakazohusisha zaidi ya wapigakura bilioni nne zinatazamiwa kuamua mustakabali wa kasiasa duniani, kwa miaka au miongo kadhaa ijayo.

Bangladesh iliuanza 2024 kwa uchaguzi mkuu, na Sheikh Hasina ameshinda muhula wa nne mfululizo kama waziri mkuu Jumapili iliyopita ambapo vyama vya upinzani vilisusia matokeo kwa madai kuwa uchaguzu haukua huru na haki.

Kwa mujibu wa Sauti ya America (VOA), uchaguzi mwingine muhimu wa Rais unatazamiwa kufanyika katika kisiwa cha Taiwan Januari 13, 2024 huku tishio la China kutwaa tena kisiwa hicho kwa nguvu likitawala.

Mwezi Februari, Indonesia inatazamiwa kuchagua rais mpya wa kutawala Taifa hilo lenye watu milioni 277 na kuifanya kuwa moja ya chaguzi kubwa zaidi duniani zilizopigwa kwa siku moja.

Pakistan itafanya uchaguzi wa bunge mwezi huo, huku kiongozi wa upinzani na Waziri Mkuu wa zamani, Imran Khan bado akiwa jela kwa tuhuma za kuvujisha siri za serikali, jambo ambalo amelikanusha.

Russia watapiga kura katika uchaguzi wa rais Machi, ingawa wachambuzi wanatabiri kwamba Vladimir Putin ana nafasi kubwa ya kushinda kutokana na ushawishi mkubwa alionao.

India itafanya uchaguzi wa bunge mnamo Aprili na Mei, huku Chama cha Bharatiya Janata (BJP), chini ya Waziri Mkuu Narendra Modi, kikipewa kipaumbele kuibuka kidedea.

Juni 2, 2024 Mexico inatazamiwa kufanya uchaguzi wake wa urais, ambao unaweza kutangaza hatua mpya kwa nchi hiyo kwa sababu ya uwezekano kwamba huenda kwa mara ya kwanza mwanamke akaiongoza Mexico.

Chama tawala nchini humo kimemchagua Claudia Sheinbaum, meya wa zamani wa jiji la Mexico kuwa mgombea wake.

Umoja wa Ulaya unaoundwa na takriban mataifa 27, unaowakilisha zaidi ya watu milioni 500, unatazamiwa kufanya uchaguzi wa wabunge mwezi Juni, 2024.

Uingereza inatarajia kufanya uchaguzi kabla ya mwisho wa mwaka huu, huku kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour Keir Starmer akiwa mbioni kumaliza miaka 14 ya misukosuko ya utawala wa chama cha Conservative, kikiwa na mawaziri wakuu watano tofauti.

Novemba 5, 2024 Marekani inatazamiwa kufanya uchaguzi wa urais unaotarajiwa kuwa na mchuano mkali kati Rais aliyeko madarakani, Joe Biden na Donald Trump wa chama cha Republican.

Mataifa mengine yanayotarajia kufanya uchaguzi mwaka huu ni pamoja na Algeria, Botswana, Chad, Comoros, Ghana, Mauritania, Zambia, Namibia, Rwanda, Senegal, Tunisia na Togo.

Mengine ni Canada, Uruguay, Venezuela, Cambodia, Iran, Mongolia, Uturuki, Ubelgiji, Finland, Iceland, Ireland, Ureno, Romania, Slavakia, Hispania na Australia.