NCA yazindua mkakati mpya ikijivunia uliopita

Dar es Salaam. Shirika la Norwegian Church Aid (NCA) Tanzania limezindua rasmi Mkakati wake mpya wa Kitaifa wa miaka mitano (2025–2029) ambao unatarajiwa kuboresha ustawi wa kijamii na kiuchumi nchini.
Uzinduzi huo uliobeba kaulimbiu “Pamoja kwa Jamii yenye haki Tanzania” ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka Ubalozi wa Norway, maofisa wa serikali, viongozi wa dini, mashirika ya kiraia, na wadau wa maendeleo.
Tukio hilo limeashiria upya dhamira ya kuokoa maisha, kujenga uwezo wa jamii kustahimili changamoto, na kutafuta haki kote nchini.
“Mkakati huu mpya utajikita katika kupambana na ukosefu wa usawa, kutokomeza ukatili wa kijinsia, kuendeleza uchumi na usalama wa chakula, kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi” alisema Mkurugenzi wa NCA Tanzania, Berte Marie Ulveseter.
Ulveseter alisema mkakati huo umejengwa juu ya dhamira ya NCA ya ushirikiano wa haki na maendeleo yanayoongozwa na jamii husika, kuhakikisha kuwa jamii haziwi wapokeaji tu wa misaada, bali washiriki wa kweli katika kuleta mabadiliko.
Katika wakati huu ambapo baadhi ya wafadhili wanajiondoa, ikiwemo USAID, NCA imetoa shukrani za dhati kwa msaada endelevu kutoka Norad na wananchi wa Norway ambao wameendelea kujitoa kwa kazi za maendeleo na kibinadamu nchini Tanzania.
“Huu si mkakati tu, bali ni mwito wa kuchukua hatua,” alisisitiza Mkurugenzi huyo. “Lazima tuendelee kuwa na mvuto, tuwe na umuhimu, na tuwe na matokeo chanya. Na zaidi ya yote, lazima tuitembee safari hii pamoja na jamii, si kwa niaba yao ili kuhakikisha matokeo ya haki na endelevu.”
Akielezea mafanikio ya mkakati uliopita wa miaka mitano, Ulveseter alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2020–2024), NCA na washirika wake wameleta mafanikio yanayopimika kupitia miradi jumuishi inayoongozwa na jamii na kushirikisha imani mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa zaidi ya Vikundi 5,000 vya Akiba na Mikopo vya Jumuiya za Kidini (Inter-Religious Community Microfinance Groups), ambavyo vimeongeza ustahimilivu wa kiuchumi katika ngazi za chini.
Katika kipindi hicho, jumla ya wanawake, wanaume na vijana 24,976 walipata taarifa za ugani kwa njia ya kidijitali na fursa za masoko kupitia jukwaa la JAMBOMAISHA.
Aidha, Ulveseter alibainisha kuwa shirika hilo limewezesha wanawake, wanaume na vijana 27,023 kutumia mbinu, teknolojia na huduma bunifu na rafiki kwa mazingira katika kilimo.
Zaidi ya hayo, vijana 5,291 wamenufaika kupitia vituo vya ubunifu wa kilimo vilivyoanzishwa kusaidia wakulima wadogo, na vikundi vya uzalishaji 934 vimeanzishwa na kusajiliwa rasmi na sasa vinapata masoko ya uhakika.
Pia, watu 15,342 wanawake, wanaume na vijana — walipata huduma za msaada wa kisheria, na wanawake na mabinti 83,747 walifikiwa na elimu ya afya ya uzazi na mipango ya familia.
Zaidi ya Kamati 100 za Ufuatiliaji wa Matumizi ya Fedha za Umma (PETs) zimeanzishwa ili kuhakikisha uwajibikaji, na kamati 40 za dini mbalimbali katika ngazi za wilaya na mikoa zimetunzwa ili kuimarisha mshikamano wa kijamii.
“Mafanikio haya yote yalikuwezekana kutokana na ushirikiano tulioujenga na jamii, mashirika ya kiraia, na hasa washirika wetu wa kidini,” alisema Ulveseter.
“Viongozi wa dini wa Kikristo na Kiislamu wamekuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza amani, sera za afya, haki ya kodi, usawa, na mabadiliko ya jamii,”