Norway, Tanzania kushirikiana kulinda misitu

Balozi wa Norway nchini Tanzania,Toni Tinnes,akizungumza katika kijiji cha Msufini Kata ya Mkula wilayani Kilombero, mkoani Morogoro alipotembelea miradi mbalimbali waliyoifadhili kupitia Mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki (EAMCEF). Picha na Janeth Mushi
Muktasari:
- Balozi wa Norway nchini Tanzania, Toni Tinnes, amesema mradi huo ni uthibitisho wa ushirikiano kati ya nchi hizo uliosaidia kulinda uhifadhi.
Morogoro. Serikali ya Norway imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali, ikiwemo ya uhifadhi ili kusaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi na kulinda uhifadhi nchini Tanzania.
Balozi wa Norway nchini, Toni Tinnes amesema hayo leo Machi 15, 2024 katika Kijiji cha Msufini, Kata ya Mkula wilayani Kilombero mkoani Morogoro, alipotembelea miradi waliyoifadhili kupitia Mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki (EAMCEF) na kuzindua jengo la kuchakata, kuhifadhia na kuuza asali.
Mradi huo wa ujenzi wa jengo umelenga kuendeleza ufugaji nyuki kwa uhifadhi wa viumbe hai na kuboresha maisha ya jamii iliyo jirani na milima ya Udzungwa, umegharimu Sh86 milioni.
Amesema miradi hiyo ni uthibitisho kuwa ushirikiano wa Serikali hizo mbili umesaidia kulinda uhifadhi na kupongeza hatua ya kutolewa elimu na ushirikishwaji wa miradi hiyo ya uhifadhi kwa makundi mbalimbali ikiwemo wanafunzi.
"Huu mradi ni uthibitisho wa ushirikiano kati ya Tanzania na Norway na tumeshuhudia matunda ya msaada huu tuliotoa hasa ikizingatiwa uhifadhi mazingira ni muhimu kwa ajili yetu na vizazi vijavyo na matukio ya uharibifu msituni yamepungua.
“Tumefurahi kuona mabadiliko kupitia miradi mingine tuliyofadhili ukiwemo wa ufugaji samaki na majiko banifu ambao ni muhimu kwa lengo la kusukuma ajenda ya nishati safi na tutaendeleza ushirikiano," amesema Balozi huyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa mfuko huo, Francis Sabuni amesema katika kipindi cha miaka 12 iliyopita mfuko umekuwa ukifadhili miradi kupitia ufadhili wa Norway ambao kuanzia mwaka 2011 hadi 2023 (Norway) wamesaidia fedha za ufadhili dola milioni 13 za Marekani (Sh321.56 bilioni) na kuwa kwa sasa maisha ya jamii katika maeneo mbalimbali yanayozunguka milima hiyo yameboreshwa na umasikini umepungua, uharibifu na athari zimepungua.
Amesema katika kipindi hicho wametoa Sh8 bilioni kwa ajili ya miradi ya kuhifadhi maeneo hayo na kati ya hizo Sh4 bilioni ambazo ni asilimia 50 ya fedha zote zilikwenda kwenye miradi ya jamii ya kuondoa umasikini na kuinua kipato cha wananchi.
Ameeleza kuwa sasa hivi ni mara chache kuona matukio ya moto kwenye maeneo hayo wanayofadhili, huku matukio ya kuanzisha mashamba, makazi na kuchunga mifugo kumeendelea kupungua na kuwa miaka ya nyuma kulikuwa na tatizo la uchimbaji madini hasa maeneo ya Chome (Same) na Amani.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya ameushukuru mfuko wa EAMCEF kwa kutekeleza miradi hiyo wilayani humo na kuwa imesaidia kulinda uhifadhi baada ya wananchi kufahamu namna bora za kufanya uhifadhi na kutekeleza miradi ya kiuchumi kwa jamii.
"Wilaya yetu inatoa maji mengi kwa ajili ya bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP), kwa takwimu tuna mito 38 ndani ya mto Kilombero na tunachangia asilimia 65 ya maji, hivyo tukitunza mazingira kwa kushirikiana na mfuko na wadau wengine tutahakikisha bwawa lile linaendelea kuwa salama," ameeleza
Katibu wa Kikundi cha Wosia wa Baba, Rexoni Mtama, amesema kikundi hicho chenye wanachama 20 kilianza mwaka 2006 kikiwa kimelenga kutunza mazingira na kuinua uchumi wao wakiwa na mtaji wa Sh50,000 uliowawezesha kununua mizinga mitano ya kienyeji.
Amesema baada ya ufadhili wa mfuko huo wameweza kuongeza idadi ya mizinga na kufikia mizinga 91, kupata elimu ya ufugaji nyuki, kupewa mavazi maalum kwa ajili ya kirina asali, vifungashio, mizinga ya kisasa, mizani ya kupima asali na kujengewa jengo hilo la kuchakata na kuuza asali.
"Tangu tumeanza hadi sasa uzalishaji umeongezeka na kufikia lita 450 kwa kipindi cha mwaka 2023 na toka mwaka 2012 hadi sasa tumevuna asali lita 267,000 na kupata fedha zaidi ya Sh 26.7milioni.
“Tumewezesha kuanzishwa vikundi vingine 14, mizinga 40 ya wanakikundi nje ya mradi wa kikundi na jengo hili la ukusanyaji, uchakataji na uuzaji wa asali limegharimu Sh86 milioni na kati ya hizo sisi kikundi tumechangia Sh 6milioni na Mfuko umetuchangia Sh 80milioni," amesema