Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Balozi Norway ataja fursa, changamoto kilimo nchini

New Content Item (1)

Dar es Salaam. Balozi wa Norway nchini, Toni Tinnes amesema Tanzania inapaswa kuwa na mipango ya kutumia kikamilifu fursa iliyonayo katika kilimo ili kuwa na uhakika wa chakula.

Balozi Tinnes ametoa ushauri huo wakati Tanzania ipo katika mpango wa kuwa mzalishaji mkubwa barani Afrika na kuongeza uzalishaji wa chakula kibiashara kwa ajili ya soko huru la Afrika (AfCTA).

Miaka mitatu iliyopita, Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na wafanyabiashara nchini Marekani, aliwakaribisha kuwekeza nchini katika sekta ya kilimo, akisema kuna fursa ya kulisha sehemu kubwa ya bara la Afrika.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa kituo cha mafunzo mkoani Iringa ili kuongeza tija kwa wakulima, Balozi Tinnes alisema uzalishaji wa tija bado changamoto kwa wakulima wa Tanzania, lakini ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi unaofanywa sasa utabadili hali ya mambo. “Nimefurahi kuona Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye kilimo na ni matumaini yangu kwamba ushirikiano tunaouona kati ya sekta ya umma na binafsi unaendelezwa kwa manufaa ya wananchi," alisema Tinnes, huku akisisitiza uwezeshaji wanawake katika sekta hiyo.

Kituo hicho kilichoanzishwa na Kampuni ya Yara Tanzania kwa kushirikiana na Farm Taasisi ya For the Future (FFF) na Seed Co. Limited kilizinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego kikiwa ni kituo cha saba, vingine vikiwa katika mikoa ya Mbeya, Morogoro, Kilimanjaro, Tabora, Manyara na Zanzibar.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego alisema uanzishwaji wa kituo hicho utasaidia kukabiliana na changamoto zinazowakwamisha wakulima kufikia kiwango cha juu cha uzalishaji.

Dendego alisema changamoto kubwa ni ukosefu wa elimu ya kilimo na pembejeo za kilimo kama mbolea, miundombinu mibovu, teknolojia nafuu, wadudu na magonjwa, uhaba wa vyanzo vya maji, kukatika kwa soko, ukosefu wa mitaji na mazingira magumu ya hali ya hewa.

Wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Yara Tanzania, Winstone Odhiambo, alisema kituo hicho ni chachu ya kuongeza upatikanaji wa elimu ya kilimo na msaada wa ugani hasa kwa wakulima wadogowadogo ambao wana changamoto ya kukosa maarifa ya utatuzi wa lishe ya mazao na njia nyingine za uzalishaji. Osmund Ueland, mwanzilishi wa FFF alisema kituo hicho kitaongeza kasi ya ndoto ya mradi wao kwa kuwa kituo cha mfano kwa maendeleo ya jamii nchini Tanzania.

"Dhamira yetu ni kufanya kazi na washirika wenye nia moja, ili kuboresha mpango wa kuwatoa katika umasikini wakulima wadogo 2,000 kutoka vijiji 16 vinavyozunguka mradi ifikapo  mwaka 2030," alisema Ueland.

Mkurugenzi Mtendaji wa Seed Co. Limited Clive Muganda alisema, kampuni hiyo itaendelea kusaidia mipango inayoendesha matumizi ya utafiti na ujuzi wa pamoja juu ya afya ya udongo, uendelevu wa mazingira na kuimarisha minyororo ya thamani ya kilimo kwa ajili ya uzalishaji wa mali shirikishi."