NCCR-Mageuzi wazichapa kavukavu

Muktasari:

Bundi ametua ndani ya chama cha NCCR- Mageuzi.

Dar es Salaam. Bundi ametua ndani ya chama cha NCCR- Mageuzi.

Ndivyo unavyoweza kueleza, baada ya Halmashauri Kuu ya chama hicho kumsimamisha Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia na Makamu Mwenyekiti Bara, Angelina Mtahiwa, huku makao makuu ya chama hicho yakigeuka kuwa uwanja wa mapambano kwa muda kati ya wafuasi wa pande mbili zenye mgogoro.

Uamuzi wa kumsimamisha Mbatia ulitolewa jana jijini hapa, baada ya kikao hicho kilichohudhuriwa na wajumbe 52 kati ya wajumbe 82 waliopaswa kuwapo.

Hata hivyo, baada ya kikao hicho, Katibu Mwenezi wa chama hicho, Edward Simbeye aliyezungumza na waandishi habari katika ofisi za makao makuu Bungoni Ilala, alisema kilichofanyika ni uhuni na uhaini ndani ya chama.

Simbeye alisema awali walishapeleka taarifa ya uamuzi ya kikao cha Kamati Kuu katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu kusimamishwa kwa katibu mkuu huyo.

Hata hivyo, Naibu Msajili wa vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza alisema kuwa ofisi ya Msajili kama mlezi wa vyama vyenye usajili wa kudumu, ina jukumu la kuhakikisha vyama vinajiendesha kwa mujibu wa Katiba ya nchi na ile ya chama husika.

“NCCR walituletea barua kuwa wana mabadiliko ya bodi ya wadhamini, pamoja na mabadiliko ya bodi hiyo, kukawa na ajenda nyingine ambayo ni kusimamishwa kwa mwenyekiti na makamu wake,”alisema Nyahoza.

Aliongeza: “Kikao kimefanyika na wajumbe wapo tunasubiri barua rasmi ili kutoka uamuzi. Sisi tutaenda kuangalia na wajumbe wamesomwa na akidi imetimia hivyo tunangoja ratiba rasmi na kwenda kupitia katiba yao.’’

Kwa upande wake, Mbatia hakuwa tayari kuzungumza lolote, huku akimweleza mwandishi kuwa atatoa taarifa kesho (leo).

Hatua ya kumsimamisha Mbatia na makamu wake imekuja ikiwa ni wiki mbili tangu Katibu Mkuu wa chama hicho, Martha Chiomba kuzungumza na waandishi wa habari na kudai kuwapo kwa njama za kumwengua katika nafasi yake, kauli iliyopingwa vikali na jumuiya ya vijana na ile ya wanawake za chama hicho.


Hali ilivyokuwa jana


Baada ya kumalizika kwa mkutano wa Halmashauri Kuu, Katibu Mkuu Martha Chiambo akiwa ameongozana na walinzi walifika makao makuu ya chama hicho na kuamuru ofisi hizo kufungwa.

Baada ya katibu huyo kuondoka na kuacha vijana wakilinda eneo hilo, Katibu mwenezi wa chama hicho, Edward Simbeye aliwasili na kufungua ofisi hizo kisha kuzungumza na waandishi wa habari.

Alipomaliza, Mbatia aliwasili akiwa na ameambatana na Makamu Mwenyekiti Zanzibar na kuingia moja kwa moja ndani ya ofisi hizo bila kuongea na mtu.

Kundi lililokuwa limeachwa kulinda ofisi hizo lilianza kusogea wakati Mbatia akiingia ndani, ndipo ugomvi ulipoibuka baina ya makundi hayo mawili, kabla ya polisi kuingialia kati na kuwatuliza.


Uamuzi

Akizungumza na wanahabari jana katika ukumbi wa Jeshi la Wokovu uliopo Kurasini jijini hapa, mjumbe wa Halmashauri Kuu na Mwenyekiti wa maazimio hayo, Joseph Selasini alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya kubaini kumekuwepo na mwenendo wa kuwagombanisha viongozi na kuwalazimisha kujiuzulu.

“Halmashauri Kuu imeazimia kumsimamisha Mwenyekiti Mbatia na Makamu Mwenyekiti Bara hadi pale mkutano mkuu utakapoitishwa mapema mwaka huu na kuja kujieleza,” alisema.

Selasini, aliyehamia chama hicho mwishoni mwa mwaka 2020 akitokea Chadema, alisema maazimio mengine ni pamoja kulivunja baraza la wadhamini la NCCR -Mageuzi na kuteua wajumbe wengine, ambao watasajiliwa kwa taratibu zitakazowekwa.

“Halmashauri Kuu inamuagiza katibu mkuu kuvunja sekretarieti ya chama, kutokana na kuchochea mtafaruku na kuhakikisha wanaunda sekretarieti nyingine mapema iwezekanavyo,” alisema.

Kuhusu tuhuma nyingine zinazomkabili Mbatia, Selasini ambaye pia ni miongoni mwa waanzilishi wa chama hicho mwaka 1990 kabla ya kujitoa mwaka 2009, alisema Mwenyekiti huyo aliitisha kikao cha Kamati Kuu na kubadilisha uamuzi wa chama kushiriki katika kongamano la vyama vya siasa na Msajili lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzani (TCD).

“Tulibaini kikao cha Kamati Kuu iliyoamua kufuta uteuzi wa wajumbe, lakini chama kimeweka marufuku ya kufanyika kura kwa njia ya mtandao, kikao kile hakikuwa na Katibu Mkuu, kama katibu hayupo basi Naibu Katibu Mkuu au mjumbe wa sekretarieti,” alisema.

“Kikao hicho katibu alikuwa Edward Simbeye ambaye alikuwa hana mamlaka kutokana na kutokaimishwa na kwa mujibu wa sheria na taratibu za chama,” alisema.

Aidha, Selasini alisema vurugu ziliendelea ndani ya chama hadi Mei 15 ambapo walimsimamisha Katibu Mkuu na kuzuia mkutano wa Halmashauri Kuu.

“Tangu mwaka 2010 chama hakijawahi kushiriki shughuli za chama wala ziara mkoani zaidi ya vikao na waandishi wa habari. Tunasimama na itikadi ya utu, tunaunga mkono kauli ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ya kufanya siasa za kistaarabu na za kujenga hoja.

“Tunajitenga na kauli zilizowahi kutolewa na Mbatia dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan, na tunampongeza kwa jitihada za kuleta vyama pamoja na maridhiano. Halmashauri Kuu tunataka maridhiano na vyama vifanye kazi kwa kuheshimiana,” alisema.

Selasini alisema wawili hao hawataruhusiwa kujihusisha na shughuli zozote za chama hadi pale mkutano mkuu utakapoitishwa na wao kufika mbele ya wajumbe na kujieleza.


Bundi alivyotua NCCR-Mageuzi

Kwa miezi miwili sasa, mwangwi wa mgogoro ndani ya NCCR-Mageuzi ulianza kusikika hasa baada ya wajumbe wa Halmashauri kuu kwenda kinyume na msimamo wa chama, jambo lililoashiria hali si shwari.

Mathalani, licha ya chama hicho kutangaza msimamo wa kususia mkutano wa wadau wa siasa ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa Desemba mwaka jana, baadhi ya viongozi wake walihudhuria mkutano huo.

Lakini takribani wiki moja iliyopita, Katibu mkuu wa chama hicho alijitokeza kwa wanahabari akieleza kuwa hayuko tayari kujiuzulu wadhifa huo ‘kihuni’ kwa shinikizo la baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho.

Katika mkutano huo alidai wapo viongozi wakuu wanashiriki moja kwa moja kuharibu amani, utulivu na mshikamano ndani ya chama.

Hata hivyo, hivi karibuni Mbatia alinukuliwa akisema hakuna mgogoro wowote wa kiuongozi ndani ya chama hicho na kwamba mambo yote yatajadiliwa na kutatuliwa kwa vikao kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho.

Na jana alipoulizwa na Mwananchi kuhusu kilichotokea, alisema atazungumza kesho (leo) na wanahabari.


Mgogoro 2015

Septemba 22, 2015, chama hicho kilimsimamisha uongozi Makamu mwenyekiti wa chama hicho, Leticia Mosore kwa madai ya kukihujumu chama hicho, lakini Msajili wa vyama, Jaji Mutungi alimrejesha.

Migogoro ya uongozi ndani ya NCCR-Mageuzi ilianza mwaka 1997 baada ya aliyekuwa mwenyekiti wake, Augustino Mrema kutakiwa kuachia nafasi hiyo katika mkutano uliotawaliwa na vurugu.

Katika mkutano huo uliofanyika hoteli ya Raskazone jijini Tanga, Mei 1997, taa zilizimwa ghafla ambapo walinzi wa Mrema walifanya kazi kubwa ya kumlinda kiongozi huyo baada ya viti kuanza kurushwa.

Nyongeza na Daniel Mjema.