Ndani ya Habari: Siri wanafunzi wa vyuo kudondoka masomoni
Dar es Salaam. Wakati idadi ya wanafunzi wanaofeli na kushindwa kuendelea na masomo vyuo vikuu ikiongezeka, ugumu wa maisha unatajwa kuchangia hali hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti iitwayo Vitalstats iliyotolewa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), wanafunzi katika vyuo hivyo walifeli kwa asilimia 95 katika mwaka wa masomo wa 2021/2022.
Ripoti hiyo ya mwaka 2022 iliyotolewa hivi karibuni, ilionyesha wanafunzi wanaoacha masomo baada ya kufeli imefikia 2,893 katika mwaka 2021/2022 kutoka wanafunzi 1,484 mwaka 2018/2019
Aidha ripoti hiyo inawataja wanawake kuwa vinara kwa kuacha chuo ikilinganishwa na wanaume katika mwaka huo.
Mwaka 2021/2022 wanawake 1,732 walifeli na kushindwa kuendelea na masomo yao ikilinganishwa na wanaume 1,161.
Sababu ya kuacha masomo
Ukosefu wa fedha za kujikimu, ni moja ya sababu kwa wanafunzi wengi kuingia katika shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato ambazo zimekuwa zikiwachukulia muda mwingi badala ya kusoma.
Pia umri mdogo unatajwa kuchangia baadhi yao kushindwa masomo kwa wengi kushindwa kutumia uhuru wanaoupata wakiwa vyuoni.
Sababu nyingine zilizotajwa ni kufutiwa usajili, huku takwimu zikionyesha mwaka 2021/2022 waliofutiwa walikuwa 653, waliofukuzwa kwa utoro, wanafunzi 67 na waliofariki wakiwa 27.
Akizungumzia suala hilo, mtafiti wa elimu, Muhanyi Nkoronko alisema wakati mwingine kufeli kwa wanafunzi kunatokana na kutotilia mkazo masomo, huku akisema wengi wanaoangukia katika kundi hilo ni wa mwaka wa pili na wa tatu.
Hiyo ni kutokana na kile alichokieleza kuwa wanafunzi hao wamekuwa na shughuli nyingi ikiwemo kujihusisha na biashara na kazi ili waweze kujiingizia kipato jambo ambalo limekuwa likiwafanya wakose muda wa kujisomea.
“Kuna watu wanajisomesha, hawana hela za kujikimu, inabidi wafanye hivyo matokeo yake wengine wanajikuta wameweka nguvu sehemu moja na kupoteza sehemu nyingine,” alisema Nkoronko.
Sababu nyingine ya wanafunzi kufanya vibaya ni kusoma fani ambazo hawawezi kuzimudu jambo ambalo linawafanya kuishia kufanya vibaya.
“Mtu anasomea udaktari lakini hawezi kumudu masomo yake vyema, mwishowe anaishia kufanya vibaya, vyema wachague fani wanazoweza kuzimudu ili kuepuka hili,’’ alisema Nkoronko.
Faraja Kristomas kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema kushindwa kumudu masomo ya chuo kikuu, ni sababu kubwa ya watu kufeli.
Hilo linaanzia katika mfumo wa upatikanaji wa wanafunzi hao unaotumika sasa kwa kutumia ufaulu wa kidato cha sita tofauti na ule wa wanafunzi kufanya mitihani ya udahili wa vyuo vikuu uliokuwa ukifanyika awali.
"Hii imefanya uwezo wao wa kuhimili masomo kuwa ni mgumu kwani chuo kikuu ni tofauti na sekondari ambapo mwanafunzi atasimamiwa na walimu, lakini huku inabidi ajisimamie kuanzia katika usomaji na kujiendeleza katika alichofundishwa,’’ alisema.
Pia aina ya maisha ya chuo imetajwa kuwa moja ya sababu hasa katika wakati huu wa sayansi na teknolojia, huku umri wa wanafunzi nao ukitajwa kuwa wengi kushindwa kujisimamia.
"Ili kutatua hili ni vyema waandaliwe huko sekondari ili wawe na uwezo wa kutosha na kumudu masomo wakiwa chuoni, hii ndiyo njia inayoweza kupunguza hili,’’ alisema.
Naye Dk Luka Mkonongwa kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), alisema uandaaji wa wanafunzi kwa ajili ya kujiunga kidato cha sita, umekuwa changamoto kwani mara zote wanapoingia vyuo huona kama wamekutana na vitu vipya.
“Wengi unakuta wameingia vyuo wakiwa wamefaulu vizuri, lakini ukiangalia nyuma tangu anamaliza kidato cha nne na sita alikuwa akitegemea twisheni ambazo zote walimu walimpa notisi akasome hivyo amezoea spoon feeding (kufanyiwa kila kitu), akija chuo mwalimu anategemea wewe ndiyo ukasome,” alisema Dk Mkonongwa.
Alisema hilo linaonekana sana katika maswali ambayo yanahitaji mtu kutumia ufahamu katika kuyajibu kwani wanafunzi wengi wamekuwa wakishindwa.
“Pia aina ya maisha ya chuo ya uhuru, wengi hawakuwa wameyazoea, hakuna mtu wa kuwasimamia, umri wao mdogo mwisho wa siku wanasahau kusoma,” aliongeza kusema.
Aliguswa pia na hali ngumu yaa maisha kwa baadhi ya wanafunzi wakiwa vyuoni.
Anasema: “Nafikiri pia kuna haja ya kuangalia namna mikopo inavyotolewa, baadhi ya walio na hali ngumu wanakotoka wamekuwa wakipata kitu kidogo ambacho hakikidhi mahitaji yao, hivyo kuwafanya waingie katika shughuli ndogondogo za kujiingizia kipato ambazo zinawafanywa mwishowe wafeli.’’
Aidha, ukosefu wa vifaa wezeshi vya kutosha katika maktaba za baadhi ya vyuo hususani vitaabu na intaneti ya uhakika, nalo limetajwa kuwa sababu ya wanafunzi kushindwa kufikia baadhi maarifa muhimu ya mtandaoni na vitabuni.
Nini kifanyike?
Kwa upande wa Nkoronko, ni vyema Serikali ikaongeza ufadhili wa masomo kwa wanafunzi, kwa sababu wengi wanashindwa kufanya vizuri kutokana na kukosa mahitaji ya msingi ili waweze kumudu masomo yao.
Pia alipendekeza kuwa muundo wa vyuo vikuu, ubadilishwe na kuwa rafiki hasa kwa wale wanaofeli katikati pindi wanapotaka kusoma tena wasilazimike kuanza mwanzo bali waendelee pale walipokwama.
“Ni wakati sasa mifumo iwekwe sawa, kama mtu alikwama mwaka wa pili na mwaka wa kwanza alifanya vizuri, ni vyema aendelee alipoishia badala ya kuanza upya hii itawasaidia wengi,” alisema Nkoronko.
Dk Mkonongwa naye anapendekeza kuongezwa kwa uwekezaji upande wa elimu wa juu hasa katika mikopo kwa wanafunzi na kuongeza idadi ya wahadhiri vyuoni ili kuwapunguzia mzigo mkubwa wa kufundisha wanaokuwa nao.
“Tukipunguza mzigo wa kufundisha kwa wahadhiri tunaweza kupunguza idadi ndogo ya wanaofeli kwa makosa ya kibinadamu. Wengine kunakuwa na makosa katika usahihishaji kwa sababu mtu alichoka, umakini ukapungua na kwa sababu wanafunzi ni wengi darasani hawezi kurudia mara mbili,” alisema Dk Mkonongwa.
Mdondoko wa wanafunzi hauishii kwa wanafunzi walio vyuoni pekee.
Hata kwa waliomaliza fani ya sheria wakalazimika kusomea uwakili katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST), wengi wamekuwa wakiangukia pua.
Kufeli kwa idadi kubwa ya wanafunzi katika taasisi hiyo, kuliisukuma Serikali kuunda kamati maalumu kufuatialia hali hiyo.