Wasomi wakumbushwa kusoma vitabu zaidi

Mwalimu Maneno Mng'ong'o mtunzi wa kitabu Cha Ukombozi kutoka kitabuni akiwahamisha wanafunzi katika Chuo cha Mipango Dodoma kuwa na utamaduni wa kusoma vitabu.

Muktasari:

  • Wito umetolewa kwa vijana na Watanzania kwa ujumla wajenge tabia ya kujisomea ili kuongeza maarifa na ujuzi.

Dodoma. Wito umetolewa kwa vijana na Watanzania kujenga tabia ya kujisomea ili kuongeza maarifa na ujuzi.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumapili Juni 4, 2023 na mtunzi wa kitabu cha ukombozi, Mwalimu Maneno Mng'ong'o wakati akizungumza na vijana na wasomi wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini Cha Jijini Dodoma.

Kitabu hicho kimetungwa kwa ufadhili wa Sanlam Life Insurance, Mng'ong'o amesema kundi kubwa la watu kwa sasa hawana utamaduni wa kusoma vitabu badala yake wamezamia katika mitandao ya kijamii na mambo yasiyofaa.

Mwandishi huyo ametaja changamoto hiyo kwamba inalitafuna Taifa la kesho ambalo kwa mtazamo wake linajengwa na vijana wa leo.

Kwa mujibu wa Mng'ong'o, kwa siku za hivi karibuni majengo ya Makazi yanajengwa lakini wamiliki hawakumbuki hata kuweka sehemu za kujisomea.

"Hata kwa mafundi selemala hukuti wakichonga vifaa au kabati za vitabu, hivi tunakwenda wapi ndugu katika Dunia hii ambayo inataka maarifa zaidi," amehoji.

Kuhusu kitabu cha ukombozi amesema kinabeba maudhui ya hamasa ya watu kupenda kujisomea zaidi kwa makundi yote.

Mchungaji Canon Elikana Gonda wa Kanisa la Anglikana Chuo cha Mipango Dodoma amesema misingi ya Taifa imara inajengwa na vijana wasomi ambao watapenda kujishughulisha katika kutafuta maarifa ikiwemo vitabuni.