Ndingo ataka mazungumzo mgogoro bonde la Ihefu

Mgombea ubunge wa Mbarali wa tiketi ya CCM, Bahati Ndingo akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ifushilo wilayani humo katika mwendelezo wa mikutano ya hadhara ya kujinadi kuwania jimbo hilo.

Muktasari:

  • Mgombea ubunge wa jimbo la Mbarali, mkoani Mbeya kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), awataka wananchi wa jimbo hilo kuwa watulivu, huku wakitoa ushirikiano kwa Serikali katika utatuzi wa mgogoro wa ardhi wilayani humo.

Mbarali. Mgombea ubunge wa jimbo la Mbarali, kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bahati Ndingo, amewataka wakazi wa jimbo hilo, kuwa watulivu na kushirikiana na Serikali kwenye utatuzi wa mgogoro wa ardhi wilayani humo, badala ya kutunishiana misuli.

Amesema mwaka 2008 Serikali ilitoa tangazo la kuwazuia wakazi wa wilaya hiyo wasifanye maendeleo ya kudumu kwa baadhi ya maeneo ya bonde la Ihefu hadi watakapotangaziwa vinginevyo.

Uamuzi huo wa Serikali ulitokana na ripoti za watalaamu kuwa endapo wananchi wataendelea kubakia na kufanya shughuli zao watazuia mtiririko wa maji toka Mto Ruaha na Bonde la Ihefu.

Leo Alhamisi Septemba 14, 2023 na akiwa kwenye kampeni katika vijiji vya Ifushilo, Ukwavila na Woninyika, Ndingo amesema Serikali ya CCM ni sikivu na yenye kujali wananchi wake ndiyo maana tangu wakati huo mpaka sasa haijatumia mabavu.

"Ndugu zangu hakuna kitu kizuri kama maelewano hata pale inapotokea tofauti ni vema pande mbili zikakutana na kutafuta suluhu badala ya kutunishiana misuli," amesema.

Amesema amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kupitia kwa Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda na Spika wa Bunge, Dk Tulia Akson, aridhie wakulima wa Mbarali kufanya shughuli zao kwenye maeneo yaliyozuiliwa.

Ndingo amesema aliwasilisha ombi hilo kwa kuwa anaamini Rais Samia ni msikivu na anayependa maendeleo hivyo anaamini jambo hilo atalifanyia kazi.

Ndingo amesema wakulima wakiachwa wafanye shughuli za kujipatia kipato huku Serikali ikiendelea na taratibu nyingine zikiendelea kufanyiwa kazi.

"Najua vipato vyetu hasa wakulima vimeathirika kwa kuwa tangazo la Serikali limezuia, naamini hili jambo tukilipeleka kwa busara na kwa kushirikiana na Serikali litapatiwa ufumbuzi unaostahili, nawaombeni mnipe kura nikashirikiane na wenzangu kutetea masilahi yenu" amesema

Ndingo ambaye alikuwa mbunge wa viti maalumu lakini alijiuzulu mwezi uliopita baada ya Kamati Kuu ya CCM kupitisha jina lake, anawania kiti hicho ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa Mbarali, Francis Mtega aliyefariki Julai Mosi mwaka huu kwa baada ya kugongwa na trekta dogo (Power Tiller), shambani kwake.

Ndingo amesema yeye ndiye mtu sahihi wa kwenda bungeni kuyasemea matatizo ya wananchi wa vijiji vya Ifushilo, Ukwavila na Mbarali.

"Mimi ni mwenzenu na ninajua matatizo yetu hivyo naombeni mnipe kura zenu niende bungeni nikawawakilishe ili tupige kasi katika maendeleo na tufurahie rasilimali zetu," amesema na kuongeza;

"Nitahakikisha ninajenga hoja kuhusu suala hili ili Serikali inisikilize, uzuri Rais Samia ni mama mpole mnyenyekevu atanisikiliza. Kikubwa ni kujenga hoja ya msingi aje kuona haya mambo na kutoa uamuzi, msinione hivi kazi hii (ubunge) ninaiweza, nitasimama kwa maslahi ya Mbarali," amesema Ndingo.