Ndugai ajitosa sakata la bodaboda, Lema amjibu

Muktasari:

  • Spika mstaafu wa Bunge, Job Ndugai amejibu kauli ya kazi ya bodaboda laani ambayo imewahi kutolewa na mbunge wa zamani wa Arusha Mjini kupitia Chadema, Godbless Lema.

Dar es Salaam. Spika mstaafu wa Bunge, Job Ndugai amejibu kauli ya kazi ya bodaboda laana ambayo imewahi kutolewa na mbunge wa zamani wa Arusha Mjini kupitia Chadema, Godbless Lema.

Lema aliwahi kutoa kauli iliyozua gumzo kwenye mitandao ya kijamii kwamba ajira ya bodaboda siyo kazi bali ni chanzo cha umaskini.

Ndugai aliyetangaza kujiuzulu nafasi ya uspika Januari 6, mwaka jana, alitoa majibu hayo jana wakati akiongea na wananchi wa Jimbo lake la Kongwa Jijini Dodoma jana na msingi wa majibu hayo aliwataka vijana  waache kuchagua kazi ya kufanya kama wanahitaji kufanikiwa.

Hata hivyo Lema ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini amemjibu Ndugai kupitia kwenye mtandao wake wa kijamii wa Twitter kwa kudai “Umenikumbusha, nikukumbuke. Subiri kidogo,”amejibu Lema.

Katika mazungumzo yake ya jana Jumapili, Ndugai aliwaambia wananchi wa jimbo hilo, ili waachane na tabia ya kumuona mtu aliyefanikiwa kwa kufanya jitihada zake binafsi kuwa ni adui ni lazima wafanye kazi ikiwemo biashara halali na inayoingiza kipato kizuri.

“Kwa hiyo kijana na wewe anza kwa biashara yako halali, kazi ni kazi acheni na mtu anayesema wamelaaniwa sijui wamefanyaje labda amelaaniwa yeye,” amesema Ndugai.

Ndugai amefafanua kuwa  mtu anayesema vijana wabodaboda wamelaaniwa  basi atakuwa amelaaniwa mwenyewe huku akiwaeleza kazi ni kazi ilimradi iwe halali na inaingiza kipato.

“Wewe chagua kazi uone, wewe kama mamantilie fanya kazi yako vizuri tunza fedha andelea kukuza biashara yako, itafika mahali utamiliki hoteli na utafikia mahali nyota mbili hadi tano,”amesema.

Ndugai alienda mbali kwa kudai hata wafanyabiashara wakubwa kama Bakhressa alianza hana chochote, mara fundi viatu lakini kwa sasa ni tajiri mkubwa lakini biashara yake kubwa anauza maandazi.  

“Lakini wewe kijana nikikuambia uanzishe biashara ya maandazi mtaanza kusema nifanye biashara ya maandazi mimi, sisi wengine tatizo letu tunachangua kazi bila kujua tunaanza huku chini.

 “Kwamba biashara ile inalaana lakini biashara yenye laana Wachungaji na Mashekh watatuambia lakini mimi sijasikia wakisema ukifanya biashara ndogondogo ya maandazi na chapati au bodaboda ni laana ya mwenyezi Mungu,”amesema.

Ndugai wakati anawaeleza hayo alikuwa anawapitisha kwenye historia yake hadi anakuja kuwa mbunge wa jimbo hilo na kutoa wito kwa vijana kufanyabiashara yeyote iliyohalali wapate fedha wawekeze kwani hatua za kupitia kwenye magumu ni hatua yakufikia mafanikio.