Lema atua Tanga ahoji majengo ya kale, kilimo

Muktasari:

  • Akizungumza katika mkutano wa hadhara jijini Tanga, Godbless Lema amesema anasikitishwa kuona majengo ya kale yakibomolewa wakati yangeweza kutumika kitega uchumi cha kivutio cha kitalii kama ilivyo kwa nchi nyingine ikiwamo Morocco.

Tanga. Mwenyekiti wa Chadema, Godbless Lema amesema kama rasilimali zilizopo za bandari, majengo ya kale na ardhi yenye rutuba itatumia vizuri mkoa huo utaingiza fedha za kigeni za kuihudumia Tanzania kwa sekta zote.

Amesema anasikitishwa baada ya kuona majengo ya kale yakibomolewa wakati yangeweza kutumika kitega uchumi cha kivutio cha kitalii kama ilivyo kwa nchi nyingine ikiwamo Morocco.

Lema ameyasema hay oleo Machi 20 alipokuwa akiwahutubia wakazi wa Jiji la Tanga katika uwanja wa Madina.

Amesema viongozi na watendaji mkoani Tanga hawatumii muda wao kuweka mikakati ya kuinua uchimi wa wananchi, Mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla badala yake wanaweka mipango yenye kuwadidimiza wananchi kiuchumi.

"Niwaaambie wataalamu na viongozi wa CCM msibomoe majengo ya zamani ni utajiri mkubwa unavutia watalii wengi ambao wanakimbilia kuyaona kuliko hata twiga au tembo hifadhini," amesema Lema.

Kuhusu bandari, Mwenyekiti huyo ambaye yupo mkoani Tanga kwa ziara ya kikazi amesema ni kubwa ambayo inaweza kuzihudumia nchi za Maziwa makuu na kuongeza ajira ya vijana mkoani Tanga badala ya kukimbilia kuendesha bodaboda.

"Kama viongozi mliowachagua wangekuwa na mipango ya kuwainua kiuchumi,wangejikita katika kuiwezesha bandari ya Tanga ambayo ingeweza kutoa ajira kwa idadi kubwa ya wana-Tanga," amesema.

Kuhusu kilimo Lema ameeleza kushangazwa kwake na kitendo cha Tanzania kuwa na njaa wakati ipo ardhi yenye rutuba na maji yenye kuweza kutumika kwa umwagiliaji.

"Abu Dhabi ni jangwa lakini wanalima ngano na yenye kutosheleza nchi na kuuza nchi za nje, halikadhalika ni jangwa lakini ni maarufu kwa kilimo cha matunda, kwa nini Tanzania kuwe na njaa?" amesema Lema.

Kuhusu kazi ya kuendesha pikipiki maarufu kwa jina la bodaboda, amepigilia msumari akisema hawezi kuomba msamaha kwa kauli yake kuwa ni kazi ya laana, kwa sababu anaangalia miaka 30 ijayo Tanzania itakuwa katika hali gani.

"Baada ya miaka michache ijayo kama viongozi waliopo wataendelea kuwapotosha vijana kuwa bodaboda ni kazi nzuri tutakosa hata mafundi wa bomba,” amesema.

Awali Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Yosepha Komba amezungumzia kero katika Bima ya afya akisema dosari iliyopo katika Mpango wa Bima ya Afya wa kuondoa kifurushi cha Toto kuwa kinatakiwa kupingwa kwa kuwa kinawanyonya wananchi waliomasikini.