Ndugai: Viongozi tuepuke fedheha

Ndugai: Viongozi tuepuke fedheha

Muktasari:

Kauli ya aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai ya kuwataka viongozi wa kuchaguliwa kujipima kabla ya kugombea tena nafasi hizo katika chaguzi zijazo ili kuepuka aibu ya kushindwa, imewaibua viongozi wa siasa.

Bahi/Moshi. Kauli ya aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai ya kuwataka viongozi wa kuchaguliwa kujipima kabla ya kugombea tena nafasi hizo katika chaguzi zijazo ili kuepuka aibu ya kushindwa, imewaibua viongozi wa siasa.

Ndugai, ambaye ni Mbunge wa Kongwa (CCM), alisema yeye hatagombea tena nafasi hiyo kwenye uchaguzi mkuu 2025 na kuwataka viongozi wengine kujipima na kama wanaona kuna ugumu wasigombee, ili kuepuka aibu ya kukataliwa na wananchi.

Kutokana na kauli hiyo, viongozi mbalimbali wa kisiasa na wa dini, wamemuunga mkono wakisema baadhi ya wabunge na madiwani walioingia 2020 na viongozi wa Serikali za Mitaa walioingia 2019, nao wanapaswa kujipima.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alikwenda mbali zaidi na kueleza uchaguzi huru 2025 ndio utakuwa kipimo cha kukubalika kwao.

Kauli hiyo ya Ndugai inathibitisha orodha ndefu ya baadhi ya viongozi maarufu wa kisiasa na wengine wakiwa wamewahi kushika nafasi nyeti serikalini, lakini waliangushwa ama kwenye kura za maoni ndani ya CCM au kwa wapiga kura.

Miongoni mwao ni Waziri mkuu mstaafu, John Malecela aliyekuwa Mbunge wa Mtera na mwaka 2010 aliangushwa na Livingstone Lusinde katika uchaguzi wa ndani wa CCM. Pia, Ester Bulaya wa Chadema alimwangusha Steven Wasira wa CCM katika jimbo la Bunda mjini mwaka 2015.

Wengine ambao waliwahi kuwa mawaziri lakini wakaangushwa ni Rita Mlaki, aliyeangushwa na Halima Mdee, Christopher Chiza aliyeangushwa na Kasuku Bilago wa Chadema katika uchaguzi mkuu 2015. Hata hivyo, baada ya Bilago kufariki dunia Mei 26, 2018, Chiza alirejea tena bungeni baada ya kuibuka mshindi katika uchaguzi mdogo. Katika orodha ya waliowahi kuangushwa yumo pia, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha aliyeangushwa na Ezekiah Wenje wa Chadema katika uchaguzi wa mwaka 2015 Jimbo la Nyamagana.

Mbali na hao, wengine wenye majina walioangushwa ni Monica Mbega wa CCM aliyeangushwa na Mchungaji Peter Msigwa katika jimbo la Iringa Mjini mwaka 2010.

Hawa Ghasia aliangushwa na Shamsia Mtamba wa CUF na Ally Keissy aliyeangushwa na Aida Khenan wa Chadema katika uchaguzi mkuu uliopita.

Hawa wote walikuwa wanasiasa wakongwe na walioshika nyadhifa za juu, huku wakionekana pia kuwa na ushawishi, lakini mwishowe waliangushwa pasipo kutarajia.


Alichokisema Ndugai

Kauli ya Ndugai, aliyezaliwa Januari 21, 1963, aliitoa juzi katika Kijiji cha Mtitaa wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, wakati akitoa salamu za rambirambi katika msiba wa waziri wa zamani wa uchukuzi, William Kusila.

Ndugai alisema Kusila alitangaza kuachia ubunge mwaka 2010 wakati watu walikuwa wanampenda, na hivyo kuwashtua wengi kwa kuhoji ni kwa nini anaachia madaraka wakati bado alikuwa na uwezo wa kushinda ubunge. “Viongozi tujifunze kuiga mfano wa huyu mwenzetu. Ndiyo nilishasema mapema kuwa 2025 nami nitanyanyua mikono kule Kongwa ili niachie wengine,” alisema Ndugai, ambaye alijiuzulu uspika baada ya kupishana kauli na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Mtu unapaswa kujipima kwanza, ukiona kuna ugumu hata kama umetumika miaka mitatu achia nafasi hiyo wachukue wengine kuliko kusubiri aibu,” alisema Ndugai, bila kufafanua kama naye ameona ugumu wa kushinda tena au ni hiari.

Kufikia 2025 Spika huyo mstaafu atakuwa ameliongoza jimbo la Kongwa kwa miaka 25 mfululizo, kipindi ambacho ni kirefu ukilinganisha na miaka aliyoongoza Kusila katika jimbo la Bahi kabla ya kuachia ngazi mwenyewe mwaka 2010.

Ndugai alizungumza kauli hiyo akimtolea mfano Kusila katika kipindi cha uhai wake kwamba, aliamua kwa hiari yake kutangaza kutogombea ubunge baada ya kutumikia vipindi vinne mfululizo kati ya 1990 hadi 2010.

Kusila alifariki Agosti 21, 2022 jijini Dar es Salaam, alikokuwa amepelekwa kwa matibabu na mwili wake ulizikwa juzi, huku mamia ya watu wakihudhuria, wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa, Serikali, viongozi wa dini na wananchi.

Mbali na kujipima hilo, Ndugai aliwaomba viongozi wanapostaafu warudi vijijini walikotoka ili wakajipime na kuyaishi maisha ya wengine, kwani hapo ndipo watatambua kama sera walizozitunga zilikuwa na manufaa au hazikufaa kabisa.

Kuhusu maisha ya Kusila, alimweleza kama kielelezo na mfano wa kuigwa kwa mambo mengi, ikiwamo shughuli za kilimo, mazingira na kuishi kijijini ambavyo kwake aliwaambia waombolezaji kuwa, ameiga yote ya Kusila na kufanikiwa.

Alisema kwa watunga sera kurudi vijijini kunasaidia kujitafakari kama sera na sheria walizozipitisha zina msaada au zipo kwa sababu zilitakiwa kuwepo, akisema kuna baadhi ya mambo wakienda huko wanajiuliza kama sera zilipitishwaje.

Alimwelezea Kusila katika kipindi cha uhai wake kuwa alikuwa ni mtu aliyepinga rushwa hadharani na kukataa uonevu, lakini alama kubwa ni jinsi alivyopambana kuondoa njaa mkoani Dodoma.


Alikimbia furushi la fedha

Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), George Simbachawene alisema wanasiasa wengi wanapaswa kujifunza maisha ya Kusila, ambaye Taifa lilijua weledi wake na kueleza aliwahi kulikwepa furushi la fedha nyingi zilizopelekwa na mmoja wa wafanyabiashara wakubwa ili afanye uamuzi wa upendeleo.

Simbachawene alisema mpaka sasa mfanyabiashara huyo bado yupo, na kwamba alipeleka fedha nyingi akitaka Kusila azipokee halafu wakubaliane namna ya kufanya. Hata hivyo, akashangaa kukataliwa na kuitiwa maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), jambo lililomkimbiza.

Waziri huyo aliagiza viongozi walioko madarakani kuishi kama watu wenye hofu ya Mungu, ili wawe na mchango kwa Taifa badala ya kuwa mzigo kwa mambo machafu na uonezi yanayofanywa na baadhi yao kwa wananchi.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alimweleza marehemu Kusila kama alama ya ukumbusho kwenye kazi yake kutokana na jinsi alivyojenga msingi mzuri wa kuigwa.

Senyamule alisema Kusila alikuwa ni mkuu wa mkoa wa saba kwa Dodoma tangu Uhuru, lakini hadi anachukua kijiti yeye Senyamule ambaye ni wa 16, bado jina lake linatajwa kwa alama zake.


Alichosema Mbatia na Lema

Mbatia alisema ni sahihi viongozi walioingia 2019 na 2020 kujipima kama watapita chaguzi zijazo, akisema hiyo inatokana na namna walivyoingia kiasi kwamba baadhi wamekosa alichodai kuwa ni ushirikiano kutoka kwa wananchi.

“Kwa vile CCM ilishatamka kuhusu Katiba mpya, hebu tuache maneno twende kwenye vitendo na tunapo pa kuanzia ama rasimu ya Jaji Warioba au Katiba Inayopendekezwa. Tukae chini kabla ya 2025 ili wajitathmini vizuri,” alisema.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema alisema msimamo na ushauri wa Ndugai ni mzuri, lakini akamtaka awashauri wale walioupata ubunge na udiwani kwa hila mwaka 2020 nao wajipime.