Ndugu wahoji alipo mtoto wa wazazi waliofariki dunia

Muktasari:

Miili ya watumishi saba wa Halmashauri ya Kiteto waliopoteza maisha kwa ajali ya gari imeagwa jana, huku utata ukitawala alipo mtoto (miezi minane) wa wazazi waliofariki dunia.


Kiteto. Miili ya watumishi saba wa Halmashauri ya Kiteto waliopoteza maisha kwa ajali ya gari imeagwa juzi, huku utata ukitawala alipo mtoto (miezi minane) wa wazazi waliofariki dunia.

Mtoto huyo alikuwa miongoni mwa abiria tisa waliokuwa kwenye gari la wagonjwa la Kituo cha Afya Sunya lililokuwa limepata ajali eneo la Pori namba moja Kata ya Partimbo Novemba 7, 2022.

Baada ya ajali hiyo alikimbizwa Hospitali ya Mkoa Dodoma na baadaye alichukuliwa na watu waliojitambulisha ni ndugu wa baba yake.

Hata hivyo, jana baadhi ya ndugu waliokataa kutaja majina yao walisema wanashangaa kutomuona mtoto katika msiba huo.

Wakati miili inaagwa hakuna taarifa rasmi iliyotolewa alipo mtoto huyo, huku ndugu hao wa mama yake wakihoji watu waliokabidhiwa mtoto.

Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Pascal Mbota alisema hali ya mtoto huyo ipo salama.

“Siamini kilichotokea; hiki kichanga kilikuwa kimepakatwa na mama yake Catherine Asenga walipoanza safari, mpaka ajali hiyo inatokea walikuwa wote lakini mama na baba wamefariki, sasa imekuwaje kichanga kubaki salama, hii ni mipango tu ya Mungu,” alisema.

Katika ajali hiyo, watumishi saba wa Halmashauri ya Kiteto walipoteza maisha, huku dereva wa gari hilo, Juma Mbaruku (45) akipelekwa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma kwa matibabu zaidi.

Baada ya ajali hiyo ilielezwa kuwa mtoto huyo ni miongoni mwa waliopelekwa Hospitali ya Dodoma kuchunguzwa afya na ilibainika kuwa yuko salama.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Charoline Mthapula akizungumza na waombolezaji wakati wa kuagwa miili hiyo alitoa pole kwa wafiwa na kuonya madereva kuwa makini barabarani.

“Haya yote ni mapenzi ya Mungu, nilipopata taarifa za ajali hii saa 12 jioni niliumia sana na ilipofika saa sita usiku nikajulisha kifo cha Catherine Asenga Thadei, mama wa kichanga hicho aliyefariki wakati akiandaliwa kukimbizwa kwenda Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu.”

Abasi Famao, mmoja wa wananchi Kiteto alisema kunusurika kwa kichanga hicho ni fundisho na fumbo kwa wanadamu kuwa hakuna linaloweza kufanyika bila mapenzi ya Mungu.