Vifo ajali iliyoua mume, mke vyafika saba

Muktasari:

Ajali hiyo iliyotokea jana Jumatatu Novemba 7, 2022 jioni katika eneo la Pori namba moja Kata ya Partimbo wilayani Kiteto mkoani Manyara imehusisha gari la wagonjwa kugongana uso kwa uso na gari dogo.

Kiteto. Idadi ya vifo vilivyosababishwa na ajali ya gari iliyotokea eneo la Pori Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara imefika saba baada ya majeruhi mmoja kufariki akiwa katika Hospitali ya Dodoma.

Ajali hiyo ilitokea jana Jumatatu Novemba 07, 2022 baada ya gari la kubeba wagonjwa kugongana uso kwa uso na gari lingine aina ya Prado.

Jana, taarifa zilithibitisha vifo vya watumishi sita wa Serikali, Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, wakiwamo mke na mume.

Hata hivyo, leo Jumanne Novemba 8, 2022 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara (RPC), George Katabazi amesema mtu mwingine alifariki dunia baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Dodoma kwa ajili ya matibabu zaidi baada ya kutolewa katika hospitali ya Kiteto.

Miongoni mwa waliofariki katika ajali hiyo ni wanandoa Agapiti Kimaro na Catherine Mathei.

Wanandoa hao, Agapiti ambaye ni Mkuu wa Shule ya Esamatwa huku Catherine akiwa muuguzi, wameacha mtoto wa miezi nane.

Wanandoa ambao ni miongoni mwa watu sita walifariki dunia katika ajali gari iliyotokea eneo la Pori namba moja Kata ya Partimbo wilayani Kiteto Mkoani Manyara.

Kwa mujibu wa Kamanda Katabazi, wengine waliofariki katika ajali hiyo ni pamoja na; Joseph Bizuku na Kadidi Saidi ambao wote ni wauguzi, madaktari wawili Edward Makundi na Nickson Mhongwa pamoja na mtumishi wa maabara Celina Nyimbo.

Majeruhi waliopo katika Hospitali ya Dodoma wakipatiwa matibabu ni dereva wa gari hilo la wagonjwa lililopata ajali Juma Mbaruku (45) na dereva wa dereva Prado, Method Malick (55).

Majeruhi wengine ambao wamelazwa katika hospitali ya Kiteto ni Ibrahim Selemani (71) na Mbaraka Shabani (44).

Jana, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mbaraka Batenga akiwa Hospitali ya Kiteto alisema ajali hiyo ilihusisha gari la wagonjwa la Kituo cha Afya Sunya lililokuwa limepeleka mgonjwa Hospitali ya Wilaya ya Kiteto likirudi likiwa limebeba watumishi kurejea eneo la kazi Sunya liligongana uso kwa uso na gari dogo aina ya Prado.

"Ajali hii imehusisha gari letu la afya ‘ambulance’ la Kituo cha Afya Sunya ambalo limegongana uso kwa na gari lingine dogo aina ya Prado na kusababisha vifo vya watu sita na majeruhi watano wamepelekwa hospitali ya Dodoma, wangine wawili wanaendelea na matibabu hospitali ya Wilaya ya Kiteto," alisema Batenga.