NEC: Chadema walitupatia majina ya wateule viti maalum

Friday November 27 2020

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk Wilson Mahera leo Ijumaa Novemba 27, 2020 amesema katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika alimuandikia barua  Novemba 19, 2020 yenye orodha ya majina ya wanachama wanaopendekezwa kuteuliwa kuwa wabunge wa viti maalum  na kwamba tume hiyo ilitumia orodha hiyo kuteua wabunge wa viti hivyo.

NEC imeeleza hayo wakati kikao cha kamati kuu ya Chadema kikifanyika leo jijini Dar es Salaam kuwajadili wanachama wao 19 ambao Novemba 24, 2020 waliapishwa kuwa wabunge wa viti maalum mjini Dodoma  jambo lililopingwa na chama hicho na kueleza kuwa hakikuyapitisha majina yao na kuitaka tume hiyo kusema ukweli.

Baada ya  wanachama hao kuapishwa, Mnyika alifanya mkutano na wanahabari na kueleza kuwa hakuna kikao kilichokaa na kupitisha majina hayo na kuyapeleka NEC lakini leo tume hiyo imemtaja Mnyika kuwa aliwasilisha majina hayo.

Katika taarifa yake kwa umma, Mahera amesema, “ifahamike kwamba katibu mkuu wa Chadema alimuandikia mkurugenzi wa NEC barua yenye kumbukumbu namba C/HQ/ADM/20/TU/05/141 ya  Novemba 19 ambayo iliwasilisha orodha ya majina ya wanachama wanaopendekezwa kuteuliwa kuwa wabunge wa viti maalum.”


“Tume ilitumia orodha iliyowasilishwa na Chadema kuteua wabunge wa viti hivyo. Hivyo, wabunge wanawake wa viti maalum wa Chadema waliteuliwa kwa kuzingatia taratibu zote za kikatiba na kisheria.”

Advertisement

Mahera amesema kuanzia Septemba 26, tume hiyo imekuwa ikipokea barua kutoka kwa vyama mbalimbali zenye mapendekezo ya wanawake wabunge na madiwani wa viti maalum.

 “Septemba 26 tume ilipokea kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM)  na Novemba 19 ilipokea kutoka Chadema. Mapendekezo ya wabunge wanawake wa viti maalum kwa Chadema yaliwasilishwa tume kwa barua.”

“Mnamo Novemba 20 tume katika kikao chake iliteua wabunge na madiwani wanawake wa viti maalum kwa kuzingatia matakwa ya katiba na sheria,” alisema Mahera huku akieleza kuwa si kweli kwamba  tume iliteua wabunge wa Chadema ambao majina yao hayakuwasilishwa kwa kuzingatia taratibu.


Advertisement