Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NEC yatangaza matokeo ya Urais majimbo 158

Muktasari:

Kwa upande wa majimbo ya Zanzibar, mgombea wa CCM, Dk John Magufuli anaendelea kuongoza na kufuatiwa kwa mbali na Mgombea wa Chadema, Tundu Lissu na Bernard Membe wa ACT Wazalendo.

Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetangaza matokeo ya urais katika majimbo 158 ambayo ni sawa na asilimia 60 ya majimbo yote 264 ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage wakati akiahirisha shughuli ya utangazaji wa matokeo hayo jana usiku Saa 6:33 na kueleza kuwa kazi hiyo inaendelea leo Ijumaa Oktoba 30, 2020 kuanzia Saa 3 asubuhi.

Katika siku ya kwanza ya utangazaji wa matokeo hayo, NEC imeweza kutangaza matokeo ya urais kwa zaidi ya nusu ya majimbo ya uchaguzi na huenda mchakato huo wa kutangaza matokeo ambao umeingia siku ya pili, ukakamilika leo na mshindi kutangazwa.

“Leo tumeweza kutangaza asilimia 60 ya majimbo yote 264 ya Tanzania Bara na Visiwani. Kesho (leo) tutaendelea na majimbo mengine kwa kadri tunavyoyapata,” alisema Kaijage.

Katika matokeo hayo yaliyotangazwa, mgombea wa CCM, Dk John Magufuli anaongoza kwa wingi wa kura akifuatiwa kwa mbali na mgombea wa Chadema, Tundu Lissu huku mgombea wa NRA, Leopold Mahona naye akifanya vizuri kwa majimbo ya Tanzania Bara.

Katika jimbo ya Kongwa, Dk Magufuli anaongoza kwa kura 126,262 sawa na asilimia 97.25 wakati Lissu akipata kura 2,686 sawa na asilimia 2.07 na Mahona akishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 303 sawa na asilimia 0.23.

Katika jimbo la Mlalo mkoani Tanga, Magufuli amepata kura 48,548 (asilimia 94.41) wakati Lissu akipata kura 1,981 (asilimia 3.85) na Mahona akipata kura 333 (asilimia 0.65).

Magufuli ameongoza pia katika jimbo la Kisarawe mkoani Pwani kwa kupata kura 27,663 (asilimia 86.17) wakati Lissu akipata kura 2,626 (asilimia 8.18) na kufuatiwa na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF kwa kura 1203 (asilimia 3.75).

Katika jimbo la Butiama mkoani Mara, Magufuli amepata kura 59,729 (asilimia 90.25) wakati Lissu amepata kura 5,665 (asilimia 8.56) na Mahona wa NRA akipata kura 317 sawa na asilimia 0.48.

Kwa upande wa majimbo ya Zanzibar, Magufuli ameendelea kuongoza na kufuatiwa kwa mbali na Lissu wa Chadema pamoja na Bernard Membe wa ACT Wazalendo.

Katika jimbo la Mkwajuni mkoani Kaskazini Unguja, Magufuli amepata kura 11,324 sawa na asilimia 84.48, Lissu amepata kura 1,506 (asilimia 12.15) na Membe amepata kura 436 (asilimia 3.32).

Katika jimbo la Nungwi, Magufuli amepata kura 8,824 sawa na asilimia 69.55 wakati Lissu akipata kura 2,075 (asilimia 16.35) na Membe akipata kura 1,086 sawa na asilimia 8.36 ya kura zilizopigwa.

Vilevile, katika jimbo la Tumbatu, Magufuli amepata kura 10,234 sawa na asilimia 82.60 wakati Lissu akipata kura 1,506 (asilimia 12.15) na Membe akipata kura 436 (asilimia 3.32).