Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Marekani, Iran hapajaeleweka

Muktasari:

  • Licha ya kutiwa saini kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Iran na Marekani, bado mataifa hayo yameonekana kushambuliana.

Washington/Tehran. Marekani imeendelea kuishambulia Iran kwa usiku wa nane mfululizo, huku mvutano kati ya mataifa hayo ukiongezeka, licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi mmoja uliopita.

Mashambulizi hayo yamekuja saa chache baada ya Marekani kutangaza kuwa wanajeshi wake wawili wameuawa nchini Jordan na mwingine mmoja kutoweka baada ya shambulio lililodaiwa kufanywa na Iran.

Tukio hilo limeongeza hofu ya kurejea kwa vita kati ya mataifa hayo, vinavyotajwa kuwa na athari kubwa kwa uchumi wa dunia na usalama wa Mashariki ya Kati.

Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (Centcom) ilisema mashambulizi ya anga yalianza saa 6:00 usiku kwa saa za Marekani, yakifanyika kwa maelekezo ya Rais Donald Trump.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mashambulizi hayo yalilenga kupunguza uwezo wa Iran wa kutishia usafiri wa kibiashara katika Mlango wa Hormuz na kuyadhoofisha majeshi ya Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), yaliyohusishwa na mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa Marekani nchini Jordan.

Baadaye, Centcom ilithibitisha kuwa mashambulizi hayo yalifanikiwa kulenga vituo vya ufuatiliaji wa pwani, mifumo ya ulinzi wa anga na miundombinu mingine ya kijeshi ya Iran.

Vyombo vya habari vya Iran viliripoti kuwa maeneo karibu na Sirik kusini mwa nchi hiyo na Shadegan karibu na mpaka wa Iraq yalilengwa, ingawa mamlaka za Iran zilisema hakuna vifo wala uharibifu wa miundombinu ulioripotiwa.

Katika hatua ya kulipiza kisasi, Iran ilitangaza kufanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya mali na vifaa vya kijeshi vya Marekani katika Kambi ya Al-Adiri na Kituo cha Anga cha Ali Al Salem nchini Kuwait.

Televisheni ya Taifa ya Iran ilisema mashambulizi hayo ni sehemu ya operesheni zinazoendelea dhidi ya maslahi ya Marekani na washirika wake katika eneo la Ghuba.

Marekani ilisema vifo vya wanajeshi wake wawili vilitokea Ijumaa, Julai 17, 2026, huku mwanajeshi mwingine akiwa bado hajulikani alipo.

Takwimu hizo zimefanya idadi ya wanajeshi wa Marekani waliouawa tangu kuanza kwa vita hivyo kufikia 16, huku zaidi ya 420 wakijeruhiwa.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, amesema kupitia mtandao wa X kuwa kujitoa kwa wanajeshi hao kumeongeza dhamira ya Marekani kuendelea na operesheni zake za kijeshi dhidi ya Iran.

Wakati huohuo, Iran imeonekana kupanua mashambulizi yake dhidi ya washirika wa Marekani katika eneo la Ghuba. Ripoti mbalimbali zinaonesha kuwa Kuwait, Bahrain, Jordan na Saudi Arabia zimekuwa miongoni mwa maeneo yaliyolengwa baada ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya madaraja, vituo vya umeme na miundombinu mingine muhimu ndani ya Iran.

Katika taarifa iliyonukuliwa na vyombo rasmi vya habari vya Iran, Kiongozi Mkuu wa nchi hiyo, Ayatollah Mojtaba Khamenei, amesema hatua za Marekani zimeonesha kuwa ahadi na makubaliano yaliyotiwa saini na Rais Trump hayana uaminifu wala thamani yoyote.

Ameonya kuwa Marekani inaweza kukabiliwa na gharama kubwa zaidi na fedheha endapo itaendelea na mashambulizi hayo.

Mahali alipo Khamenei bado hakujafahamika, jambo linalozua maswali mengi kuhusu usalama wake wakati wa mzozo huo unaoendelea.

Vita hivi vilianza mwishoni mwa Februari baada ya Marekani na Israel kuanzisha mashambulizi dhidi ya Iran kwa lengo la kudhoofisha programu zake za nyuklia na makombora pamoja na makundi yanayoungwa mkono na Tehran katika eneo la Mashariki ya Kati.

Tangu wakati huo, hali ya usalama imeendelea kudorora na kusababisha hofu ya kuvurugika kwa usambazaji wa nishati duniani.

Nchini Kuwait, jeshi la nchi hiyo limesema limefanikiwa kudungua makombora ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani zilizorushwa na Iran.

Hata hivyo, baadhi ya askari wa zimamoto na wafanyakazi wa sekta ya mafuta walijeruhiwa wakati wakishughulikia madhara ya mashambulizi hayo.

Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu wa Iran wamedai kushambulia Kambi ya Arifjan na kuharibu kituo cha rada katika Kituo cha Anga cha Ali Al Salem. Shirika la Mafuta la Kuwait limesema moja ya mitambo yake iliharibiwa baada ya kushambuliwa mara kadhaa.

Iran pia imedai kushambulia maeneo ya kijeshi nchini Bahrain na Jordan yanayotumiwa na Marekani. Hata hivyo, taarifa hizo hazikuthibitishwa.

Saudi Arabia nayo imetoa tahadhari za usalama kwa wakazi wa maeneo ya Al-Kharj na Yanbu kutokana na taarifa za mashambulizi. Al-Kharj lina kituo cha kijeshi kinachohifadhi wanajeshi wa Marekani, wakati Yanbu ni moja ya vituo muhimu vya usafirishaji wa mafuta kupitia Bahari Nyekundu.

Wakati mapigano yakiendelea, Mlango wa Hormuz umeendelea kuwa kitovu cha mvutano. Marekani imesema inalinda usafiri wa baharini katika eneo hilo, huku Iran ikiituhumu kwa kutaka kudhibiti njia hiyo muhimu ya biashara ya kimataifa.

Takribani asilimia 20 ya mafuta yote yanayosafirishwa duniani hupitia katika mlango huo.

Wizara ya Afya ya Iran imesema watu 50 wameuawa na zaidi ya 500 kujeruhiwa kutokana na mashambulizi ya Marekani katika kipindi cha wiki tatu zilizopita.

Kwa upande wake, Marekani imeendelea kusisitiza kuwa operesheni zake zinalenga miundombinu ya kijeshi pekee.

Umoja wa Ulaya na nchi za Ghuba zimetoa wito kwa Iran kusitisha mara moja mashambulizi yote dhidi ya meli na kuhakikisha Mlango wa Hormuz unabaki wazi kwa usafiri wa kimataifa.