Necta yaonya udanganyifu, darasa la nne, kidato cha pili wakianza mitihani

New Content Item (1)

Muktasari:

  • Wakati darasa la nne na kidato cha pili wakitarajiwa kuanza mitihani yao ya upimaji kwa siku tofauti, Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limeendelea kuzionya shule zinazopanga kufanya udanganyifu kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Dar es Salaam. Wanafunzi milioni 1.62 wa darasa la nne wanatarajia kuanza mitihani yao ya upimaji (SFNA) kesho Jumatano Oktoba 25 na 26 mwaka huu, huku Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) likikemea udanganyifu kwa wanafunzi.

Wakati wao wakimaliza, Jumatatu ya Oktoba 30 hadi Novemba 9 mwaka huu wanafunzi 759,573 wa shule za sekondari 5,546 Tanzania Bara wanatarajia kuanza mitihani yao ya upimaji kidato cha pili (FTNA).

Akizungumza na wanahabari, Dk Said Mohamed ambaye ni Katibu Mtendaji wa Necta amesema kati ya wanaofanya mtihani wa darasa la nne wavulana ni 828,591 sawa na asilimia 48.95 na wasichana ni asilimia 51.05.

“Pia kati ya wanafunzi milioni 1.692 waliosajiliwa kufanya upimaji wa kitaifa wa rarasa la Nne mwaka 2023, asilimia 94.84 watafanya kwa lugha ya Kiswahili asilimia 5.16 watatumia lugha ya kiingereza ambayo wamekuwa wakiitumia katika kuiifunzia,” amesema Dk Mohamed.

Idadi ya wanaofanya mtihani huu wa upimaji ni pungufu kwa asilimia 5.26 ikilinganishwa na wanafunzi milioni 1.71 waliofanya mtihani huo mwaka uliopita.

Akiendelea kufanya uchambuzi wa wanafunzi wa darasa la nne, amesema wenye mahitali maalum wapo 6,402 ambapo kati yao 1,074 ni wenye uoni hafifu, 93 ni wasioona, 1,240 wenye ulemavu wa kusikia, 2,209 ni wenye mtindio wa akili na 1,786 ni wenye ulemavu wa viungo vya mwili.


Kidato cha pili

Siku ya nne baada ya darasa la nne kumaliza mitihani yao, wavulana 353,807 na wasichana 405,766 kutoka sekondari 5,546 Tanzania Bara watakaa darasani kwa ajili ya mitihani yao ya upimaji kidato cha pili.

Kati yao, wanafunzi wenye mahitaii maalum ni 1,382 ambapo 683 ni wenye uoni hafifu, 82 ni wasioona, 290 wenye ulemavu wa kusikia na 309 ni wenve ulemavu wa viungo vya mwili na 18 wenye ulemavu wa akili.

“Upimaji huu muhimu kwani unatuwezesha kujua kiwango cha wanafunzi katika kumudu stadi za juu za kusoma, kuandika na kuhesabu. Kwa upande wa kidato cha pili hupima uwezo na uelewa wa wanafunzi katika yale yote wallyojifunza kwa kipindi cha miaka miwili a masomo yao ya Sekondari,” amesema Dk Mohamed.

Ametumia nafasi hiyo kuwataka wasimamizi wahakikishe kuwa wanafanya kazi ya usimamizi kwa weledi na kwa kuzingatia kanuni za mitihani na miongozo waliyopewa ili kila mwanafunzi husika apate haki yake.

“Baraza halitarajii kuona mwanafunzi yeyote kujihusisha na vitendo vya udanganyifu. Mwanafunzi yeyote atakayebainika kufanya udanganyifu, matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa Kanuni za Mitihani,” amesema Dk Mohamed.

Pia Necta imewataka wamiliki wa shule kutambua kuwa shule zao ni vituo maalum va mitihani na hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha ufanyikaji wa Upimaji huo.

“Baraza halitosita kukifuta kituo chochote cha mitihani endapo litajiridhisha pasipo shaka kuwa uwepo wake unahatarisha Usalama wa Upimaji wa Kitaifa,” amesema Dk Mohamed.