Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NHIF yakamata kadi 1,346 zinazotumika na wasio wanachama wake

Muktasari:

  • Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umekamata kadi za bima 1,346 zilizokutwa zinatumika na watu wasio wanachama wa mfuko huo.

Dar es Salaam. Kumbe si kila anayekwenda hospitali na kadi ya bima ya afya ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kupata huduma ni mwanachama wa mfuko huo.

Wapo wanaofanya janjajanja ya kuazima kadi za wanachama na hatimaye kwenda kupata huduma ilhali si stahiki yao.

Hilo linathibitishwa leo Jumanne Julai 11 na NHIF kupitia uhakiki wa wanachama wake, iliyoanza kuifanya Juni 1, mwaka huu katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Arusha na Dodoma.

Kwa kipindi cha mwezi mmoja wa uhakiki huo, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga amesema kadi 1,346 zimekamatwa zikitumika na watu wasio wanachama.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Konga amesema mbali na kuzikamata kadi hizo, uchambuzi unafanyika kubaini gharama zilizotumika kuhudumia watu wasio wanachama kwa kutumia kadi hizo.

"Kama zilitumika fedha lazima mwanachama arejeshe fedha, uchambuzi unaendelea kubaini kiasi cha fedha kilichotumika kinyume na taratibu," amesema.

Kufanya hivyo, amesema ni kinyume na utaratibu na yeyote atakayebainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Hata hivyo, amesema uchunguzi unaendelea kufanyika kubaini imewezekanaje watoa huduma kushindwa kutambua wasio wanachama wanaotumia kadi za wanachama.

Mbali na hilo, Konga amesema uhakiki huo ndani ya mwezi mmoja umebaini wanachama 2,490 wameacha kadi zao vituoni.

"Tunaendelea kuchunguza ili kujua je, mtoa huduma amemtaka mwanachama aache kadi ili baadae atengeneze dai, au mwanachama ameisahau," amesema.

Kingine kilichobainika katika uchunguzi huo, amesema ni baadhi ya wanachama kudurufu kadi za NHIF.

"Wanachama wanatoa nakala na kuziwasilisha katika vituo vya kutolea huduma za afya au wanatumiana kwa WhatsApp hii ni kinyume cha sheria mwanachama anapaswa kwenda na Kadi yake halisi," amesema.