Nini kina Whozu? kuna mambo 'mobu' kwenye simu...

Whozu, Mbosso na Bilinenga. Wamepigwa stop kudili na muziki kwa miezi kadhaa. 'Maskanka' sijui 'mabapa', yalirusha stimu zao masela na kufanya video wanayoijua wao na pisi zao. Mamlaka ikakunjua makucha.

Tuachane na hao masela. Kuna kile kinachoendelea kwa 'madenti' wengi wa kike, haswa wanaosoma shule za kutwa. 'Samutaimu' hunilazimisha niunge mkono kitendo cha Magufuli. Alipokataa kusomesha 'madenti' waliopigwa 'vibendi'.

Kuna upuuzi unaoendelea kwa 'madenti' wengi. Utafiti niliofanya mwenyewe kwa kipindi kifupi. Nimegundua 'madenti' ambao wana fursa ya kumiliki simu hutumia kwa michongo isiyoendana na sekta yao ya 'kidenti denti.'

'Smati foni' hurahisisha kupata elimu mbadala kwa njia ya mitandao. Lakini 'madenti' wengi hutumia kwa matumizi mengine. Ambayo nayo ukitumia 'smati foni' ni rahisi sana kupata au kupatwa kimahaba.

'Madenti' wengi hutumia 'smati foni' kwa mbanga za mapenzi zaidi. Kutazama picha na video za ngono na 'ishu' za aina hiyo. Na ushawishi huanzia kwenye ‘profile’ picha za 'wasapu'.

Kisha ushawishi unaendelea kutamalaki kwenye mipozi ya picha kule insta. 'Viklipu' vya Tik Tok na 'snap chati'. Huko hakuna cha jiografia wala 'siviksi'. Hakuna cha 'baioloji' wala 'litrecha'. Ni ngono tu.

Uwepo wa 'smati foni', mambo 'mobu' ikiwa ni pamoja na mfumo mzima wa maendeleo na namna ya kuishi. Yamebadilika huku 'madenti' hasa wa kike wakibadilika zaidi. Kifupi ni majanga mbaya.

Wakati baadhi ya shule zikiwabana juu ya matumizi ya simu, kuna baadhi siyo tu wameshindwa kuwabana, bali hata kufuatilia hawataki. Madenti wengi wana 'smati foni', tena za gharama kubwa ambazo haziendani na vipato vya familia zao. Kuna wazazi huwapa watoto wao simu kwa sababu maalumu na zenye uzito. Lakini 'madenti' wanazitumia kwenye udwanzi tofauti na matarajio ya wazazi.

Wazazi huwapa ili kuwajulisha wakipata tatizo, lakini wao hutumia kimapenzi.

Waathirika wakubwa ni wasichana, ambao mara nyingi hukosa ujasiri wa kujisimamia. Kwa ambao wazazi hawana uwezo wa kuwanunulia simu hupata vishawishi vya kujiingiza katika ngono za kibwege ili wapate mkwanja wa simu.

Sababu kubwa ya kujiingiza kwenye uhusiano wa kingono kwa wasichana wengi, ni ile hali ya tamaa ya kumiliki simu kama wenzao, na madhara yake huwa ni mimba. Kitu ambacho 'Anko Magu' aligoma kusomesha.

Baadhi ya wazazi wamekuwa wazembe sana, kiasi cha kushindwa kudhibiti mienendo ya watoto wao. Na kusababisha wakibaki kushuhudia  simu za thamani zikimilikiwa na watoto wao kuliko wazazi husika.

Ukiachana na simu hata pamba za 'madenti' wakiwa nje ya shule. Ni ya utata kinoma, wengi wanapiga pamba ambazo hushawishi hisia za masela kitaa. Na mengine yakidhalilisha utu wa mtoto wa kike. Noma sana.

Pamba zingine ambazo ni kama  kivuli cha 'madenti' kufanya ngono ni vazi takatifu la hijab na dera. Hutembea nayo kwenye begi za shule. 'Madenti' wenye pepo la ngono, huyavaa ili kujificha wakienda kwenye miadi wa vidume.

Wapo 'madenti' ambao huaga 'homu' kama wanakwenda 'skonga', wakifika njiani huvaa dera au hijab kisha kwenda wanakojua wao. Kifupi tatizo la ngono kwa wanafunzi linahitaji mjadala mpana wa kitaifa.

Naomba ieleweke kutoeleweka kuwa, hata nyimbo za kina Whozu, wanaimba na kufanya kinachofanywa kitaani. Wanaiimbia jamii yao ambayo siyo tu huyapenda bali wanayafanya kiufundi kuliko video za kina Whozu.

Jiongeze

Banza Stone alama ya dansi

Ramadhan Masanja 'Banza Stone'. 'Ticha wa Maticha'. 'Le Jeneral'. Fundi wa sauti, utunzi, vionjo na upangiliaji wa ala za muziki. Mabega yake yalitumika kuibeba Twanga Pepeta yote, ikiwa ni pamoja na wanamuziki, wamiliki, vyombo mpaka mashabiki. Mwili wake umelala pale Sinza Makaburini.

Hatunaye Msukuma huyu maarufu zaidi kisanaa kupata kutokea. Katika wakati wake kipaji kilitumika kuwaweka kando Wacongo na mbwembwe zao. Bendi zote zilizojaza Wacongo zilikufa kifo cha mende. Baada ya balaa la Banza kuamsha popo kwa machizi dansi katika viunga vya Dar es Salaam.

Wakati Wacongo waliigiza kilekile kikichofanywa kwenye rap na kina Def Defao katika mitaa ya Lubumbashi na Kinshasa. Yeye Banza Stone aliwalia denge kwa kuingiza vionjo kwa lugha ya Kiswahili. Achana na Chamukware na Ndombolo. Banza alienda sawa na Nambriiiiiiiiiiiiiieeee.

Mwamba kabisa.

Jide alitumia muda vyema

Amepita njia tofauti na wasichana wengi wasiojielewa. Jide asingezingatia muda kama tabia za wasichana wengi, huenda hii leo asingekuwa pale. Aliutumia muda vyema wa kuandika mashairi, kufanya mazoezi na kukesha studio.

Hakuwa mtoto wa kishua. Pia akawa tofauti na wasichana wa uswazi kutegemea pesa za wanaume. Akawa na hasira na maisha huku akiamini ataishinda kupitia muziki. Akaweka nia na kuzingatia kazi yake hivi sasa anakula matunda.

Jide hakupenda sifa za kijinga. Wakati wasichana wa mjini wakipambana kupata nafasi za kuuza sura kwenye kurasa za udaku. Jide alijenga uadui na habari za udaku. Kasikilize nyimbo zake utaelewa. Angekuwa mpenda sifa angechafua sana kurasa.