Nisher kuagwa ‘Nyumba ya Matamko,’ wasanii wamlilia
Mtaarishaji wa video za muziki wa kizazi kipya, Nick Davie maarufu kama Nisher enzi za uhai wake.
Muktasari:
- Mtaarishaji wa Video za Muziki wa Kizazi Kipya, Nick Davie maarufu kama Nisher, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Desemba 12, 2023; ambapo wasanii mbalimbali katika majiji ya Arusha na Dar es Salaam ambao wamewahi kufanya naye kazi wameendelea kutoa salamu zao za pole.
Arusha. Shughuli zote za msiba wa Mtaarishaji wa video za muziki wa kizazi kipya, Nick Davie maarufu kama Nisher, zinatarajiwa kufanyika kuanzia leo jioni katika nyumba ya matamko Kisongo, wilayani Arumeru.
Katika eneo hilo la nyumba ya matamko ndipo baba wa msanii huyo, Nabii Dk GeorDavie huendesha mahubiri yake katika Kanisa la Ngurumo za Upako.
Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 12, 2023 msaidizi wa nabii huyo, Apostle Sekela amesema ratiba kamili ya shughuli za mazishi itatolewa baadaye leo.
"Bado sijapewa ratiba kamili lakini shughuli zote zitafanyika hapa Nyumba ya Matamko Kisongo," amesema.
Nisher alifariki saa nane na dakika tisa usiku wa kuamkia leo Desemba 12 jijini Arusha na tayari baba yake amethibitisha kutokea kwa msiba huo.
Wasanii mbalimbali katika majiji ya Arusha na Dar es Salaam ambao wamewahi kufanya kazi na Nisher, wametoa salamu za pole na kuomboleza msiba huo.
Msanii Shabani Juma, maarufu kama Shah Bang amesema siku ya leo ni ya huzuni sana kwake baada ya kupata taarifa za msiba huo, kwa sababu ndiye alikua msanii wa kwanza kumshirikisha.
"Nisher tulishirikiana kwenye wimbo wangu ulioitwa ‘Maisha ya Ujana’ ulifanyika Bongo Records kwa mtayarishaji P funky Majani, ambapo pia Nisher ndiyo alitayarisha video ya wimbo na ni video hiyo ndiyo ilimtambulisha katika tasnia ya muziki Tanzania," amesema.
Kwa mujibu wa Shah Bang, baada ya video ya wimbo huo kutoka, alikutana na msanii Joh Makini ambaye aliipenda na kuamua kwenda Arusha kufanya kazi na marehemu, “Joh Makini alifanya naye kazi kupitia wimbo ‘Sijuitii’ na kuanzia hapo Nisher akawa maarufu.
"Baada ya hapo alifanya video nyingi ambazo zilifanya vizuri ndani na nje ya nchi, kwa hiyo kifo chake ni pigo kubwa katika tasnia ya muziki wa Arusha na Tanzania kiujumla,” amesema msanii huyo.
Amemueleza Nisher kama mtu aliyekuwa na kipaji kikubwa katika kuandaa video za muziki na alikuwa na ndogo za kuja kuwa muandaa bora wa muziki nchini.
Msanii mwingine Jordan Peter amesema wamepoteza mtu muhimu sana katika tasnia ya muziki ambaye alifanya uwekezaji mkubwa katika kazi zake.
Hata hivyo, familia ya Nisher, bado haijaweka wazi chanzo cha kifo cha msanii huyo.