NMB yatoa misaada yenye thamani ya Sh53.4 milioni Lindi
Muktasari:
- Benki hiyo imeendelea kuelekeza nguvu zake katika kusaidia sekta za elimu na afya pamoja na kutoa misaada mbalimbali wakati wa majanga.
Lindi. Benki ya NMB imetoa msaada wa bati 900 kwa shule za msingi, sekondari na zahanati katika Halmashauri ya Mtama, mkoani Lindi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha miundombinu ya elimu na afya katika eneo hilo.
Mbali na bati hizo, benki hiyo pia imetoa vifaa tiba katika Hospitali ya Nyangao na Hospitali ya Rufaa ya Sokoine kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii.
Akizungumza leo Alhamisi Juni 25, 2026, wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo, Meneja wa NMB Kanda ya Kusini, Olipa Hebel amesema wameendelea kuelekeza nguvu katika kusaidia sekta za elimu na afya pamoja na kutoa misaada mbalimbali wakati wa majanga.
Amesema kwa zaidi ya miaka 10 sasa mfululizo, NMB imekuwa ikitenga asilimia moja ya faida yake kwa ajili ya kurudisha sehemu ya mafanikio yake kwa jamii.
“Tumeleta bati 900 kwa shule za msingi, sekondari na zahanati zilizopo Halmashauri ya Mtama. Pia tumetoa madawati na meza kwa shule mbalimbali,” amesema Hebel.
Ameongeza kuwa imetoa pia baiskeli za kubebea wagonjwa, vitanda vya kubebea wagonjwa, vitanda vya kujifungulia pamoja na makabati kwa Hospitali ya Nyangao.
“Vilevile tumetoa benchi za kusubiria wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Sokoine iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Lindi. Misaada yote tuliyotoa ina thamani ya Sh53.4 milioni,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Mtama, Boniface Fungo, ameishukuru NMB kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za jamii.
Ameahidi kuwa vifaa vilivyotolewa vitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwataka wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kusaidia maendeleo ya halmashauri hiyo.
“Tunaishukuru Benki ya NMB kwa msaada mkubwa mlioutoa. Tunawahakikishia kuwa vifaa hivi vitatumika kama ilivyokusudiwa. Pia tunatoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kuchangia maendeleo ya Halmashauri ya Mtama ili kuharakisha maendeleo ya wananchi,” amesema Fungo.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mihogoni, Clemence Mwambe amesema shule hiyo ina uhitaji wa vyumba saba vya madarasa zaidi kutokana na ongezeko la wanafunzi.
Amesema kwa sasa shule hiyo ina vyumba tisa vya madarasa na kwamba msaada uliotolewa na NMB utasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
“Tunashukuru NMB kwa msaada huu mkubwa. Utasaidia kuboresha mazingira ya elimu, kupunguza utoro na kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira bora zaidi, jambo litakalosaidia kuongeza ufaulu wa kitaaluma,” amesema Mwambe.