Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NSSF kuuza mradi wa Dege Eco Village

Muktasari:

  • Kutokana na sababu tofauti zilizoifanya NSSF ishindwe kuukamilisha mradi huo sasa inawakaribisha wawekezaji wa kimataifa kuuendeleza.

Dar es Salaam. Baada ya kusuasua kukamilika kwa mradi wa Dege Eco Village kwa thamani ya dola 653 milioni za Marekani (zaidi ya Sh1.3 trilioni), Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) lililokuwa linautekeleza limetangaza kuuza kwa mwekezaji mwingine atakeyevutiwa nao.

Ujenzi wa mradi huo wa mji mpya wa Kigamboni jijini Dar es Salaam ulioanzishwa na NSSF mwaka 2014 ulisimama tangu Januari 2016 ukidaiwa kufisidi zaidi ya Sh179 bilioni hivyo kutokamilika kwa nyumba za kifahari, hoteli, maduka makubwa, eneo la wazi la mapumziko, baa, shule, hospitali, kumbi za mikutano, nyumba za ibada na migahawa.

Taarifa iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba na kusambazwa leo, Jumanne Oktoba 25 imetangaza kutafutwa kwa mzabuni atakayeuendeleza mradi huo.

“NSSF inakusudia kuuza mradi mzima wa Dege Eco Village, shirika halitowajibika tena baada ya mauzo haya. NSSF inakaribisha zabuni zilizofungwa kuununua mradi huu kwa viwango vya kimataifa vilivyoainishwa kwenye Kanuni za Ununuzi wa Umma zilizochapishwa kwenye gazeti la Serikali namba 446,” inasomeka sehemu ya taarifa ya NSSF.

Kwa wawekezaji watakaovutiwa kuuendeleza mradi huo uliosimama kwa miaka saba sasa, NSSF imesema wanaweza kuutembelea huko Rasi ya Dege iliyopo Kigamboni jijini hapa ili kuukagua na kujiridhisha na mandhari yake kuanzia saa 4:00 asubuhi mpaka saa 7:00 mchana wa Novemba 3.

Zabuni zote, shirika hilo limesema zinapaswa kuwasilishwa mpaka Novemba 14, saa 9:00 alasiri kabla hazijafunguliwa mbele ya waombaji wote watakaokuwa wamejitokeza kwenye ukumbi wake uliopo ghorofa ya saba katika Jengo la Benjamin William Mkapa.