Nyasi zilivyogeuka dili vita ya ukame Monduli

Wadau wa masuala ya mazingira wakiwa na baadhi ya wanufaika wa mradi wa uzalishaji wa nyasi kwenye maeneo yaliyoathirika na ukame wilayani Monduli,wakionyesha mfano wa nyasi hizo katika shamba darasa lililopo eneo la Selela,wilayani Monduli mkoa wa Arusha

Monduli. Hivi unafahamu namna nyasi zinavyoweza kuboresha maisha, hasa katika jamii zinazoathirika na ukame? Ukizungumza na Nengai Laizer utaelewa zaidi.

Yeye ni mmoja wa wanufaika wa mradi wa uzalishaji nyasi unaolenga maeneo yaliyoathirika na ukame kutokana na mabadiliko ya tabianchi, akiwa kati ya wanawake zaidi ya 100 kutoka vijiji vinne vilivyopo kata ya Losirwa wilayani Monduli mkoani Arusha.

Kupitia vikundi vya kijamii, wanawake hao wamewezeshwa kupanda nyasi kama mbinu mojawapo ya kurutubisha ardhi ili kuirejesha katika hali nzuri.

Nyasi hizi hutumika kuezeka nyumba, ila muhimu zaidi, zimekuwa njia mojawapo ya kinamama kujiingizia kipato, wakiziuza kwa ajili ya malisho ya mifugo, au mbegu.

Hatua hii inawapa uhakika wa kipato kiasi na inawawezesha kutunza makazi yao na mifugo yao, huku ikisaidia jamii hizo kuondokana na mfumo wa maisha ya kuhamahama.

"Hii imetusaidia kwa sababu kule mlimani tumeacha kwenda na hapa hapakuwa na kitu kinaota ila kwa sasa baada ya wataalamu kuchukua udongo na kwenda kuufanyia uchunguzi wametuletea mbegu hizi na tunapanda nyasi hizi na tumeweka mlinzi, tunadhibiti eneo hili mifugo haiingii," anasema Nengai, anayeishi Kijiji cha Selela.

Saingo Ngalalai wa Kijiji cha Baraka anaeleza kipindi cha kiangazi wanawake walikuwa wakikumbana na changamoto hasa ya kwenda kutafuta majani ya kuezeka nyumba ila kwa sasa wameondokana na changamoto.  Muhimu zaidi, mradi huo umewaondoa katika hali ya utegemezi kwa kuwapa kipato.

"Tumewezeshwa tukachimba makinga maji, tukapanda mbegu. Tulikata tamaa; awali palikuwa pakavu, tukashtuka haitakubali na sasa mbegu imekubali. Tumefurahia huu mradi na baada ya kupanda yale majani kuna mbegu tofauti zimekubali na mimea mingine imetokea," anasema.

Mwenyekiti wa kikundi cha Naisho Selela, Maria Mukare, anaeleza kilimo hicho kimekuwa na manufaa kwao kwani wameondokana na kukaa majumbani bila kuwa na shughuli za kiuchumi na badala yake sasa wanajishughulisha.

"Tunajihusisha na mambo ya kupanda nyasi za majani na kuvuna mbegu na sisi wanakikundi tunajinufaisha kwa kuuza. Sisi tumepata manufaa, tumefundishwa namna ya kupanda mbegu na kutunza na tumeshavuna mbegu, na mradi utatusaidia kujikwamua kiuchumi.”

Anaongeza: “Sisi wamama wa kifugaji hatuna biashara nyingi ambazo tunafanya ila tulivyopata shamba hili la kikundi tukawa hatukai nyumbani tunajishughulisha kuhangaika na shamba hadi kuvuna mbegu.”

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Monduli, Adil Mwanga ameiambia Mwananchi kuwa mradi huo umeweza kusaidia kuhuisha maeneo ya ardhi yaliyokuwa yanakabiliwa na ukame uliotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Mwanga anaeleza kilimo cha nyasi ni njia muafaka ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi na itasaidia kuondoa hali ya jamii kuhamahama kipindi cha kiangazi kwa ajili ya kutafuta malisho, na inawezesha vijiji nufaika kujiingizia kipato.

"Faida za majani ni kuwa yanasaidia kupata chakula cha mifugo, kuuza mbegu ndiyo faida kubwa na sisi ni mara ya kwanza kusikia mradi kama huu – na kilo ya majani ni Sh25,000. Ukipiga kwa haraka ni kubwa na inaletaja faida kwa haraka.”

Christina Shusho ambaye ni balozi wa Justdiggit, waliowezesha mradi huo wakishirikiana na Trias, Lead Foundation na Baraza la Wanawake Wafugaji (PWC), amesema utekelezaji katika vijiji hivyo vinne umeongeza ustahimilivu wa mabadiliko ya tabia nchi, na umeonekana kuanza kusaidia kubadilisha maisha ya wanawake na kuwainua kiuchumi.

“Ujuzi huu (wa kuzalisha nyasi) utabaki kwenu. Fanyeni kwa bidii kwa sababu mbali na kuboresha uchumi wenu, mtaboresha pia mazingira.”

Mradi huo wa kilimo cha nyasi umetekelezwa kwa kiwango cha ekari 44 mpaka sasa, kati ya ekari 100 zilizokusudiwa, ukilenga kunufaisha zaidi ya wanawake 100 katika vijiji shirika.

Makala hii imeandalikwa kama sehemu ya ushirikiano ya Mwananchi Communications Limited na Justdiggit katika kuangazia jamii za kitanzania zinavyokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.