Ofisa Takukuru aeleza uhusika watuhumiwa kesi ya Sabaya

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imeelezwa uhusika wa washitakiwa wanaodaiwa kuunda genge la uhalifu lililodaiwa kuratibiwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya

Arusha. Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imeelezwa uhusika wa washitakiwa wanaodaiwa kuunda genge la uhalifu lililodaiwa kuratibiwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya,wakati walipoenda kuomba na kupokea rushwa ya Sh90 milioni.

Uhusika wa washitakiwa hao umeelezwa leo Januari 4,2022 mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo,Patricia Kisinda,na shahidi wa 13 wa jamhuri ambaye ni Ofisa uchunguzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini(Takukuru),Ramadhan Juma.

Akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili wa Serikali Mwandamizi,Felix Kwetukia,shahidi huyo alidai washitakiwa hao wakiongozwa na Sabaya,Januari 22 mwaka jana walienda kuomba na kupokea rushwa ya Sh 90 milioni kutoka kwa mfanyabiashara Francis Mrosso.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 27 ya mwaka huu,mbali na Sabaya watuhumiwa wengine ni Enock Mnkeni,Watson Mwahomange,John Aweyo,Sylvester Nyegu,Jackson Macha na Nathan Msuya.

Shahidi huyo ambaye kabla ya kueleza uhusika wa kila mshitakiwa siku hiyo ya tukio,aliwatambua washitakiwa wote saba akiwemo Sabaya ambapo alidai watuhumiwa hao walikamatwa katika maeneo tofauti ikiwamo Dar Es Salaam na Moshi.

Shahidi huyo amedai kuwa katika upelelezi wake aliweza kubaini uhusika wa kila mshitakiwa wakati wakitekeleza tukio hilo la kuomba na kupokea rushwa toka kwa Mrosso.

Amedai katika upelelezi wake alibaini kuwa Sabaya aliunda na kuratibu genge la uhalifu na kwamba katika genge hilo alikuwa na vijana.

"Enock alikuwa moja ya vijana walioshiriki katika genge hilo ambaye alikuwa mlinzi mkuu wa Sabaya na siku hiyo ya tukio pale kwa Mrosso alitambulishwa kama afisa usalama wa taifa.Na alikuwa amevalia kaunda suti ya dark bluu na kutokana na mavazi yake alimtisha Mrosso,"



Aliendelea kueleza mahakama kuwa Mwahomange majukumu yake yalikuwa kutafuta taarifa mbalimbali zenye madhaifu kutoka kwa wafanyabiashara wilayani Hai,Kilimanjaro na Arusha na kuzipeleka kwa Sabaya ambaye akishazipata hupanga namna ya kuzifanyia utekelezaji.

"Januari 20,2021 Watson alitumwa na Sabaya kwa  Mrosso  kama kiigizo cha kwenda kutengeneza pump na hakupewa risirti ya EFD aliandikiwa risiti ya mkono baada ya kuelezwa mashine imeharibika,"alidai

"Januari 22,2021 Watson alipelekwa kwa Mrosso  akiwa amefungwa pingu na Sabaya wakiwa na lengo la kumhadaa Mrosso kuwa Watson amekamatwa na watu wenye mamlaka na kusababisha Mrosso aingiwe hofu,"

Juma aliieleza mahakama mshitakiwa wa nne,Aweyo,alikuwa miongoni mwa walinzi wakuu wa Sabaya na alishiriki tukio la kuomba na kupokea rushwa na alikuwa anaimarisha ulinzi kuanzia kwa Mrosso hadi benki ya CRDB tawi la Kwa Mrombo.

Alidai Nyegu alikuwa msaidizi mkuu na wa kudumu wa Sabaya na siku ya tukio alikuwa na Sabaya eneo la Aim Mall,alikuwa sambamba na Sabaya.

"Walipofika kwa Mrosso,Macha alitambulishwa na Sabaya kama Afisa kutoka Mamlaka ya Mapato nchini(TRA) na aliingia benki akiwa na Mrosso na alimuweka chini ya ulinzi mkali na walitoka pamoja wakiwa na fedha hizo,"alidai na kuongeza

"Msuya naye ni miongoni mwa vijana waliokuwa wanaunda genge hilo na alikuwa dereva na siku ya tukio alikuwa anaendesha gari aina ya VX Toyota Land Cruiser lenye namba T 144 CZU na alikuwa na wenzake Aweyo na Sadick Kiiza ambaye hajapatikana hadi sasa hivi,"

Katika hatua nyingine mahakama hiyo ilihamia nje ya Kituo Jumuishi cha utoaji haki (Arusha),wakati gari linalodaiwa kuwa la Sabaya ambalo ni kielelezo cha 10 mahakamani hapo,shahidi huyo alipoenda kulitambua.

Baada ya shahidi kumaliza kutoa ushahidi wake wa msingi Waili wa utetezi Mosses Mahuna,aliiomba mahakama itoe ahirisho hadi kesho kwa sababu shahidi huyo ni muhimu na amezungumza masuala mengi kwa siku tatu hivyo wangetamani kupata wasaa wa kumhoni maswali ya msingi.

Wakili wa Serikali Mwandamizi Tarsila Gervas,alisema upande wa jamhuri hawana pingamizi na ombi hilo na kuomba nao wanapoomba ahirishi isiwe kwamba wanakwamisha kesi hiyo kukamilika.

Hakimu Kisinda aliridhia ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Januari 6, ambapo alieleza kuwa leo kesho, ana majukumu mengine ya kiofisi ambayo anapaswa kuyashughulikia.