Ole Nasha kuzikwa kijijini kwake

Ole Nasha kuzikwa kijijini kwake

Muktasari:

  • Mwili wa aliyekuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), William Ole Nasha utazikwa Jumamosi kijijini kwake wilayani Ngorongoro, Arusha.


Dodoma/Arusha. Mwili wa aliyekuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), William Ole Nasha utazikwa Jumamosi kijijini kwake wilayani Ngorongoro, Arusha.

Ole Nasha, ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Uvuvi na Mifugo, na Elimu, Sayansi na Teknolojia alifariki dunia usiku wa kuamkia juzi jijini Dodoma.

Akizungumza jana, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema: “Familia imeomba ndugu yao azikwe Jumamosi na sisi tumelipokea hili, tumeona halina shida na mwili utaagwa kitaifa leo saa tano asubuhi katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma”.

Wakati huohuo, mashirika yasiyo ya kiserikali Mkoa wa Arusha yamepokea kwa mshtuko kifo cha Ole Nasha, yakisema alikuwa na mchango mkubwa.

Mkurugenzi wa Mtandao wa Mashirika ya Wafugaji, Wawindaji na Waokota Matunda (PINGOs Forum), Edward Porokwa alisema mara ya mwisho kuwasiliana naye ilikuwa Jumapili iliyopita.

“Katika maisha yake Nasha nitamkumbuka kwa uchapakazi, alipenda kuona maendeleo katika jamii yake na Tanzania kwa ujumla,” alisema Porokwa.

Mratibu wa Mtandao wa Mashirika ya Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa alisema watamkumbuka Nasha kwa kuwaunganisha wananchi wa Ngorongoro na kuwapa taarifa za maendeleo ya jimbo hilo katika kundi WhatsApp.

Ofisa miradi wa shirika la Wanahabari la Watetezi wa Jamii za Pembezoni (Maipac), Andrea Ngobole alisema Ole Nasha alikuwa kiungo muhimu cha shirika hilo na wananchi na muda mwingi alishauri.

Mkurugenzi wa shirika la Utafiti, Maendeleo na Huduma kwa Jamii (Cords), Lilian Looloitai alisema kifo cha Ole Nasha ni pigo sio kwa wana-Ngorongoro pekee, bali jamii nzima, kwani alikuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya wananchi anaowawakilisha.