Ole Sendeka autaka tena ubunge 2025
Mbunge wa Simanjiro mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka, akizungumza kwenye kikao cha baraza la jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) cha wilaya hiyo, kilichofanyika mji mdogo wa Mirerani. Picha na Joseph Lyimo
Muktasari:
- Mbunge wa Simanjiro Mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka amesema atagombea tena ubunge mwaka 2025, huku akiwataka wote yenye nia kama yake kujitokeza na ‘kupambana’ naye uwanjani.
Mirerani. Mbunge wa Simanjiro Mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka amesema atagombea tena ubunge mwaka 2025, huku akiwataka wote yenye nia kama yake kujitokeza na ‘kupambana’ naye uwanjani.
Ole Sendeka aligombea na kushinda ubunge Jimbo la Simanjiro kwa mara ya kwanza mwaka 2005 hadi 2015 alipoangushwa James Ole Millya kabla ya kurudi tena mwaka 2020 hadi sasa.
Ole Sendeka akizungumza kwenye kikao cha baraza la jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Simanjiro kilichofanyika ukumbi wa Panama Mji Mdogo wa Mirerani, amesema bado ana uwezo na nguvu za kuwatetea wananchi wa eneo hilo.
"Uwezo wa kutumikia wana Simanjiro na kuwasemea wafugaji na wakulima bado ninao, nguvu za kupambana na changamoto za wachimbaji wa madini ya Tanzanite na kuzungumza Bungeni bado ninazo," amesema Ole Sendeka.
Amesema mwanasiasa yeyote mwenye uwezo, nia au hamu ya kugombea ubunge mwaka 2025 aingie ulingoni apambane naye.
"Kama una Mwanasiasa wako umemweka mfukoni mlete uwanjani mwaka 2025 ili tupambane mradi tuu msipokee bahasha kwani rushwa ni adui wa haki," ametahadharisha Ole Sendeka.
Mkazi wa mji huo John Melita amesema zama za mwisho za Ole Sendeka kuwa mbunge zimefika mwishoni kwani wana Simanjiro hawawezi kumchagua tena mwaka 2025.
"Muda wa Ole Sendeka kupumzika umefika, tunahitaji fikra mpya,” amesema Melita.
Hata hivyo, hoja ya Melita inapigwa na Mkazi wa Kata ya Endiamtu, Mashaka Jeroro ambaye amesema bado wana Simanjiro wanataka kuendelea kuongozwa na mbunge makini Ole Sendeka.
"Kazi ya mbunge ni kuchukua changamoto za wananchi wake na kuzifikisha sehemu husika ndivyo Ole Sendeka anavyofanya kwa hiyo panapo majaliwa tutamchagua tena," amesema Mashaka.