Prime
Rais wa Singapore akifika kwao atacheka sana
Leo Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam, anamaliza ziara yake Tanzania. Amekuwapo kwenye ardhi ya taifa lililoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, tangu Juni 8 (Jumatatu).
Kwa heri mgeni. Anapoondoka, kama nchi inabidi kujitafakari. Singapore, nchi ndogo, kisiwa, Mashariki ya Asia, lakini tajiri na iliyojengwa kisasa. Tanzania, nchi kubwa, Afrika Mashariki, inayopambana kujikwamua kutoka kwenye umaskini. Singapore, nchi iliyoendelea. Tanzania, nchi inayoendelea.
Singapore ina ukubwa wa kilometa za mraba 734 (haifiki hata 1,000). Tanzania ukubwa wake ni kilometa za mraba 947,300. Maana yake, Tanzania ukiigawa kwa ukubwa wa Singapore, unatengeneza nchi nyingine 1,291. Tanzania ina watu takriban 70 milioni, wakati Singapore idadi yake ni watu 6.1 milioni. Ukiwagawa Watanzania kwa idadi ya Wasingapore, unaweza kutengeneza Singapore 11 na nusu.
Tafakuri namba moja; Singapore na udogo wake, pato lake la ndani la taifa (GDP), ni dola 572.47 bilioni (Sh1,488.4 trilioni au Sh1.5 kwadrilioni). Tanzania, GDP ni dola 94 bilioni (Sh244 trilioni). Hesabu hiyo inakwambia kuwa mapato ya Singapore ni mara sita ya Tanzania. Yaani Tanzania zikiwa sita, zitalingana na Singapore moja. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Pato la mtu mmojammoja (GDP per capital), Singapore ni dola 97,134 (Sh252.5 milioni), kwa mwaka. Tanzania, pato la mtu ni dola 1,300 (Sh3.38 milioni), kwa mwaka. Inawekana hoja hii ikawa haina tija kwa sababu Singapore ina watu wachache ukilinganisha na Tanzania. Hata hivyo, baki na hoja kuhusu GDP ya Singapore dhidi ya Tanzania.
Tafakuri namba mbili; kiwango cha maliasili. Singapore haina kabisa. Wasongapore wanasikia kwa watu kuhusu madini, mafuta, gesi na maliasili nyingine. Hawana ardhi ya kilimo. Tanzania ni nchi yenye kila kitu. Ardhi kubwa kwa ajili ya kilimo, utajiri mkubwa wa madini, gesi, vivutio vya watalii, mbuga za wanyama zenye kuruhusu shughuli za uwindaji.
Singapore hawana maji safi. Wanategemea kuagiza kwa majirani zao, Malaysia. Tanzania ina utajiri wa maji safi. Maziwa makubwa kwa madogo, mito, chemchemi zisizo na idadi, mabwawa na maporomo yanayotiririsha maji kwa mwaka mzima. Sasa jiulize; kwa nini Tanzania ipo nyuma mno kwa Singapore?
Jibu ni uongozi. Singapore waligundua mapema nchi yao ni maskini wa maliasili. Walichofanya cha kwanza ni kuwekeza kwenye mtaji wa watu. Wamewasomesha raia wao vizuri, wanawafadhili kwa mafunzo, na kuwawezesha kibiashara na kiteknolojia. Hivi sasa, Singapore ni nchi mstari wa mbele katika maendeleo ya kiteknolojia.
Pili, waliona fursa ya kijiografia. Singapore, ipo kwenye kona muhimu wa Mlango Bahari wa Malacca, ambayo inaunganisha peninsula ya Malay na kisiwa cha Sumatra, Indonesia. Ni mlango bahari mfupi, lakini ndiyo kiunganishi cha Bahari ya Hindia na Pacific. Kwa kutambua hayo, Singapore walijenga moja ya bandari kubwa zaidi za mizigo duniani, vilevile bandari za udhibiti (control-tower ports), zaidi iliunganisha uwezo wake wa bandari na mtandao wa anga wa usafirishaji mizigo.
Singapore ni matokeo makubwa ya uongozi wenye maono yenye uendelevu. Uzalendo wa viongozi ni mkubwa, na mifumo inayodhibiti watu kujinufaisha kwa mali za umma ni imara. Mifumo holela ya Tanzania, na maono yasiyo na mwendelezo, ni sababu nchi yenye kila kitu, isiyo na misukosuko ya majanga na vita, ipo nyuma mno ya taifa dogo lenye umaskini wa rasilimali.
Kama Singapore waliona watu ndiyo rasilimali namba moja. Mawazo hayohayo yangewekezwa Tanzania, maana yake taifa lingekuwa na mtaji mkubwa mno. Leo, vijana wanamaliza vyuo vikuu, wapo wenye shahada hadi mbili, wanaendesha taksi za mtandaoni, wengine bajaji na bodaboda. Wapo wamachinga. Nchi haiumii kuona rasilimali zinatumika vibaya mitaani.
Machi 23, 2015, Singapore ilimpoteza Baba wa taifa lao, wenyewe wanamwita Baba wa Uhuru (Father of Independence), Lee Kuan Yew. Lee alikuwa Waziri Mkuu wa Singapore tangu mwaka 1959 wakati taifa hilo lilipokuwa halijapata uhuru wa bendera na aliliongoza kuingia kwenye Shirikisho la Malaysia kisha kujitoa kabla ya baadaye kuiwezesha kujipatia uhuru kamili kutoka kwa UK mwaka 1965.
Katiba ya Singapore inaitambulisha Singapore kuwa Jamhuri ya mfumo wa Serikali ya Kibunge (parliamentary constitutional republic), kwa hiyo chama chenye wabunge wengi ndicho kinaunda serikali. Kutokana na hali hiyo, Lee akiwa kiongozi wa chama chake cha People's Action (PAP), moja kwa moja akawa waziri mkuu, na mwenye cheo hicho ndiye mtendaji mkuu mwenye mamlaka (key figure) wa Serikali ya Singapore.
Kwa nguvu hiyo, aliweka rekodi ya kuivusha Singapore kutoka kwenye uchumi wa dunia ya tatu mpaka ya kwanza ndani ya miaka 31 ya utawala wake. Aliachia ngazi kwa hiari yake Novemba 1990. Aliigeuza Singapore kutoka vijiji ndani ya bahari (vijiji vya uvuvi), na kuifanya kuwa jiji lililojengeka kisasa, tena lenye kuvutia zaidi kuliko miji mingi mikubwa ya Uingereza, Ufaransa na Marekani.
Lee anasifika kuifanya Singapore kuwa na hadhi sawa na mataifa makubwa ya Ulaya na kuifanya kuwa ya tofauti mno na mataifa mengine ya Bara la Asia. Alidhibiti rushwa na kuboresha huduma muhimu kwa wananchi wake. Hakika huwezi kuizungumzia Singapore na mabadiliko yake ya kiuchumi na kimaendeleo pasipo kumtaja Lee.
Kipindi cha utawala wa Lee, aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Taifa, Teh Cheang Wan, alituhumiwa kwa vitendo vya rushwa. Taarifa zilipomfikia Lee, aliiagiza Mamlaka ya Uchunguzi na Mashtaka ya Rushwa (CPIB), kumchunguza Teh. Kwa kiwewe, Teh alijiua kabla ya kufanyiwa uchunguzi kutokana na woga aliokuwa nao dhidi ya Lee. Hicho ni kipimo cha juu kuwa mifumo haikuwa na utani katika masuala ya mmomonyoko wa maadili ya uongozi.
Misingi iliyowekwa na Lee imekuwa na mwendelezo, hata muongo wa nne, baada ya yeye kuachia ngazi, na miaka 11, tangu kifo chake. Ni nafasi ya kujiuliza; Tanzania inakwama wapi? Kijiografia, nchi ipo pazuri. Bandari zipo, ufanisi wake je? Zinatosha kulingana na mahitaji? Utajiri wa rasilimali watu unachezewa, kama ambavyo maliasili zinavyofujwa kifisadi.
Leo, wakati wa kumuaga Rais wa Singapore, anayemaliza ziara yake nchini, inatakiwa nyuso ziwe chini kwa aibu. Maana, hakuna sababu yoyote Singapore kuwa mbele ya Tanzania, zaidi ya ukosefu wa maono sahihi, ubinafsi, ufisadi na mambo mengine hasi. Na kwa alivyoiona Tanzania, na utajiri wake, maendeleo duni ya miji, na watu wake wakiwa maskini, atacheka sana akifika kwao.