Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Operesheni ving’ora, vimulimuli kwenye magari yanukia

Dar es Salaam. Wakati baadhi ya watu wenye magari binafsi ya kifahari wakiyafunga ving’ora na vimulimuli, kisha kuviwasha wanapokuwa kwenye foleni ili kupita haraka, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhan Ng’azi amesema wanatarajia kurejesha operesheni ili kuwakamata wanaovunja sheria kwa kufunga vifaa hivyo.

Mtindo huo wa kuviwasha ving’ora na vimulimuli vilivyofungwa kwenye vyombo vya moto, unaelezwa unaendelea kuota mizizi na kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara yanayopita magari hayo.

Kwa kawaida matumizi ya ving’ora na vimulimuli ni kwa ajili ya magari ya polisi, majeshi ya ulinzi, zimamoto na uokoaji, magari ya kubeba wagonjwa na mengine yanayopata kibali kutoka Wizari ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali.

Katika uchunguzi uliofanywa na gazeti hili mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Mwanza, Tanga, Kilimanjaro na Arusha, magari hayo yenye namba za kawaida, wanaoyaendesha wakifika maeneo yenye foleni wanawasha ving’ora na vimulimuli ili kupata njia ya kupita.

Hata hivyo, Mwananchi ilipomtafuta Kamanda Ng’azi hivi karibuni kuhusu tatizo hilo alisema hilo ni kosa la jinai kwa sheria za usalama barabarani.

“Kama kuna mtu bado anaendeleza tabia hiyo tutarudisha operesheni yetu kali na tunatoa wito kwa yeyote tutakayemkamata amefunga gari yake king’ora au kimulimuli hatua zitachuliwa, kwa kuwa kisheria hatakiwi kuwa na kifaa hicho,” alisema Kamanda Ng’anzi.

Alisema katika operesheni hiyo wanayotarajia kuianzisha, watakaokamatwa wana vimulimuli na ving’ora, vitang’olewa na watashtakiwa kwa mujibu wa sheria za nchi ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia kama hiyo.

“Nikuhakikishie wanaofanya mtindo huo ni kosa la jinai kwa upande wa sheria za usalama barabarani, waliofunga ving’ora waviondoe wenyewe kabla ya kukamatwa na kushtakiwa,” alisema Kamanda Ng’anzi.

Kwa Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza kwenye pilikapilika hasa asubuhi na jioni, kunapokuwa na foleni zinazosababishwa na taa kuruhusu magari kupita kwa zamu, wenye magari hayo hutumia mwanya huo kupenya.

Licha ya mtindo huo kushamiri katika barabara za Dar es Salaam, bado matrafiki wanaosimama kwenye makutano wamekuwa hawafuatilii magari hayo kiasi cha wao kuendelea kutumia fursa hiyo.

Joseph Silvanus, anayefanya biashara ya fedha maeneo ya Mwenge alisema, “ni kweli kuna watu wanamiliki magari ya kifahari na wamefunga ving’ora wanasumbua barabarani, hasa muda wa asubuhi watu wanapokwenda kazini na jioni wanaporudi nyumbani.”

Alisema wakifika sehemu zenye foleni huwa wanawasha ving’ora na vimulimuli, madereva wa magari ya kawaida hususan daladala wamekuwa wakiyapisha magari ya aina hiyo.

“Mimi biashara yangu ni hii, nafungua asubuhi na kila siku magari ya ving’ora yanapita na ukiangalia yanakuwa na namba za kawaida, hizi Land Cruiser Prado TX na V8 Prado, watu wanakimbiza tu barabarani humu,” alisema Silvanus.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Said Juma, mwendesha bodaboda kituo cha Afrikasana akisema wakati mwingine wanapita njia isiyokuwa sahihi, jambo linaloweza kusababisha ajali.

“Nafikiri tunapaswa kujiuliza watu wanazipata wapi hizo taa? Kama tunajua basi mamlaka zizuie zisiuzwe kiholela, nchi za wenzetu kama unataka kununua rangi nyekundu na bluu lazima uende na barua kutoka mamlaka husika, sisi tunafanya hivyo?” alisema Juma.

Alisema hata kampuni za ulinzi, taa zao rangi ya orange (ya chungwa) lakini kuna wanamiliki taa hizo wanazitumia, nchi imekuwa na vurugu kila kona kiasi cha kila mtu kujiamulia cha kufanya.”

Mkazi wa Dodoma, Mary Msafiri alisema suala hilo halikuwepo awali, “lakini sasa tangu Serikali imehamia hapa, hali imebadilika, magari yamekuwa mengi, foleni nazo kama tulizokuwa tunazisikia huko Dar es Salaam, kwa hiyo mbinu za Dar es Salaam zinahamia huku.”


Kauli ya kamati ya Bunge

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje, Vita Kawawa alisema watu wanaofanya mtindo huo wanakiuka utaratibu na sheria, huku akieleza wao kama kamati walishatoa mapendekezo yao.

“Na katika mapendekezo yetu yale, Jeshi la Polisi lilisema kabisa watu wanaofanya mtindo huo litawachukulia hatua na walielekeza watu gani wanapaswa kufunga viong’ora baada ya sisi kutoa mawazo yetu,” alisema Kawawa.

Alisema kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi, kuna viongozi na taasisi maalumu ambazo gari zao zinapaswa kuwa na ving’ora, mathalani hospitali kwa kuwa na ambulance (magari ya wagonjwa), fire (magari ya zimamoto na ukoaji) na vyombo vilivyopo kwa mujibu wa sheria.

“Sasa kama hilo linaendelea ni muhimu akaulizwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, lakini sisi kama kamati kwa mujibu wa sheria tulishaeleza kwa sababu kuna wanaopaswa kuwa na ving’ora na wanapaswa wazingatiwe,” alisema Kawawa.

“Polisi wanapaswa kutoa maelekezo pale wanapoonekana watu wa namna hiyo basi wao wanajua ni hatua zipi wanapaswa kuzichukua katika kusimamia usalama barabarani,” alisema Kawawa.


Kilio cha madereva wa kawaida

Dereva wa daladala kutoka Segerea hadi Makumbusho, John Materu alisema wamiliki hao wanakera,huku akitolea mfano Barabara ya Segerea kuna mtu binafsi anamiliki Land Cruiser Prado kila kukiwa na foleni anawasha.

“Tukiwa barabarani tunachanganywa madereva na watumiaji wengine wa barabara kwa kushindwa kubainisha upi msafara wa viongozi na magari ya dharura na upi sio,” alisema Materu.

“Madereva wa daladala na watumiaji wengine kwa udhaifu wa kutokujua sheria wamekuwa wakimpisha wakijua kiongozi mkubwa na hata akipita mataa ya Tabata Reli, ambako kuna matrafiki (askari wa usalama barabarani) hawamsimamishi.

Materu alisema ni muhimu sheria ikafuata mkondo wake, huku akieleza wako wengi wenye mtindo huo na imefikia hatua akinunua gari ya kifahari anafunga king’ora.

“Kukipiga barabara nzima imekuwa kama fasheni bila kujua watumiaji wengine tunaumizwa na jambo hili na ukizingatia wanaowasha ving’ora tunajua ni watu wa kawaida,” alisema Materu.

Hata hivyo, Saimon Kumburu, dereva wa lori alishangaa kuona wanaopaswa kusimamia sheria wanawaangalia wenye mtindo huo kila siku, wanapita wakiwasha ving’ora.

“Wanatunyanyasa sana, inakuwaje wengine tunasota kwenye foleni, wao kina nani wanawasha na wanapita bila kusumbuliwa mbona unakuwa ubaguzi,” alisema Kumburu.