Operesheni ya siku 14 yanasa kilo 767.2 za dawa za kulevya

Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lyimo akizungumza na waandishi wa habari juu ya operesheni waliyoifanya katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga.

Muktasari:

Kati ya dawa zilizokamatwa, heroin ni kilo 233.2, methamphetamine kilo 525.67 na skanka kilo 8.33

Dar es Salaam. Bandari ndogo zilizorasimishwa na zisizo rasmi (bubu) zimetajwa kuwa lango la kuingizia dawa za kulevya nchini, huku baadhi ya boti za wavuvi zikitumika kuzifikisha nchi kavu.

Bandari hizo zimetajwa kuwa ni za Kunduchi na Mbweni zilizopo Dar es Salaam; na Bagamoyo iliyopo mkoani Pwani.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imesema hayo leo Aprili 22, 2014 ikitangaza kukamata kilo 767.2 za dawa za kulevya katika operesheni zilizofanyika kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga kuanzia Aprili 4, 2024 hadi Aprili 18.

Kati ya dawa zilizokamatwa, heroin ni kilo 233.2, methamphetamine kilo 525.67 na skanka kilo 8.33.

Mbali ya hayo, DCEA imesema watuhumiwa 21 wamehusika na dawa hizo miongoni mwao wapo wafanyabiashara wawili wakubwa wa dawa za kulevya wanaotarajiwa kufikishwa mahakamani leo.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Kamishna wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema katika tathmini iliyofanyika wamebaini dawa hizo zinapitishwa kupitia bandari zilizorasmishwa na zisizo rasmi zilizopo katika mwambao mwa Bahari ya Hindi.

“Tumebaini dawa hizi zinapitishwa kupitia bandari ndogo zilizorasimishwa wanachanganya na mizigo mingine, hususani bandari za Kunduchi na Mbweni (Dar es Salaam) na Bagamoyo,” amesema Lyimo.

Amesema watahakikisha wote wanaobainika kuhusika kusaidia upitishwaji wa dawa hizo wanachukuliwa hatua za kisheria, watakapothibitishwa hata ikiwa ni watumishi wa Serikali.

Amesema katika operesheni wanazofanya watahakikisha njia ya Kusini, ukanda wa Pwani ya Tanga, Dar es Salaam na Mtwara wanaongeza doria.

Lyimo amesema katika ukanda wa bahari kuna bandari bubu zaidi ya 600 zinazotumika kuingiza dawa za kulevya, hivyo wataongeza nguvu katika eneo hilo.

Amesema baadhi ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya wamekimbilia nje ya nchi na wanafanya biashara wakiwa huko kupitia makubaliano na baadhi ya wamiliki wa boti ndogo za uvuvi wa samaki.

“Wakishatuma dawa za kulevya kupitia majahazi, wanapofika katika kina kirefu cha bahari, wanawapigia simu wamiliki wa boti ndogo wanaenda kuchukua na kuzileta katika pwani ya Dar es Salaam na Zanzibar, halafu baadaye wafanyabiashara wengine wadogo wanakuja kupokea na kusambaza kulingana na maelekezo wanayopewa,” amesema Lyimo.

Amesema wamezitambua baadhi ya boti ambazo zinasadikiwa kutumika kubeba dawa za kulevya kutoka baharini, akieleza ukaguzi utafanyika na zitakazobainika zitataifishwa.

“Tuwape onyo wamiliki wa boti za kuvua samaki, kuna baadhi tunaendelea kuzifuatilia ili kuzikamata kuzihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya. Tutoe onyo kwa wamiliki wa boti ikiwa wanaendesha wenyewe au wamekodisha, wahakikishe hazitumiki kusafirisha dawa za kulevya,” amesema Lyimo.

Amesema baadhi ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya wameendelea kutumia vifungashio vyenye majina ya aina mbalimbali ya kahawa na chai kama vile organic coffee, cocoa, na green tea kwa lengo la kukwepa kutiliwa shaka wakati wakizisafirisha.

Hali hiyo amesema imefanya baadhi ya watu kusafirisha dawa hizo pasipo kujua ndani kuna nini jambo ambalo linawaweka hatarini.

Biashara na matumizi ya dawa za kulevya ni moja ya matishio ya kiusalama duniani kwa sababu vijana ndio kundi linaloathiriwa zaidi na dawa hizo.

Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, idadi ya vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa ni milioni 20.612

“Kati ya watuhumiwa wanaokamatwa, wengi wao wako katika kundi la vijana. Ikiwa kundi hili litaendelea kujiingiza kwenye biashara na matumizi ya dawa za kulevya litapoteza ustawi binafsi, Taifa litapoteza nguvu kazi na hatimaye kuhatarisha uchumi na usalama wa Taifa letu,” amesema Lyimo.

Operesheni ilivyokua

Kwa mujibu wa kamishna huyo, Aprili 4, 2024, katika eneo la Mikanjuni jijini Tanga watuhumiwa wawili walikamatwa wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroin kiasi cha gramu 329.412.

Aprili 8, 2024, katika eneo la Wailes Temeke Mtaa wa Jeshini, jijini Dar es Salaam zilikamatwa kilo 1.49 za dawa za kulevya aina ya skanka, watuhumiwa wawili walikamatwa.

Aprili 10, eneo la Zinga, Bagamoyo mkoani Pwani, zilikamatwa kilo 424.84 za methamphetamine.

“Watuhumiwa watatu walikamatwa kuhusika na dawa hizo na tarehe hiyohiyo katika eneo la Kunduchi, jijini Dar es Salaam alikamatwa mtuhumiwa mmoja akiwa na heroin gramu 158.24,” amesema Lyimo.

Aprili 14, 2024 eneo la Bandari jijini Dar es Salaam zilikamatwa kilo 4.72 za skanka, huku watuhumiwa watatu wakikamatwa.

Aprili 16, katika Kata ya Kunduchi, jijini Dares Salaam zilikamatwa kilo 232.69 za heroin na kilo 100.83 za methamphetamine zilizokuwa zinaingizwa nchini kupitia Bahari ya Hindi. Watuhumiwa tisa wakikamatwa.

Aprili 18, mtuhumiwa mmoja alikamatwa eneo la Bandari jijini Dar es Salaam akiwa na kilo 2.12 za skanka,” amesema.