Wasomi watajwa kuongoza matumizi ya dawa za kulevya

Muktasari:
- Utafiti mdogo katika mikoa ya Mbeya, Arusha, Mwanza na Geita kwa waraibu 125, wamebaini zaidi ya asilimia 50 ni vijana wasomi ndio watumiaji wakubwa ya dawa za kulevya ikiwemo kuchepusha kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya.
Arusha. Kundi la Vijana wasomi hasa wa vyuo vikuu limetajwa kuongoza katika matumizi makubwa ya dawa za kulevya nchini.
Hayo yamesemwa jijini Arusha leo Oktoba 16, 2023 na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kukevya (DCEA), Aretas Lyimo katika hafla utiaji saini hati ya ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi katika kudhibiti uchepushwaji wa kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya.
“Tumefanya utafiti mdogo na tumegundua vijana wasomi tunaowategemea kuja kushika nyadhifa mbalimbali ndio wanaongoza kwa matumizi ya dawa za kulevya tena wengine wanasoma vyuo vikuu vya hapa nchini na wengine nje ya nchi,” amesema.
Amesema kwa utafiti mdogo walioufanya 2023, katika mikoa ya Mbeya, Arusha, Mwanza na Geita kwa waraibu 125, wamebaini zaidi ya asilimia 50 ni vijana wasomi ndio watumiaji wakubwa ya dawa za kulevya ikiwemo kuchepusha kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya.
Hali hii inaleta hofu ya hatari kubwa ya nchi yetu kuja kukosa wasomi kwani wengi wao ni wale wenye akili na wanafanya vizuri shuleni lakini matokeo yake wakishakuwa waraibu wanafikia hadi hatua ya kuacha shule na kuharibika afya ya akili.
“Kila mmoja avae dhamana ya kuhakikisha ulinzi na usalama wa taifa letu unalindwa na kwamba tushirikiane kwa pamoja kuhakikisha kuwa tunalinda kizazi hiki dhidi ya matumizi ya dawa ya kulevya kwani bila hivyo tutakuja kuwa na nchi yenye wazee tu kutokana na hawazaliani lakini zaidi wageni watashika nyadhifa mbalimbali serikalini na ofisi za kitaaluma,” amesema.
Amesema katika kukabiliana na changamoto ya uchepushaji wa kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na Baraza la FamasiaTanzania, wamemeendelea kushirikisha sekta binafsi ili Kuimarisha na kuzuia uchepushwaji wa kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya.
"Katika kutekeleza mkakati huu hadi sasa tumeimgia makubaliano kwa kusaini hati ya ushirikiano (MoU) na kampuni za kemikali zaidi ya 50 na jumuiya mbili zinazojihusisha na dawa za binadamu zenye zaidi ya wanachama 300,"amesema.
Amesema moja ya mafanikio ni mwaka 2017 hadi 2023 wamefanikiwa kuvunja mtandao wa usafirishaji haramu wa dawa za ketamine zenye uzito wa kilo 405 kutoka nchi za Ulaya kuja nchini Tanzania kwa kutumia vibali vya kughushi.
“Pia ukamataji wa dawa za pethidine chips (ampoules) 7,026, fentany (ampoules) chupa 4,260 na Morphine chupa 250 zilizoingizwa nchini kutokea nchi jirani kupitia mipakani, huku kemikali bashirifu zaidi ya tani 601 na zaidi ya lita 85 zilizuiwa kuingia nchini kutokana na ukiukwaji wa sheria za udhibiti,” amesema.
Mwakilishi wa TMDA Kanda ya Kaskazini, Proches Patrick aliwataka wauzaji wa kemikali hizo kuwa makini pale wanapouza dawa tiba kwa wateja sambamba na kuzihifadhi vyema hospitalini, lakini pia kuwa na tabia ya kuwahoji wateja wao kila mara wanapokuja kununua dawa hata kama ana cheti cha daktari.
"Lazima mjue mnahifadhi wapi hizi dawa na pia mnaouza dawa hizi lazima mjue mnamuuzia nani au kama mtu wa duka la dawa lazima ujue mgonjwa huyo kwa udhibitisho wa cheti cha daktari lakini pia muwe mnawatilia shaka wanapokuja mara kwa mara kwa dawa aina moja," amesema.