Othman: Tofauti za kisiasa hazitaikomboa Zanzibar

Muktasari:

Othman ameteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kufuatia kifo cha Maalim Seif Sharif Hamad.

Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud amesema kubeba itikadi za vyama vya siasa haitaisaidia Zanzibar kusonga mbele kiuchumi na badala yake wazike tofauti hizo ili kuleta mabadiliko.

“Rangi za vyama vyetu wala itikadi za vyama vyetu vya siasa kwa sasa sio suluhisho la ukombozi wa Zanzibar badala yake tuwe na mapenzi ili tunajenga nchi yetu,” amesema Othman.

Ametoa kauli hiyo leo Machi 6, 2021 kwenye Msikiti wa Arafa ulipo Mombasa Wilaya ya Magaharibi B Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, ambapo amewataka wananchi kuwa wamoja na kuleta maendeleo yatakayomnufaisha kila mmoja bila kujali itikadi za vyama.

Othman amesisitiza umoja na mshikamano ndio njia kuu ya kuisadia Zanzibar kutoka mahali ilipo sasa na kufikia malengo yake.

Amesema kwa kufanya hivyo itakuwa ni dua kubwa ya kumuenzi mtangulizi wake Hayati Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye alijitoa kusimamia hilo kwa nguvu zote.

Othman, ambaye amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati wa utawala wa Dk Ali Mohamed Shein, pia amefika nyumbani kwa Hayati Maalim kutoa mkono wa pole kwa wana familia wakiongozwa na Mama Awena, mke wa Maalim Seif.