Prime
Padri Soka alivyoruka viunzi kesi za ubakaji
Muktasari:
Padri Sosthenes Soka (42) amefanikiwa kupangua kesi ya tatu miongoni mwa kesi za ubakaji wa watoto wa mafundisho ya Kipaimara alizokuwa zinamkabili.
Moshi. Padri Sosthenes Soka (42) amefanikiwa kupangua kesi ya tatu miongoni mwa kesi za ubakaji wa watoto wa mafundisho ya Kipaimara alizokuwa zinamkabili.
Padri Soka, aliyekuwa akitoa huduma katika parokia teule ya Mtakatifu Dionis Aropagita ya Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi, Septemba mwaka jana alifunguliwa kesi tatu tofauti za kubaka watoto watatu zilizosomwa kwa mahakimu tofauti.
Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Moshi, Erasto Philly alisema padri huyo ameachiwa huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha tuhuma hizo kwa viwango ambavyo sheria inataka.
Katika kesi hiyo namba 349/2022, ilidaiwa tarehe isiyofahamika ya Agosti mwaka 2021, katika eneo la kanisa alilokuwa akihudumu alimbaka mtoto mwenye umri wa miaka 13.
Hakimu Philly alisema ametoa hukumu hiyo kwa kuwa kulikuwa na tofauti kubwa kati ya shahidi na hati ya mashtaka.
Mbali na kutofautiana kwa maelezo yaliyotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka, ilielezwa sababu nyingine za kuachiwa huru kwa Padri Soka ni kama kesi hiyo upelelezi wake haukufanywa, kwani kulitofautiana kati ya hati ya mashtaka iliyoeleza mtoto alifanyiwa tukio hilo siku moja, huku maelezo ya mtoto yakionyesha alifanyiwa tukio hilo zaidi ya mara moja.
Katika kesi ya kwanza iliyotolewa hukumu Septemba 22 mwaka huu na Hakimu Mkazi, Jenipha Edward alimwachia huru Padri Soka katika kesi namba 44/2022 ya ubakaji na ulawiti baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha tuhuma hizo. Katika kesi hiyo alidaiwa kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 12.
Septemba 25, mwaka huu ilitolewa hukumu katika kesi ya pili namba 45/2022, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Herieth Mhenga alimwachia huru padri huyo baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha shtaka la kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 12 katika kanisa hilo.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mhenga alisema upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha tuhuma hizo na kwamba kulikuwa na mashaka mengi katika ushahidi.
Alisema upande wa mashtaka ulishindwa kutoa majibu na kutofautiana kwa maelezo ya mashahidi, hivyo kusababisha ushahidi wao kutotiliwa maanani na mahakama.
Ilivyokuwa mahakamani
Baada ya padri huyo kuachiwa huru alionekana mwenye uso wa furaha alipotoka katika chumba cha mahakama, kisha kwenda hadi walipokuwa ndugu zake na kukumbatiana kwa furaha.
Padri huyo aliyekuwa akificha uso kwa kutumia kofia ya sweta lake kila alipofikishwa mahakamani, jana ilikuwa ni tofauti, kwani alionekana akitoka bila kujificha, huku akijadiliana mambo na wakili wake na kwenda mpaka walipokuwa wamekaa ndugu zake.
Kwa mara ya kwanza padri huyo akiwa ndani ya viunga vya mahakama alionekana kujiachia na kuzungumza na watu mbalimbali bila woga, tofauti na siku nyingine alipokuwa akitoka kwenye chumba cha mahakama, kwani alikuwa alienda moja kwa moja kwenye gari akihofia kupigwa picha na waandishi wa habari waliokuwa wakifuatilia kesi hiyo.
Akizungumzia hukumu hiyo, wakili wa utetezi, Edwin Silayo alisema kuwa baada ya mahakama kufuatilia mwenendo wa kesi pamoja na kusikiliza mashahidi wa pande zote, upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha tuhuma zilizokuwa zikimkabili padri huyo.
Alieleza baada ya upande wa mahakama kupitia maelezo ya pande zote mbili kulikuwa na mashaka mengi upande wa mashtaka, hivyo mahakama ikathibitisha kuwa Padri Soka hakuwa na hatia katika kesi hiyo.
"Leo (jana) ilikuwa ni hukumu kati ya kesi tatu zilizokuwa zikimkabili, mahakama baada ya kufuatilia mwenendo wa kesi na yote yaliyojiri na kusikiliza mashahidi wa pande zote wamekuta hana hatia kwa kuwa upande wa mashtaka wameshindwa kuthibitisha tuhuma hizo.
“Kulikuwa na mashaka mengi ambayo yaliibuka na ushahidi ulikuwa wa kutosha kwa pande zote, lakini baada ya kuangalia pande zote (upande wa mashitaka na wa utetezi) mahakama ikathibitisha Padri Soka hana hatia hata kidogo katika shauri hili,” alisema na kuongeza;
“Leo tunashangilia na tuna furaha kubwa kwa kuwa mahakama imethibitisha katika kesi zote kwamba Padri Soka hakuhusika kwa namna yoyote katika tuhuma zilizokuwa zikimkabili,” alieleza wakili huyo. Alieleza kuwa katika hukumu iliyotolewa jana, Mahakama imetenda haki kwa kuwa ushahidi alioutoa mtoto huyo ulikuwa ni wa kugongana na ilikuwa ni kama maelezo yoyote ambayo mtu angeweza kuelezwa na kuyasema.
“Ukiachilia mtoto kusema mambo tofauti ambayo hayakuwa na uhusiano unaothibitisha tukio hilo katika kesi hii, hata daktari aliyemfanyia vipimo mtoto huyo hakufika mahakamani kuthibitisha hayo zaidi fomu ya PF3 iliyotolewa na askari mpelelezi ambaye hakuizungumzia na kufafanua chochote kilichokuwepo ndani yake.
“Mahakama imesisitiza mashahidi waliotoa ushahidi ambao walikuwa ni viongozi wa kanisa namba 3 na 4 waliacha majukumu ya kuwasaidia watu kiroho na badala yake wakajiingiza katika kile walichokiita upelelezi na badala yake mpelelezi kufanya kazi yake ni kama ilifanywa na watu wengine, hivyo kufanya ushahidi wao kutofautiana kwa kiwango kikubwa na kuonekana kuwa na mashaka,” alieleza.
Kesi hiyo ilikuwa na vielelezo vitatu, mashahidi watano kutoka wa upande wa mashtaka huku upande wa utetezi ukiwa na mashahidi wanne, akiwemo mshtakiwa.