Panya waliza wakulima Handeni, washambulia ekari 23,000 za mahindi

Muktasari:

  • Ofisa kilimo wa halmashauri ya wilaya Handeni, Yibarila Chiza amesema jumla ya ekari 23,000 zimeharibiwa na panya hao na tayari Wizara ya Kilimo imepeleka dawa kwa ajili ya kugawa kwa wakulima wote ambao wameathirika na panya hao.

Handeni. Baadhi ya wakulima wa mahindi wa tarafa ya Magamba wilaya ya Handeni mkoa wa Tanga wameiomba Serikali kuwasaidia dawa ya kuthibiti panya waliovamia mashamba yao na kuharibu mazao, hali inayoweza kusababisha uwepo wa njaa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakulima hao wamesema kuna uvamizi wa panya kwenye mahindi yao ambao wanakata yale yalioanza kukomaa na kufukua mbegu ambazo zimeshapandwa.

Mkulima Habiba Waziri, amesema katika shamba lake, panya wamefukua mbegu za mahindi zilizopandwa, pia jamii ya maboga aina ya mamung'unya yote yameshambuliwa na panya hao waharibifu.

Mkulima mwingine, Bakari Kipimo anaeleza kwenye shamba lake alipanda mahindi, lakini yamefukuliwa na kwa sasa anajaribu kupanda maharage, bado ana mashaka yanaweza kuathiriwa na panya hao.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Ofisa tarafa ya Magamba, Boniface Deusdetit amekiri kuwepo uharibifu wa panya hao kwenye kata nne za eneo hilo ambazo ni Kwachaga, Kwalugulu, Kangata na Kwankonje, tayari wameshatoa taarifa ngazi ya wilaya kwa ajili ya hatua zaidi kwa wakulima hao kupatiwa msaada wa dawa na kunusuru mazao yao.

Mkuu wa wilaya ya Handeni, Albert Msando amesema ofisi yake imepokea taarifa hizo na zimeanza kufanyiwa kazi kwa ofisa kilimo wilaya kutafuta dawa haraka na wakulima wapewe ili kuthibiti panya hao.

Ofisa kilimo halmashauri ya wilaya Handeni, Yibarila Chiza amesema jumla ya ekari 23,000 zimeharibiwa na panya hao na tayari Wizara ya Kilimo imepeleka dawa kwa ajili ya kugawa kwa wakulima wote walioathirika na panya hao.