Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Peramiho wasimamisha shughuli kumuaga Jenista Mhagama

Muktasari:

  • Mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Peramiho (CCM), Jenista Mhagama unatarajiwa kuzikwa kesho Jumanne ya Desemba 16, 2025 katika Kijiji cha Ruanda, Mbinga mkoani Ruvuma.

Dar es Salaam. Vilio na huzuni vimetanda kila kona kwa wakazi wa Peramiho huku watu wengi wakijitokeza kutoa heshima ya mwisho kwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Jenista Mhagama.

Wananchi hao ambao wengi walitarajiwa kuwa mashambani na wengine kwenye shughuli mbalimbali kama biashara au maofisini, leo Desemba 15, 2025 wamefunga biashara zao na kujitokeza katika misa ya kumuombea Jenista iliyofanyika Kanisa la Mtakatifu Benedict, Parokia ya Peramiho Jimbo kuu la Songea.

Jenista ambaye amekuwa mbunge wa Peramiho kuanzia mwaka 2005, alifariki dunia Alhamisi, Desemba 11, 2025 jijini Dodoma, mwili wake unatarajiwa kuzikwa kesho Jumanne ya Desemba 16, 2025 katika Kijiji cha Ruanda, Mbinga mkoani Ruvuma.

Mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Jenista Mhagama, ukiwasili kanisani katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Benedict, Abasia ya Peramiho, Parokia ya Peramiho iliyopo Jimbo Kuu la Songea, Ruvuma, panapofanyika misa ya kuuaga leo Jumatatu Desemba 15, 2025.

Daines Komba mkazi wa Peramiho A, amesema wananchi wamejitokeza kwa wingi kutokana na kumpenda mbunge wao ndio maana wamefunga biashara zao na kuahirisha shughuli zao za kila siku kwa ajili ya kutoa heshima ya mwisho.

"Umati huu mkubwa ni heshima kwa malkia wa Peramiho, ametupatia heshima na maendeleo makubwa mno tunamuombea apumzike kwa amani," amesema Daines.

Bosco Ngonyani mkazi wa Parangu alisema hakuna mtu aliyejua kifo cha Jenista kingekuwa cha ghafla hivyo, ndio maana wameumia na kuja kutoa heshima zao.

"Kifo hiki kimetuumiza wengi, wananchi walitarajia kuwa awamu hii wangepata maendeleo makubwa zaidi kutokana na mchango mkubwa aliokuwa nao kwa watu wake na alipenda jimbo hili,” amesema Ngonyani.

Naibu Askofu Jimbo Kuu Katoliki la Songea aliyeongoza misa hiyo, Erick Mapunda amesema wengi hawapo tayari kukipokea kifo au kupokea vifo vya wapendwa wao, akisema hali hiyo inachangia wengi wao kuzusha taharuki na kutokubali kuwa ni vifo vya kawaida.

 “Kwa nini hatupo tayari, mimi nadhani wengi wetu tumejisahau tumeukumbatia sana ulimwengu tukidhani maisha yetu ni hapahapa duniani, tunaendelea kula anasa na mengineyo.”

Amesema wengi wanabaki kuishi maisha ya kila siku waliyoyazoea, akitaja sababu nyingine ya kutokukipokea kifo ni wengi kutojiandaa kiroho.

Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Jenista Mhagama, likiwa katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Benedict, Abasia ya Peramiho, Parokia ya Peramiho iliyopo Jimbo Kuu la Songea, Ruvuma, panapofanyika misa ya kuuaga leo Jumatatu Desemba 15, 2025.

“Tunaogopa tukifa huko mbele itakuwaje, hatujajitayarisha kwa uhakika, Jenista hakuogopa kifo, hakuukumbatia ulimwengu ndiyo maana maisha yake daima alikuwa mcha Mungu ndiyo maana alikuwa anasali sana hakukubali siku ipite bila kuomba,” amesema.

Mapunda ametaja jambo la pili ni kupokea vifo vya wenzetu, akisema siku ya kifo ikifika lazima upokee lakini kupokea vifo vya wenzetu mara nyingi huleta shida.

Ametaja mifano kuwa vifo vya wenzetu akifa mmoja maneno yanakuwa mengi sana, vurugu zinakuwa nyingi, magomvi na kutokuelewana miongoni mwa familia.

Mapunda amewataka Watanzania kuwa na utaratibu wa kumtanguliza Mungu katika mipango yao, ili waendelee kuishi wakimtumaini Mungu.

“Mungu ametufanyia mengi sana katika familia zetu, jamii, kanisa na Serikali kupitia mtumishi wake huyu Jenista Mhagama, amewatumikia wananchi kwa miaka mingi,” amesema Mapunda.

Akitoa salamu za rambirambi, Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba amemwelezea Jenista kuwa alikuwa mpatanishi na kiungo muhimu na mtu aliyeamini ukimtanguliza Mungu na ukafanya bidii inawezekana.

“Nimefanya naye kazi akiwa mnadhimu wa shughuli za Serikali bungeni, amekuwa akibeba jukumu linaloangukia kila wizara kama lake aliamini katika mafanikio, hiyo ndiyo ilimpa sifa ya kuitwa kiraka kwamba nafasi yoyote ya wizara aliyopewa aliimudu kama sekta yake ya ubobevu, alifanya hivyo alipokuwa Waziri wa Utumishi wa Umma na hata alipokwenda kwenye sekta ya kitaalamu kama Waziri wa Afya,” amesema.

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, Spika wa Bunge, Mussa Zungu na na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi wakishiriki misa ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama, leo Desemba 15,2025 katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Benedict, Abasia ya Peramiho, Parokia ya Peramiho, Jimbo Kuu la Songea, Ruvuma.

Mwigulu ameelezea namna alivyoshirikiana naye kwenye masuala ya uongozi na familia akisema alikuwa moja ya marafiki wa familia na kwamba walikuwa na majadiliano mengi na vikao vingi kama marafiki.

“Niwaambie watoto hamtakuwa peke yenu, hamtakuwa yatima tutaendelea kushirikiana. Tutasimamia kila kitu wajomba zenu tupo tutashirikiana nanyi ili zile ambazo zilikuwa ndoto za Jenista zisiishie hapa sababu yeye ametangulia mbele za haki,” amesema.

Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Azzan Zungu amesema Jenista alikuwa mtu mwema na alimzoea sana.

Amewahi kumuuliza jina la Zungu limetoka wapi akamjibu kuwa bibi yake mzaa baba ni Mngoni na mtu wa Nyasa na ni Mzulu na hilo ni jina la Kizulu.

Zungu ametoa shukurani zake kwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, mawaziri, wabunge na viongozi wengine wakiwamo viongozi wa dini huku akitoa agizo.

“Niwashukuru viongozi wa dini, tumekuwa pamoja mpaka kesho tunakwenda kumpumzisha Jenista. Mkuu wa Mkoa uko hapa, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi uko hapa na nyota ya mtoto wetu yuko hapa, nafikiri nimeeleweka, nyota ya mtoto wetu yupo hapa, familia mshikamane, mpendane hiki ni kipindi kigumu kwenu lakini mkishikamana mtavuka salama,” amesema Zungu.

Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda, ameeleza namna Jenista alivyompambania hadi kuibuka kinara wa kushika wadhifa huo.

“Hata yeye mwenyewe kwangu mimi alinisaidia sana na aliniambia Chatanda, tukazane tukishindwa nitauweka wapi uso wangu, watu wameshajua nakusaidia wewe, alifanya kila linalowezekana kuhakikisha nashinda,” amesema Chatanda.