Pinda alia na rushwa kwenye uchaguzi

Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda wakati akifanya mahojiano na Mwananchi. Picha na Idd Hassan.
Muktasari:
- Amesema katika kipindi hiki kuelekea kwenye uchaguzi, kumekuwa na tabia ya watu wanaotaka nafasi kwenye ngazi mbalimbali kutumia fedha kuwashawishi wananchi ili kupata nafasi.
Katavi. Wakati Taifa likielekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa 2025, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda amekemea wanasiasa wanaotumia fedha ili kuwashawishi wananchi wawachague.
Amesema jambo hilo linasababisha kupatikana kwa viongozi wasiosimamia maslahi ya wananchi.
Pinda ameyabainisha hayo jana Julai 19, 2024 alipofanya mahojiano maalumu na Mwananchi kijijini kwake Kibaoni, katika Halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi, zikiwa zimepita siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya ziara yake mkoani humo.
Pinda amesema katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi, kuna baadhi ya watu wanaotaka nafasi kwenye ngazi mbalimbali hutumia fedha kuwashawishi wananchi kwa kuwapatia rushwa.
Amesema jambo hilo halipaswa kuachwa litamalaki, bali likemewe kwa nguvu zote kwa kuwa halistahili katika kupata kiongozi bora.
"Serikali imeweka utaratibu na bahati nzuri Serikali iliyopo madarakani inaongozwa na chama tawala na inasimamiwa na ilani ya uchaguzi, pia, kuna Katiba na kanuni na vitu vingine, vinaelekeza vizuri vitu vya kufanya na ambavyo si vya kufanya kwenye uchaguzi," amesema Pinda.
Kiongozi huyo mstaafu amesema kuwepo kwa utaratibu huo, kumefanya wananchi wengi kuwa na matarajio ya kupata viongozi bora na sio bora viongozi.
Amesisitiza nyakati kama hizi ni muhimu kuangalia hali ikoje na kufanya maboresho yatakayosaidia kuepuka hali hiyo.
"Vikwazo vipo kwenye matumizi ya fedha (rushwa) kwenye uchaguzi, ukiangalia kuna watu kwenye macho ya wengi hawastahili kuwa na cheo chochote serikalini, lakini ana vifedha ikifika kwenye uchaguzi, anaomba nafasi na siku ya kuamkia uchaguzi, yeye halali usiku, anaandaa watu wake ambao wanatembea nyumba kwa nyumba kuzungumza na wananchi na kuwaachia kitu kidogo (bahasha) ili kuwashawishi wamchangue.
"Hii inahitaji very strong mind (msimamo mkubwa wa akili) kwa wananchi kusema 'pamoja na kahela ulikonipa sikuchagui, namchagua mtu ninayemtaka mimi'. Binafsi natamani kuwa na watu wengi wa namna hiyo, kwamba kula hela yake na anamchagua mtu anayefaa kuwa kiongozi na sio bora kiongozi," amesema Pinda.
Mwanasiasa huyo mkongwe anasema kwa sasa anaona kila chama kinahangaika kupata aina bora ya watu watakaowasimamisha kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi.
"Katika kupata viongozi bora lazima uangalie na upande wa pili wao wamejipangaje ili kujiandaa na kutafuta mgombea ambaye sifa zake zitawazidi wapinzani na wananchi kukubali kumchagua, sisi kama CCM tunaenda vizuri sana na mtu yeyote atakayeomba nafasi kwa kutumia fedha (rushwa), tutamkata jina lake na hatutaangalia sura ya mtu wala wadhifa wake. Tutachukua watu wazuri kuingia kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi katika nafasi za ngazi zote.
"Ndio maana elimu tunayotoa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani, tunahimiza wananchi watuletee kiongozi anayefaa, mtu anayetambua dhamana yake ya kuwa kiongozi anayekubalika katika eneo husika, mcha Mungu na si vinginevyo,” amesema Pinda.
Amewataka viongozi walio madarakani kuanzia mwenyekiti wa mtaa, diwani na mbunge, watambue kuwa nafasi walizonazo ni dhamana tu na mabosi wao ni wananchi.
“Bahati mbaya sana wengi wao wakichaguliwa wanapandisha mabega na kuwaona wananchi sio chochote, jambo linalowapa wakati mgumu wa kutetea nafasi zao inapofika kipindi kama hiki,” amesema Pinda.
Agusia imani za kishirikina
Waziri Mkuu huyo mstaafu, amewataka wananchi kuachana na imani za kishirikina zinazosababisha baadhi ya watu kupoteza maisha yao kwa kuamini kupata kiungo cha mtu kinamfanya ashinde kwenye uchaguzi au mafanikio mengine.
"Jambo hili ni baya sana, kuamini kukata kiungo cha binadamu mwenzako ili kupata madaraka na hili watakuja kuulizwa mbele za Mungu, hata vitabu vya dini zote vinakataza kutoa uhai wa mtu.
"Niwaombe Watanzania kuachana na imani hizi za kishirikina ambazo zinafanya baadhi ya ndugu zetu wenye ualbino kupoteza maisha yao, jambo hili ni baya sana hata vitabu vya dini na madhehebu yote vinakataza kutoa uhai wa mtu ni kitu kibaya sana mbele za Mungu," amesema Pinda.
Watoto na maadili
Pinda anayefahamika pia kama ‘Mtoto wa Mkulima’, amezungumzia suala la mmomonyoko wa maadili, amesema ubize uliopo kwa wazazi kwenye kutafuta maisha kumefanya malezi ya watoto kulegalega.
Amesema sambamba na ukuaji wa teknolojia, watoto hujikuta wakijifunza mambo mengi yasiyo na maadili kupitia kwenye mitandao.
"Ninachotaka kusema kwenye hili, tunahitaji tufanye malezi ya pamoja kwa maana wazazi wajitahidi kulea watoto kwenye misingi ya maadili na shuleni nako walimu wasimamie vyema maadili na viongozi wa dini wapatiwe nafasi ya kufundisha misingi ya dini shuleni. Hii itasaidia kumjenga mtoto kukua kwenye maadili," amesema Pinda.
Ziara ya Samia Katavi
Pinda amezungumzia pia ziara ya Rais Samia aliyoifanya hivi karibuni mkoani alikozindua na kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Amesema asilimia kubwa ya wakazi wa Mkoa wa Katavi wanajishughulisha na kilimo, ufugaji, utalii, uchimbaji wa madini na uvuvi.
Akiwa Katavi, Rais Samia alizindua vihenge na maghala ya kuhifadhia mazao huku akiutangaza Mkoa wa Katavi kuwa kanda maalumu ya kununua na kuhifadhi mazao.
Kutokana na hilo, Pinda amesema; "Asilimia 70 mpa 80 ya wakazi wa Katavi ni wakulima, ziara ya Rais Samia imefungua milango ya kufanya biashara ya mazao sisi wakulima wa hapa Katavi lakini sio hivyo tu, hata tukiangalia Serikali imewekeza nguvu kubwa kwenye kilimo.
"Zamani bajeti ya kilimo ilikuwa Sh2 bilioni lakini sasa ni zaidi ya Sh1 trilioni, huo ni uwekezaji mkubwa sana uliofanywa na Serikali ambapo imeongeza maofisa ugani karibu kila kijiji na kata, hii inaleta picha ya kwamba kilimo kimekuwa sana hapa nchini," amesema.
Pinda ameeleza kwamba wamefika hapo kutokana na elimu ya matumizi ya mbegu bora pamoja na mbolea na kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa wakulima kutumia mbolea za ruzuku, jambo lililofanya mkoa huo kuzalisha tani zaidi ya milioni moja kwa mwaka. Amesema hayo ni mafanikio makubwa sana katika sekta ya kilimo.
Licha cha kuongezeka kwa uzalishaji huo, anashangazwa na mkoa wa Katavi kuwa na udumavu wa watoto ambapo takribani asilimia 32.2 ya watoto wanaozaliwa wana udumavu lakini pia hata watu wazima wana udumavu, amesema hiyo inatokana na mila na desturi walizonazo, watu hawazingatii milo sahihi.
Amesema elimu inatakiwa kutolewa kwa wananchi ili kutumia mazao wanayolima kuondokana na udumavu.