Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pinda apiga marufuku kesi za ardhi kupelekwa kwa wakuu wa wilaya, mikoa

Wahitimu wa chuo cha ardhi Morogoro wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi Godfrey Pinda aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 41 ya chuo hicho. Picha Hamida Shariff.

Morogoro. Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Godfrey Pinda amesema kuanzia sasa atakapogundua wananchi wanapeleka kesi za ardhi kwa wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa, afisa ardhi wa eneo husika atakuwa hatoshi na hivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

Pinda ameyasema hayo leo kwenye mahafali ya 41 ya chuo cha ardhi Morogoro ambapo amesema kuwa wakuu wa mikoa na wilaya sio wataalamu wa ardhi hivyo aliwataka maofisa ardhi kuhakikisha wanamaliza migogoro na changamoto za ardhi ndani ya Ofisi za ardhi na sio kwa viongozi.

"Inakuwaje wananchi wanakosa imani na maafisa ardhi mpaka wanaamua kwenda kupeleka changamoto zao kwa wakuu wa wilaya ama wakuu wa mikoa," amehoji Pinda.

Naibu Waziri huyo ameshauri somo la maadili lifundishwe kwenye vyuo vya ardhi kwa kuwa wapo baadhi ya maafisa ardhi wanapokwenda kufanyakazi wanatoka kwenye ujuzi wao na kufanya mambo mengine ambayo yamekuwa ni chanzo cha migogoro ya ardhi.

Aidha amesema kuwa kwa sasa wizara inaendelea na kazi ya upimaji na urasimishaji wa maeneo mbalimbali hapa nchini lakini yapo baadhi ya makampuni ya upimaji yamegeuza zoezi hilo kama mtaji na hivyo kusababisha malalamiko na migogoro.

"Tumewapa kazi ya kupima na kurasimisha lakini kinachotokea wanapofika kwenye eneo la kupima wanafanya mambo ya dhuruma, wanapima eneo wakikuta eneo Lina zaidi ya mita za mraba 800 basi hizo zilizozidi wanachukua na kumuuzia mtu mwingine, hii ni dhuruma na pia uhalifu kama uhalifu mwingine," amesema Pinda.

Hivyo amesema wizara inaangalia namna ambavyo Kazi hiyo wanaweza kupewa wahitimu wa vyuo vya ardhi na pia amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Taifa (NHC) kuhakikisha miradi yote inayohitaji nguvu kazi wahitimu wa vyuo vya ardhi wapewe umuhimu na kipaumbele.

Katika hatua nyingine Pinda amesema kwa sasa ipo haja kwa chuo hicho kuanzisha kozi nyingine itakayoendana na ulimwengu wa teknolojia ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa somo la Tehama ambalo litasaidia wataalamu wa ardhi kutunza kumbukumbu na data.

"Hatutaki wananchi wapate usumbufu wa kwenda ofisi za ardhi kulipa ada za ardhi wananchi watalipa ada zao kidigitali na hii itasaidia kupunguza migogoro ya ardhi inayotokea baada ya kiwanja kimoja kumilikiwa na watu zaidi ya mmoja," amesema Pinda.

Awali akisoma taarifa ya chuo Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro, Charles Saguda amesema kuwa udahili wa wanafunzi umeongezeka mara 11 kutoka wanafunzi 60 mwaka 78 hadi kufikia mwaka 2022/ 2023 ambapo wamedahili 660.

Saguda amesema kuwa chuo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya uhaba wa wafanyakazi hata hivyo yapo mafanikio mengi yaliyopatikana ikiwemo ujenzi wa madarasa matatu unaoendelea ambayo yatasaidia kuongeza udahili na kufikia wanafunzi 1,290.

Katika risala ya wanafunzi iliyosomwa na Chacha Marwa wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi kuboresha mazingira ya chuo hicho ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kisasa vinavyoendana na teknolojia ya sasa.