Polio bado janga Pakistan

Muktasari:
- Licha ya juhudi za kutoa dozi milioni 300 za chanjo kila mwaka na matumizi ya Dola za Marekani bilioni 9.3 kati ya 2013-2023, polio bado inashika kasi, hasa Kusini mwa Khyber Pakhtunkhwa.
Pakistan. Watu 14 wameripotiwa kuugua ugonjwa wa polio nchini Pakistan ikielezwa kuwa Taifa hilo pamoja na Afghanistan ndio nchi mbili duniani zinazopambana zaidi kudhibiti ugonjwa huo.
Agosti 10, mwaka huu shirika la habari la Al-Jazeera lilitoa ripoti ikionesha wagonjwa 14 wapya wa polio katika eneo la Qilla Saifullah wilayani Balochistan huku ripoti ya wizara ya afya nchini humo ikieleza kuwa tangu 2015 wameripotiwa wagonjwa 362.
Licha ya kuripotiwa kwa ugonjwa huo, kila mwaka hutolewa dozi milioni 300 za chanjo huku Dola za Marekani bilioni 9.3 zikiwa zimetumika kununua chanjo kati ya mwaka 2013 hadi 2023.
Ugonjwa huo husababisha kupooza miguu na mikono na huambukiza ikiwa mtu atakunywa maji au kula chakula ambacho kimebakizwa na mwenye maambukizi au kugusana naye.
Dk Hamid Jafari, mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amenukuriwa na Al-Jazeera akisema ugonjwa huo upo zaidi Kusini mwa jimbo la Khyber Pakhtunkhwa nchini Pakistan.
"Hapa ndipo kuna vita kubwa kwa sababu si sehemu salama na kuna ukosefu wa huduma nyingi za msingi. Zaidi ya wilaya 50 Pakistan kumegundulika virusi vya polio.’’
‘’Mpango wa kupambana na polio upo lakini pia kuna hatari ya maambukizi kwa timu ambayo inawasaidia wanaougua kwa kuwa wapo waliofariki dunia baada ya kuugua polio wakiwa wanawahudumia wagonjwa,’’ amesema Jafari.