Mtoto agundulika na Polio Sumbawanga, milioni 3 kuchanjwa

Muktasari:

  • Kufuatia uwepo wa mtoto aliyeonyesha dalili za kupooza Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi na wadau inatarajia kuendesha kampeni ya kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio kwa watoto zaidi ya milioni 3,250,598 walio na umri wa chini ya miaka nane.

Dar es Salaam. Baada ya uchunguzi wa maabara kuthibitisha kuwa mtoto aliyekuwa amepooza Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa ana maambukizi ya virusi cha polio, Serikali imeazimia kuchanja watoto walio chini ya miaka nane kwenye mikoa ya Rukwa, Kagera, Kigoma, Katavi, Songwe na Mbeya.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa, Septemba 9, 2023 jijini Dodoma na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kampeni ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio ambayo inatarajiwa kuanza kufanyika nchini kuanzia Septemba 21 hadi 24 mwaka huu.

Amesema kuwa Tanzania inaendesha kampeni hiyo ya chanjo kutokana na wizara kupokea taarifa Mei 26, 2023 za uwepo wa mtoto mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi kumi na moja ambaye alionyesha dalili za kupooza kwa ghafla.

Mtoto huyo ambaye alitolewa taarifa kutoka Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa. Uchunguzi wa maabara ulithibitisha kuwa mtoto huyu ana maambukizi ya virusi cha Polio.

Ummy amesema pia kampeni hiyo inafuatia athari zilizoletwa na janga la Uviko19 ambalo limeleta athari kadhaa kwa afua zingine za afya ikiwemo kuathiri mwitikio wa chanjo mbalimbali nchini.

"Mathalani, kwa mwaka 2020 hadi mwaka 2022, jumla ya watoto 1,988,022 hawakupata chanjo yoyote. Vilevile, kwa kipindi hicho (2020 - 2022), jumla ya watoto 1,595,564 hawakukamilisha ratiba za chanjo mbalimbali za watoto.

"Hali hii imepelekea kuanza kujitokeza kwa visa na milipuko ya magonjwa

yanayozuilika kwa chanjo ambayo yalikuwa yamedhibitiwa ikiwemo ugonjwa wa surua, rubella na polio," amesema Waziri Ummy.

 Waziri Ummy amesema kuwa maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Polio yametolewa taarifa pia katika nchi zinazopakana na Tanzania mfano Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Zambia hivyo hali hii inaongeza tishio na hatari ya maambukizi ya Virusi vya ugonjwa wa Polio kwa nchi yetu hususani katika Mikoa inayopakana moja kwa moja na nchi hizo.

 “Napenda nichukue fursa hii kuwataarifu kuwa tutakuwa na kampeni maalum ya utoaji wa chanjo ya matone dhidi ya Polio (nOPV2) kwa watoto wote wenye umri chini ya miaka nane. Kampeni hii itafanyika kwa siku nne kuanzia tarehe 21 – 24 Septemba, 2023 katika mikoa sita inayopakana na nchi zenye mlipuko wa polio ambayo ni Rukwa, Kagera, Kigoma, Katavi, Songwe na Mbeya," amesema Waziri Ummy.

“Lengo la kampeni hii ni kuwafikia watoto 3,250,598 waliozaliwa baada ya mwaka 2016 ili kuwakinga dhidi ya Kirusi cha Polio aina ya pili (Polio Virus Type 2) kinachoweza kusababisha ulemavu wa kudumu.  Kwa Mkoa wa Rukwa tunatarajia kufikia watoto 391,883 Kagera 729,387 Kigoma 884,477 Mbeya 614,346 Katavi 227,862 na Songwe 402, 643," amefafanua Waziri Ummy.

Waziri huyo amesema ili kufanikisha kampeni hiyo, Wizara na washirika wake imeshafanya maandalizi kwa ajili ya kuwezesha zoezi bila kuathiri shughuli zingine za wananchi.

“Wakati wa kampeni kutakuwa na jumla ya timu yenye jumla ya watoa huduma za afya 5,291 kwa Mikoa yote sita itakayofikiwa na zoezi hili ambapo kila timu itakuwa na watoa huduma watatu.

“Timu hizi zitakuwa zinatoa huduma ya chanjo kwa walengwa kupitia vituo vya kutolea huduma za afya, nyumba kwa nyumba, shuleni na maeneo mbalimbali ya mikusanyiko ikiwemo Nyumba za Ibada," ameeleza Waziri Ummy na kutoa rai kwa wazazi na walezi kutoa ushirikiano kwa watoa huduma za afya ili kuwezesha watoto wao kuchanjwa kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba.

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu, amesema katika kuendeleza mikakati ya kutoa chanjo dhidi ya polio, imeundwa timu ya watu waliopata mafunzo ya kutoa chanjo hiyo katika Mikoa hiyo sita.

“Tumeunda timu nzuri ambayo imepata mafunzo ya kutoa chanjo ambayo ina watoa huduma 5,291 katika mikoa hiyo sita ili kuhakikisha watoto wote wanafikiwa katika kupatiwa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio,” amesema Profesa Nagu.

“Tunawapa hamasa wazazi wahakikishe kwamba, wanawatoa watoto wao kupata chanjo hii ili kuwaepusha watoto wetu kupata ulemavu ambao kwakweli unakingika kwa kutumia chanjo," ameongezea Profesa Nagu.