Polisi 14 matatani kwa dawa za kulevya

Muktasari:

  • Mahmoud alitoa taarifa hiyo jana alipozungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Sanaa uliopo Rahaleo mjini hapa. “Bado tunaendelea kuwasaka watu wengine na tumeongeza ulinzi katika maeneo mengi,” alisema Mahmoud.

Zanzibar. Siku chache baada ya Jeshi la Polisi Zanzibar kutoa orodha ya majina 42 ya watuhumiwa wa dawa za kulevya, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Ayoub Mohamed Mahmoud ametoa majina 14 ya askari wanaotuhumiwa kushirikiana na waingizaji na wauzaji wa dawa hizo.

Mahmoud alitoa taarifa hiyo jana alipozungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Sanaa uliopo Rahaleo mjini hapa. “Bado tunaendelea kuwasaka watu wengine na tumeongeza ulinzi katika maeneo mengi,” alisema Mahmoud.

Alisema watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa, wakati wowote watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zao.

Mkuu huyo wa mkoa alisema hawawezi kutaja majina ya askari hao hadi pale uchunguzi utakapokamilika.

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya dawa za kulevya, Rogers Sianga alisema atahakikisha hakuna mtu hata mmoja anayeingiza, kuuza au kutumia dawa za kulevya nchini.

“Mipango maalumu imeandaliwa ili kudhibiti hali hiyo na kuhakikisha kuwa maeneo yote yaliyokuwa yanatumiwa na kundi hilo la uingizaji na uagizaji wa dawa za kulevya yanadhibitiwa,” alisema.

Alisema kuna wajanja wanaovitumia visiwa vya Zanzibar kama kimbilio la kujificha.

Kamishna huyo alisema kuanzia sasa nguvu zaidi zitaelekezwa visiwani humo katika maeneo ya viwanja vya ndege na bandari ili kuhakikisha hakuna dawa itakayoingia.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali alisema wanafanya mchakato wa kuongeza mashine maalumu ya kufanyia uchunguzi katika maeneo ya viwanja vya ndege, bandarini na maeneo yanayopokea mizigo kutoka nje.