Polisi kujenga vituo vya ukaguzi wa magari nchini
Wananchi wanaoendelea kutembelea Banda la Jeshi la Polisi Tanzania wakioata maelekezi katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, wameendelea kupata elimu mbalimbali kuhusu huduma zinazotolewa na Jeshi la Polisi pamoja na masuala ya ulinzi na usalama.
Muktasari:
- Miradi mikubwa inayotarajiwa kuanza kutekelezwa ni ujenzi wa vituo vya kisasa vya ukaguzi wa magari vitakavyosaidia kuimarisha usalama barabarani na kuhakikisha magari yanayotumika yanakidhi viwango vya usalama.
Dar es Salaam. Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi Tanzania (TPF Corporation) lina mpango wa kujenga mtandao wa vituo vya kisasa vya ukaguzi wa magari nchi nzima katika jitihada za kuimarisha mfumo wa ukaguzi wa lazima wa vyombo vya moto.
Akizungumza jana Jumamosi, Julai 11, 2026, katika Maonyesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba, Ofisa Uhusiano wa shirika hilo Mratibu Msaidizi wa Polisi, Lule Mlay alisema hii ni mara ya kwanza kwa shirika hilo kushiriki katika maonesho hayo kwa lengo la kuonyesha miradi yake mbalimbali ya maendeleo.
Alifafanua miongoni mwa miradi mikubwa inayotarajiwa kuanza kutekelezwa ni ujenzi wa vituo vya kisasa vya ukaguzi wa magari vitakavyosaidia kuimarisha usalama barabarani na kuhakikisha magari yanayotumika yanakidhi viwango vya usalama.
Mbali na hilo, Mlay alisema shirika hilo linaandaa utekelezaji wa mradi wa Safe Cities, ambao utafanyika kwa ushirikiano na Serikali kwa kufunga kamera za kisasa za ulinzi katika miji mitatu ya Dar es Salaam, Dodoma na Arusha kwa lengo la kusaidia kudhibiti uhalifu.
Pia kwa kushirikiana na kikosi cha usalama barabarani wanaendelea na mpango wa kufunga kamera za usalama katika barabara kuu ili kubaini na kufuatilia madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani.
“Kama mwanzo, kamera hizo zitafungwa kuanzia Makutano ya John Kijazi jijini Dar es Salaam hadi Dodoma,” alisema.
Mlay alisema TPF Corporation pia linajihusisha na uzalishaji wa mavazi, likitengeneza sare za taasisi za Serikali na kampuni binafsi, ikiwemo kampuni za ulinzi.
“Kwa sasa tunafanya kazi na Polisi Wasaidizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jeshi la Magereza pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),” alisema.
Alisema shirika hilo linaendelea kutoa huduma za ulinzi kupitia kampuni yake ya ulinzi, huku kwa sasa likitoa huduma hizo katika Soko la Kariakoo, vituo vyote vya mabasi ya mwendokasi (DART) na katika Maonesho ya Sabasaba yanayoendelea.
Kwa upande wake, Koplo Issa Godwin alisema maonyesho hayo yamekuwa fursa ya kutangaza programu ya mafunzo kwa kampuni binafsi za ulinzi, inayojumuisha mafunzo ya kitaalamu ya matumizi ya silaha na mbinu za ulinzi.
Alisema shirika hilo pia linatoa huduma za bandarini, akibainisha kuwa takribani asilimia 60 ya wafanyakazi wa bandarini ni vibarua, hivyo huduma hizo ni muhimu katika kusaidia shughuli za uendeshaji wa bandari.
Mbali na hayo, Godwin alisema TPF Corporation linatoa huduma za usafirishaji wa fedha na vitu vya thamani na kuwataka Watanzania kutumia huduma mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo.
“Lengo letu ni kuendelea kutoa huduma za kisasa, salama na zenye kuaminika kwa taasisi za umma, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla,” alisema.