Polisi kusaka vijana watatu waliomlawiti mwanafunzi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa

Muktasari:

  • Mwanafunzi huyo alilawitiwa Februari 18, 2024 saa 12:30 jioni katika kata ya Mkolani jijini Mwanza mara baada ya mwanafunzi huyo kwenda kuazima daftari kwa rafiki yake, ndipo alipozingirwa na vijana watatu waliomtaka awapatie fedha.

Mwanza. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amemwagiza Ofisa Upelelezi Wilaya ya Nyamagana (OCCID) kuwatafuta vijana watatu wanaotuhumiwa kumlawiti mwanafunzi mwenye umri wa miaka 16 ambaye jina lake limehifadhiwa.

Mvulana huyo alilawitiwa Februari 18, 2024 saa 12:30 jioni katika kata ya Mkolani jijini Mwanza mara baada ya mwanafunzi huyo kwenda kuazima daftari kwa rafiki yake, ndipo alipozingirwa na vijana wanne waliomtaka awapatie fedha.

Baada ya tukio hilo, mama mzazi wa mvulana huyo aliibuka na madai kwamba alipotoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha Igogo aliambiwa awatafute waharifu na kuwakamata, jambo lililoibua maswali mengi kuhusu kauli hiyo na kulifanya jeshi hilo kukanusha taarifa hiyo.

Kutokana na sintofahamu hiyo, kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa alitembelea eneo hilo jana April 2, 2024 na kufanya mkutano na wananchi wa eneo hilo ambapo amesema vijana waliotekeleza tukio hilo wametokomea kusikojulikana.

Hata hivyo, Kamanda Mutafungwa amemuagiza Ofisi Upelelezi Wilaya (OCCID) ya Nyamagana kufanya oparesheni maalumu kwa kushirikiana na wananchi hao kuwapata watuhumiwa hao waliomlawiti mwanafunzi huyo.

“Vijana waliofanya lile tukio wameshajulikana na wazazi wao wamefahamika na baada ya hilo tukio wakapotea lakini jitihada za Jeshi la Polisi zinaendelea, leo tumewashirikisha wananchi kuhakikisha tunawatafuta na wazazi wao wameeleza kuwa ni kweli baada ya hilo tukio wamekimbia.

“Maagizo yangu ni kwamba Jeshi la Polisi lipo hapa na OCCID upo hapa, shirikiana na hawa wananchi hawa, vijana hao wakamatwe kwa kushirikiana na wananchi hawa na wakamatwe salama na kufikishwa kwa jeshi la polisi salama ili kuchukulia hatua za kisheria kwa mujibu wa sharia.

“Ole wenu muwadhuru OCCID, fanyeni hiyo operesheni, leta askari huku na wasitoke mpaka vijana hao wakamatwe,” amesema Kamanda Mutafungwa.

Kamanda Mutafungwa amesisitiza kwamba kila mtaa au kitongoji katika eneo hilo kuhakikisha wanaunda vikundi vya ulinzi shirikishi vitakavyosaidia kudhibitibi uhalifu.

“Tunataka vikundi vya ulinzi shirikishi katika ngazi ya mtaa kwa sababu jeshi la polisi hatuwezi kuwa na askari wa kwenda kila mtaa, ndio maana maeneo mengine tunafanya doria na kuhamasisha kuwepo kwa vikundi kama hivyo ili kuleta urahisi wa kuhakikisha usalama wa watu na mali zao katika mitaa na vitongoji,” amesema Kamanda Mutafungwa.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Buguku, Maduhu Sultan amesema mbali na hali ya usalama kuwa shwali japo kuwa wanakabiliwa na changamoto za udokozi, vibaka na madawa ya kulevya hasa kwa vijana wa eneo hilo.

“Hali ya usalama wa eneo langu ni shwari japo haikosi changamoto miongoni mwazo ni udokozi, vibaka ambao wameendelea kutusumbua na sisi tunaendelea kukabiliana nao kadri tunavyoweza. Sambamba na hilo, tunao vijana wanaoshughulika na masuala ya kuvuta bangi japo tumeendelea kupambana nao kuhakikisha tunakomesha,” amesema Sultan.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi katika mtaa huo wakizungumza katika mkutano huo wameliomba Jeshi la Polisi kuimarisha zaidi ulinzi katika eneo hilo.

“Vijana hao ambao wameingia hata kwenye tuhuma za ulawiti ni vijana wetu wa mtaani lakini wametafuta magenge makubwa kutoka sehemu zingine kuingiza hapa kwa sababu wameona hapa ni shamba la bibi la kuchezea, tungekuwa na umoja ingekuwa rahisi kukemea na kujua limetokea wapi,” amesema Selestini Batinagwa, mkazi wa Mtaa wa Buguku

Ameshauri kwamba wazazi hasa wanawake waache kukumbatia watoto wao pindi wanapoletewa taarifa zinawahusu watoto hao, wakiambiwa ameiba sio waanze kusema wamemuona wapi.

Akiunga mkono hoja hiyo, Agnes Kubozya, mkazi wa eneo hilo, ameliomba Jeshi la Polisi kuwasaidia kuimarisha ulinzi katika eneo hilo ili kukabiliana na matukio uhalifu yanayofanywa na kundi la vijana wachache wazawa wa eneo hilo.

“Polisi tunaomba mtusaidie, hawa vijana tunawapenda sana, hata tunavyowasema hapa sio kwamba hatuwapendi, ni watoto wetu tumewazaa na mimi nafurahi ninapoona mtoto wa jirani yangu akiwa na sifa nzuri. Mimi mwenyewe najivunia lakini akiwa na sifa mbaya naogopa hata kumtuma,” amesema Agnes.