Polisi Moro yakamata viroba 30 vya bangi
Morogoro. Mifuko 30 ya bangi yenye uzito wa kilo 430 imekamtwa na Jeshi la Polisi mkoani Morogoro baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema hayo leo Desemba 31,2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio.
Lori lenye tela lililokuwa likitokea mkoani Iringa kwenda jijini Dar es salaam likiwa na mifuko ya chakula cha kuku lilikamatwa Kijiji Cha Mangae, Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro liliposimama kupakia viroba vya bangi.
"Hili gari ni kampuni ya K.T. Abri na dereva aliyekuwa akiliendesha ametelekeza gari likiwa na mifuko ya chakula cha kuku kama mnavyoona na tunamtafuta, tunataka ajisalimishe," amesema.
Amesema dereva huyo na waendesha pikipiki sita wametoroka na kutelekeza pikipiki zao baada ya kushtukia mtego wa polisi katika Kijiji cha Mangae Kata ya Mangae, Wilaya ya Mvomero.
Wakati huo huo, Polisi katika kijiji cha Kimamba B', Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro limemkamata Ahmad Mlali (31) mkazi wa Kimamba B akiwa na miba 256 ya nungunungu pamoja na bunduki mbili aina ya Shotgun na Rifle zikiwa na maganda 71 ya risasi.
Kamanda Mkama amesema mtuhumiwa alikuwa akitumia bunduki hizo katika shughuli za uwindaji haramu kwenye hifadhi zilizopo jirani.
Amesema mtuhumiwa amekamatwa Desemba 31, 2023 asubuhi nyumbani kwake Kilosa.
Kamanda Mkama ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuliamini Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu, ili zifanyiwe kazi haraka.