Polisi wadaka wawili wakisambaza Smart Gin bandia

Gari ambalo limekamatwa na katoni 500 za pombe bandi zenye nembo ya Smart Gin, zikisambazwa mkoani Iringa. Picha na Mary Sanyiwa

Muktasari:

  • Zaidi ya katoni 500 za pombe bandia zikiwa na nembo ya Smart Gin zimekamatwa mkoani Iringa zikiwa tayari kupelekwa sokoni kwa watumiaji.

Iringa. Jeshi la Polisi mkoani Iringa limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili wakazi wa Kimara jijini Dar es Salaam wakiwa na katoni zaidi ya 500 za bidhaa bandia za kinywaji pombe kali zenye nembo ya Smart Gin, wakizisambaza katika Manispaa ya Iringa.

Akizungumza na vyombo vya habari jana Machi 27, 2024, Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amesema watuhumiwa hao walikuwa wakisambaza bidhaa hizo kwa kutumia gari lenye namba za usajili aina ya Toyota Dyna.

Kamanda Bukumbi amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Joseph Sawe (34) pamoja na Hassan Dinongo (34), wote wakiwa ni wakazi wa Kimara Dar es salaam.

“Katika uchunguzi wa awali tumebaini kuwa bidhaa halali za Smart Gin zinatengenezwa na kiwanda cha EuroMax Ltd cha Mabibo Dar es Salaam lakini hizo bandia zinatengenezwa na kiwanda kingine ambacho uchunguzi wake unaendelea ili kubaini mahali kilipo,” amesema kamanda huyo.

Katika tukio jingine Kamanda Bukumbi amesema kupitia msako walioufanya dhidi ya dawa za kulevya, wamemkamata mtuhumiwa Idrisa Mpalanzi (39) na wenzake watano wakiwa na kete 776 za bhangi ambazo ni sawa na gramu 412.  

Sambamba na hilo, jeshi hilo limewakamata watuhumiwa wengine saba wakiwa na mali mbalimbali zinazoaminika ni a wizi.

Bukumbi  ametaja mali hizo za wizi ambazo  zimekamatwa kuwa ni pikipiki nne (tatu aina ya Boxer na Sinoray  moja), runinga aina tofauti (11), subwoofer (5), magodoro (4), kitanda (1), komputa mpakato (3), radio (1) na spika 20,  mitungi (3) ya gesi ikiwa na majiko mawili, sofa (1) na jokofu (1) na watuhumiwa wote wamefikishwa mahakamani. 

Kamanda huyo amesema katika tukio lingine la makosa ya usalama barabarani ambapo jumla ya magari 140 yamekamatwa kwa sababu tofauti ikiwemo mwendokasi, ulevi, matumizi ya namba zisizo rasmi (3D), vimulimuli, ving’ora, pamoja na honi na taa za nyongeza.

Hata hivyo, Kamanda Bukumbi amesisitiza kuwa operesheni hiyo bado inaendelea ya kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wale wote wanaokiuka sheria za usalama barabarani.