Polisi, waganga wa jadi wajipanga kukabili uhalifu

 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe

Muktasari:

  • Kupitia vikao vya pamoja, Polisi na wagaga wa jadi wameweka mikakati kudhibiti upigaji ramli chonganishi zinazosababisha uhalifu

Bariadi. Wiki moja baada ya kuripotiwa taarifa za pacha kufariki dunia kwa madai ya kupakwa dawa ili kukuza matiti, polisi kwa kushirikiana na waganga wa jadi wamekutana kuweka mikakati ya pamoja kukomesha matukio ya namna hiyo.  

Nshola Kabadi, mama mzazi wa watoto hao, mkazi wa kijiji cha Nkololo wilayani Bariadi mkoani Simiyu anashikiliwa na polisi tangu Oktoba 4, mwaka huu kwa mahojiano kuhusiana na vifo vya watoto wake, Pendo Saku na Furaha Saku (17) waliofikwa na mauti baada ya kupelekwa kwa mganga kupakwa dawa ya kuotesha matiti ili waolewe.

Pacha hao tayari wamezikwa katika Kijiji cha Nkololo, huku msako unaendelea kumtafuta mganga wa jadi anayedaiwa kuwapaka dawa watoto hao, aliyetoroka baada ya tukio.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Oktoba 12, 2023, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe amesema kupitia vikao vya pamoja kati yao na wagaga wa jadi wameazimia kudhibiti uhalifu kwa kuweka mikakati ya kuondoa upigaji ramli chonganishi.

Amesema wamepeana mikakati ya pamoja kwamba hakutakuwa na ramli chonganishi na matukio ya ukatili wa kijinsia.

“Tumejadili na kuazimia kukataa ukatili wa kijinsia katika mkoa wetu, vikao hivi kwetu vimekuwa na manufaa makubwa tukiwekeana mikakati ya pamoja tukihakikisha Simiyu inabaki  salama,” amesema Kamanda Swebe.

Katika hatua nyingine, amesema ili kutengeneza ukaribu na ushirikiano na jamii, Polisi imeandaa mashindano kati yao na bodaboda yatakayofanyika Oktoba 14, 2023 yakilenga kuzuia, kutanzua na kubaini uhalifu kwa pamoja.

Amesema mashindano hayo yatajumuisha makundi mbalimbali katika jamii na michezo tofauti.

Katika soka, amesema timu ya Polisi itashindana na ya bodaboda; huku timu ya viongozi wa dini ikipambana na ya waganga wa tiba asili.

Wakati huohuo, amewataka wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kutumia muda uliopangwa kuhakikisha wanazisalimisha kwenye vituo vya polisi na ofisi za watendaji wa kata, mitaa na vijiji.

“Ikumbukwe kuwa silaha hizo zitapokewa katika kipindi hiki cha msamaha, hivyo watumie siku 19 (hadi Oktoba 31, 2023) zilizosalia kuzisalimisha, baada ya hapo msako mkali utaanza,” amesema.

Kamanda Swebe amesema, “Tunafahamu kuna wakazi wanaoishi maeneo ya bonde linalopakana na Hifadhi ya Serengeti wanamiliki magobole kwa hiyo kama wanazo kinyume cha sheria wazisalimishe.”