Polisi wazungumzia miili, kichwa cha mtu kukutwa mbugani
Muktasari:
- Wakati wananchi wilayani Mbarali mkoani Mbeya wakiwa na hofu kufuatia vifo vya watu watatu katika maeneo yanayodhaniwa ni hifadhi ya Ruaha, polisi wamesema vifo hivyo vimetokana na kushambuliwa na mamba na viboko.
Mbeya. Wakati wananchi wilayani Mbarali mkoani Mbeya wakiwa na hofu kufuatia vifo vya watu watatu katika maeneo yanayodhaniwa ni hifadhi ya Ruaha, polisi wamesema vifo hivyo vimetokana na kushambuliwa na mamba na viboko.
Miili ya watu hao, wakiwemo wawili wanaodhaniwa kuwa ni wa jamii ya wafugaji na kichwa cha mtu ilipatikana katika vitongoji vya Magwalasi na Ikanutwa wilayani humo.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Aprili 28, 2021 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Urlich Matei amesema miili hiyo ilikutwa pembezoni mwa mabwawa ya maji huku shingo za watu hao zikiwa zimelegea kama wamenyongwa na mmoja kikipatikana kichwa.
"Taarifa za kitabibu zinaeleza kuwa chanzo cha vifo hivyo ni kutokana na kushambuliwa na wanyama wakali katika eneo la hifadhi ya Taifa ya Ruaha wilayani humo na si kama inavyodhaniwa na baadhi ya wananchi kuwa waliuawa,” amesema.
Amewataja waliokufa kuwa ni wafugaji wawili, Salu Masanja, Ngusa Salawi na mvuvi William Estobel ambaye aliokotwa mabaki ya kichwa chake.
"Hili ni tukio kubwa kutokea mkoani hapa kama Serikali tunatoa wito kwa wananchi hususan wafugaji kuachana na tabia ya kuingia katika maeneo ya hifadhi kutokana na kuwepo kwa wanyama wakali kama viboko na mamba. Pia wachukue tahadhari katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha na kusababisha mafuriko,” amesema.
Ameonya wananchi kuachana uzushi aliodai kuwa unazua taharuki kwa jamii na kubainisha kuwa yanapotokea matukio makubwa watoe ushirikiano kwa vyombo vya dola.