Polisi yauwa majambazi wanne Dodoma
Muktasari:
- Majambazi wanne ambao hawajajulikana majina yao mpaka sasa, wameuawa na polisi wakiwa katika harakati za kunyang'anya kwa kutumia silaha.
Dodoma. Majambazi wanne wanaokadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 hadi 35, wameuawa na polisi wakiwa katika harakati za kufanya tukio la unyang’anyi kwa kutumia silaha eneo la Kisasa jijini hapa.
Majambazi hao walivamia nyumba ya Edina Joseph (41) jana saa tatu usiku kwa kuruka uzio wa nyumba yake wakiwa wamevaa barakoa kisha kufanikiwa kumnyang’anya Sh1.1 milioni, simu janja aina ya Samsung na simu ndogo tatu.
Mfanyabiashara huyo wa huduma za kifedha (wakala) mkazi wa Kisasa alivamiwa na watu hao akiwa anajiandaa kufunga mlango baada ya kumaliza shughuli zake za nyumbani.
Hayo yameelezwa leo Aprili 26, 2023 na Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma Martin Otieno wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Otieno amesema baada ya watu hao kutishia kumkata mapanga Edina alipiga kelele zilizosababisha jirani zake kutoa taarifa kwa askari waliokuwa doria eneo hilo.
“Askari walifika kwa haraka na kuwakuta watu hao ambao walijihami kwa kutaka kuwashambulia askari kwa mapanga na askari hao walijibu mapigo kwa kuwafyatulia risasi zilizowajeruhi sehemu mbalimbali za miili yao.
Hata hivyo walifariki njiani wakati wanawahishwa hospitali, hivyo kama kuna ndugu ambaye haonekani wafike hospitali ya Mkoa kwa ajili ya utambuzi wa watu hao,” amesema Otieno.