Presha yahamia kwa wakuu mikoa, wilaya

Presha yahamia kwa wakuu mikoa, wilaya

Muktasari:

  • Hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa baada ya kuwaapisha makatibu, naibu makatibu na wakuu wa taasisi aliowateua, imezidi kuwaweka matumbo joto wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi.

Dodoma. Hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa baada ya kuwaapisha makatibu, naibu makatibu na wakuu wa taasisi aliowateua, imezidi kuwaweka matumbo joto wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi.

Akizungumza jana mara baada ya kuwaapisha wateule hao, Rais Samia alisema kazi iliyobaki mbele yake ni kuteua wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi ili safu itimie na kazi iendelee kufanyika.

Alisema wakati wowote atafanya uteuzi wa viongozi hao kwa ajili ya kutimiza safu ya uongozi.

“Hivi karibuni tutakamilisha nafasi za wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri ili kusudi tukamilishe safu na kazi iende ikafanyike,” alisema Rais Samia.

Licha ya muda mfupi aliokalia kiti, Rais Samia anatajwa kuwa ni mtu asiyetabirika na anaweza kufanya lolote na kwa wakati wowote, huku akibebwa na uzoefu kwa kuwa wengi anawafahamu utendaji wao kwa karibu.

Rais Samia aliapishwa Machi 19, 2021 ikiwa ni siku mbili tangu kutangazwa kwa kifo cha aliyekuwa Rais wa tano, Hayati John Magufuli. Hata hivyo katika ipindi kifupi ameshabadilisha baadhi ya mawaziri, makatibu na wakuu wa taasisi za Serikali.

Machi 28, 2021 alianza kwa kumsimamisha kazi aliyekuwa mkurugenzi wa bandari, Deusdedit Kakoko ili kupisha uchunguza kutokana na madai ya ubadhirifu wa zaidi ya Sh3 bilioni katika sekta hiyo ulioibuliwa kwenye ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichele na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) iliyowasilishwa na mkurugenzi wake, Brigedia John Mbungo. Katika hotuba yake siku hiyo, alimnyooshea kidole aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Seleman Jafo kwamba wizara yake imejaa wizi, akamuomba aeleze kama ameshindwa ili asaidiwe, lakini siku chache baadaye alimtoa kwenye wizara hiyo na kumpelekea Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira.

Mabadiliko mengine ni kwenye baraza la mawaziri na makatibu katika baadhi ya mizara, wakiwamo wakuu wa taasisi na wakuu wa Serikali. Wakili Eliasi Machibya alisema kinachofanyika ni Rais kutimiza majukumu yake ya kikatiba ili wateule wale kiapo mbele yake, jambo alilosema ndiyo afya ya kiuongozi.

Machibya alisema kazi ya uteuzi huo pia inatakiwa kufuatwa kwa wakuu na taasisi nyingine ambazo viongozi wake huapishwa na mamlaka hiyo ya juu.