Prof Mkenda aonya wanafunzi waachwe likizo

Dodoma. Wakati Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizionya shule kuacha kuwalazimisha watoto kubaki shuleni wakati wa likizo bila kuwashirikisha wazazi, wadau wametofautiana kwa onyo hilo.

Watoto wa shule za msingi na sekondari walianza likizo ya kumaliza muhula wa kwanza iliyoanza Mei 31 na kutarajiwa kumalizika Julai 3, 2023.

Akizungumza katika viwanja vya Bunge jana, Profesa Mkenda alisema kwa shule za Serikali kuna mwongozo umetolewa na kamishna wa elimu wa siku za kufunga shule na siku za kufungua.

“Ni muhimu sana tuhakikishe wanafunzi wanapata fursa ya kupumzika. Wakuu wa shule wote na wakurugenzi wazingatie utaratibu huo,” alisema.

Alisema kwa shule binafsi, kamishna wa elimu alitoa mwanya kidogo kwamba waangalie kalenda, lakini wanaweza kufanya mabadiliko kulingana na mahitaji yao.

“Baadhi ya malalamiko tumeanza kupokea kwamba kuna shule zinazuia wanafunzi kwenda likizo bila hata kushauriana na wazazi na wengine wazazi wanatakiwa walipe kwa kuwaweka wanafunzi shuleni,” alisema.

Alitoa wito watu wasisababishe kamishna wa elimu akatoa waraka wenye masharti makali kwa sekta binafsi.

Alisema likizo zimewekwa kwa ajili ya wanafunzi kupata fursa ya kuwa karibu na wazazi wao, wapate kucheza na pia na kubadilisha mazingira.

Alisema kwa shule binafsi, kuwe na makubaliano ya hiari, siyo ya kulazimishana kuongeza muda wa watoto kubaki shuleni wakati wa likizo na wahakikishe wanatoa muda wa watoto kupumzika.


Latua mbungeni

Mbunge wa Tarime Mjini, Michael Kembaki aliomba mwongozo wa spika, huku akisema wizara hiyo imeagiza wadhibiti ubora kuzuia makambi yote ya masomo katika kipindi cha likizo, ilhali baadhi ya mikoa imepanga utaratibu wa kuongeza ufaulu kwenye maeneo yao.

“Wameagiza shule kuendelea na masomo ya ziada na hiyo itafanya wadhibiti ubora kubaki njiapanda. Watekeleze agizo la wizara au la wakuu wa mikoa,” alisema Kembaki.

Alisema katika kipindi hicho ambacho watoto wanatakiwa kufanya kazi ya ziada kuhakikisha wanafaulu, wizara inazuia walimu kufanya jitihada kuhakikisha ufaulu unapatikana.

“Ninaomba msheshimiwa Spika, wizara itupe ufafanuzi wa kutosha ni lipi lifanyike sasa kuhakikisha watoto wetu wanafaulu na wanasoma kikamilifu?” alihoji.

Akijibu, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliipa nafasi Serikali kulitolea ufafanuzi suala hilo. Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga alisema wanafunzi wanapaswa kusoma darasani siku 194 kwa mwaka kwa na vipindi vimepangwa kwa utaratibu huo.

“Kwa kuwa wakuu wa mikoa wameagiza watoto madarasa ya mitihani wabaki kwenye makambi, tuibebe hoja ili twende kulifanya kazi na kesho (leo) asubuhi tutatoa kauli na mwongozo hapa bungeni.”


Maoni ya wadau

Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Ten/Met), Ochola Wayoga, aliunga mkono agizo la Serikali, akisema kulingana na saikolojia, mwanafunzi anahitaji kupumzika.

“Serikali inakubaliana na wanasaikolojia kuwa watoto wanahitaji kupumzisha ubongo. Mtoto lazima akae nyumbani na wazazi afundishwe mambo ya nyumbani,” alisema.

Alisema umuhimu wa likizo upo pia kwa mtoto kukutana na rafiki zake kubadilishana mambo na sio kukaririshwa na masomo darasani.

“Wakati shuleni wanang’ang’ana na kukariri masomo, huku likizo wanabadilishana stori na wenzao wanaosoma shule nyingine, wanafanya mazungumzo na watu wengine na kujifunza. Akili ya mtoto ni kama sponji,” alisema.

Mmiliki wa Shule za St Anne Maria na Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza alisema wazazi hawalazimishwi, bali wanataka wenyewe watoto wabaki shule na katika jimbo lake wazazi wamekuwa wakikaa na kufanya maamuzi.

“Wanajitolea wakati wa likizo, kwenye madarasa wanaweka magodoro na wasio na uwezo wanaweka nyasi nyingi, wanaweka taa watoto wabaki pale wasome usiku na mchana waweze kufaulu,” alisema.

Rweikiza alisema anayesema hilo lisifanyike hana lengo zuri na elimu ya Tanzania.

Mdau mwingine wa elimu, Benjamin Nkonya alisema kama wazazi wanafanya hivyo kwa hiari haina shida, lakini umma uelimishwe kuwa kupumzika si mtoto kutoka darasani na kwenda nyumbani kuangalia televisheni na kuchezea simu.

“Kupumzika kwa mtoto ina maana kile walichokuwa wanafanya darasani, kumsikiliza mwalimu, kujibu maswali ya mitihani, atoke pale akafanye kitu tofauti na darasani,” alisema.

Alisema kwa mfano, mtoto anaweza kutolewa darasani na kwenda kwa mafundi samani kujifunza hesabu au hata kwenda kutembelea mbuga za wanyama kwa ajili ya kujifunza biolojia.